Ukweli ni kwamba kila mwanamke aliyetoa mimba, yaani, aliyeua mtoto wake kabla ya kuzaliwa anakabiliwa na laana. Hata kama mimba hiyo ilikuwa ndogo na changa kiasi gani. Ukubwa wa laana unatofautiana kutoka mwanamke mmoja hadi mwingine kutokana na mazingira yanayomzunguka. Lakini kama tulivyozungumza katika mada iliyopita, laana ya utoaji mimba huwapata pia wanaume [baba wa mtoto], watoto wanaozaliwa kabla au baada ya mwenzao kuuawa kwa kutolewa mimba na hata daktari au yeyote aliyehusika katika mauaji hayo. Tulisema pia kuwa laana inazikumba pia familia na hata jamii. Baadhi ya laana hizo tulizitaja kuwa ni kujisikia mkosaji, kukabiliwa na hofu, huzuni, hasira, kumbukumbu, ndoto za maono, kuharibika kwa mwenendo wa chachu mwilini, kujitenga na Mungu, aibu, n.k. Kutokana na hayo, leo tunajaribu kuwasaidia hao wanaoteseka kwa kuwaonyesha uponyaji utokanao na huruma ya Mungu. Mungu anamwalika kila atesekaye kwa laana ya utoaji mimba kwa ajili ya uponyaji. Yeye mwenyewe anatuthibitishia hilo kama tusomavyo katika Injili ya Mathayo:
“Njoni kwangu ninyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo nami nitawapumzisha” (Mt.11:28)
Hatua za kuchukua ili mwanamke aliyetoa mimba apate uponyaji:
Andika barua kueleza jinsi ulivyoumizwa
Tendo la utoaji mimba hufanywa na mwanamke na daktari/mtu anayehusika. Lakini kabla ya kufikia uamuzi wa kutoa mimba, mwanamke hupata ushauri au ushawishi wa watu mbalimbali – mume, mchumba, ndugu, rafiki, jirani. Hata fedha za kulipia mauaji hayo, pengine hutolewa na hao niliowataja. Lakini baada ya tendo la utoaji mimba yanafuata mateso na masumbuko, na mwanamke aliyetoa mimba anaathirika zaidi. Kwa hiyo, ni vizuri kila mwanamke aliyetoa mimba kuandika barua kueleza jinsi alivyoumizwa na tendo la utoaji mimba. Katika barua hiyo, mtaje aliyekuumiza au waliokuumiza; eleza jinsi ulivyoumizwa; na jinsi maisha yako yalivyobadilika kutokana na tendo la utoaji mimba ulilofanya.
Rejea tendo lako la utoaji mimba (matendo haya yafanyike wakati kila mwanamke aliyetoa mimba akiwa amefumba macho na kuinamisha kichwa)
Kubali kwamba umemwua mtoto wako ambaye ulipaswa kumpokea, kumpenda na kumlinda
Kwa vile mtoto huyo amekufa, basi kama ilivyo desturi yetu, unatakiwa uweke msiba [wa kiishara]
Katika misiba, wafiwa hulia, nawe chukua nafasi hii kumlilia mtoto wako; ikibidi mtolee machozi
Msiba hukusanya ndugu na majirani katika huzuni na maombolezo, [kwa njia ya ishara]; hebu weka msiba ili watu wajue kuwa kuna mmoja katika familia yako amefariki
Katika kila msiba watu wanasali na kuimba nyimbo za maombolezo. Kwa njia ya ishara fikiria kuwa watu wamekusanyika na unawaalika wasali pamoja nawe na kama kuna kikundi cha kwaya, basi kiimbe.
Kujipatanisha na Mungu
Leta katika taswira kisa cha “Baba Mwenye Huruma” au huko nyuma tulizoea kuita “Mwana Mpotevu ” (Lk.15:11-32). Katika kutoa mimba, mtoaji mimba anakuwa amejitenga mwenyewe na Mungu na Kanisa. Ni dhambi ya mauti inayoondoa sura na mfano wa Mungu katika roho yako, kama tunavyoelezwa katika kisa cha Kaini kumwua nduguye Abel; ni dhambi inayodai kisasi: “Hakika damu ya uhai wenu nitaitaka hesabu yake… Anakayemwaga damu ya mwanadamu, damu yake huyo itamwagwa na mwanadamu; maana kwa mfano wake Mungu alimfanya mwanadamu” (Mwa.9:5-6).
[KKK 2259-2261]
Na kwa kadiri ya adhabu ya kikanisa, mtu yeyote aliyetoa mimba anakuwa amejitenga mwenyewe na ushirika wa kanisa [latae sententiae]
Kwa hiyo yawezekana mwanamke aliyetoa mimba akajisikia vibaya kushiriki ibada mbalimbali za kanisa, na pengine kufikia hatua ya kukata tamaa kwamba hawezi kuijongea sakramenti ya upatanisho. Basi katika hali hiyo, chukua hatua zifuatazo kama alivyofanya yule Mwana Mpotevu: tambua kosa ulilotenda; zingatia (tafakari uzito) moyoni kosa ulilotenda; weka dhamira ya kuondokana na dhambi hiyo; kujutia na kutubu makosa hayo (Baba nimekosa juu ya mbingu na mbele yako).
Ukikamilisha hatua hizo, mshukuru Mungu kwani amepokea maombi yako naye atakusamehe.
Kujipatanisha na wengine
Rejea barua uliyoandika kwa wale waliokuumiza.Miongoni mwa hao ni mume, mpenzi wako wa kiume, ndugu yako, rafiki yako, daktari, mama yako mzazi, baba yako mzazi, na wengine wengi. Hao wote wamekujeruhi, wamekubadilisha fikra zako, wametonesha majeraha ya moyo wako, wamekuharibia maisha na hata afya yako. Weka dhamiri ya kuwasamehe wote hao. Ikiwezekana katika barua ile uliyowaandikia, waambie kuwa umewasamehe bila masharti, tena umewasamehe na kusahau. Katika barua ile, mtaje kwa jina yule unayetaka kumsamehe. Unaweza kuwaomba wakuandikie wakueleze kama wamekubali msamaha wako.
Kujisamehe mwenyewe
Napenda nikuhakikishie kuwa hakuna jambo gumu katika maisha yetu kama kujisamehe sisi wenyewe. Tumeshuhudia baadhi yetu wakijinyonga, wengine wakiishia kwenye ulevi wa pombe na dawa za kulevya, wengine wanajiingiza katika vitendo vya uasherati wakitaka kufidia hali fulani iliyopotea, wengine wamejikuta wakipata mimba nyingine mara baada ya kutoa mimba ili kufidia pengo. Ili uweze kujisamehe fuata kanuni zifuatazo:
Lipeke umivu hilo kwa Yesu, Mungu mkombozi wetu, kwani yeye alituahidi akisema;
“Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu, kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu. Kwa maana nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi” (Mt.11:28-30).
Mwambie Mungu juu ya yule aliyekuumiza. Jambo hilo litakuwa mwanzo wa kupona kwako.
Amua kuwa huru. Tendo hili linakudai ama kuimarisha uhusiano wako na wengine au kuvunja. Jambo hili ni gumu linapohusu ndugu au marafiki wetu wa kudumu, lakini ikifikia wakati wa kufanya uamuzi kwa ajili ya uponyaji, basi fanya kwa kadiri Mungu anavyokuelekeza. Unachofanya ni kumpelekea Mungu uhusiano wenu, uwe mzuri au mbaya, yeye atajua namna ya kushughulikia
Jishughulishe na jambo fulani litakalokuletea faraja moyoni na kukusahau machungu yanayokukabili. Najua umetoa msamaha kwa wale waliokuumiza, lakini ili msamaha utendeke katika ukamilifu wake unahitaji muda, siyo tendo la siku moja au juma moja, laweza kuwa tukio la maisha yako katika miaka mingi ijayo. Unaweza kuamua kusali kila jioni ukiwaombea wale waliokuumiza; unaweza kujihusisha na vikundi vya malezi ya watoto yatima; au kuwatembelea wagonjwa hospitalini; unaweza pia kuamua kuwapigia simu au kuwaandikia barua pepe waliokuumiza ukiwajulia hali na kuwashirikisha furaha yako ya siku hiyo.
Weka mipaka katika kutekeleza hayo niliyosema hapo juu. Yawezekana wengine watakasirika ukiwasiliana nao kwa simu. Wakati mwingine ukimya na tafakari vyaweza kukusaidia kufungua moyo.
Mpe Mungu shukrani. Mungu ni mwema mwenye kumsamehe kila amwendeaye kwa toba ya kweli. Mfalme Daudi alisamehewa dhambi yake baada ya kumlilia Mungu. Katika kumwendea Mungu, pia uwe na moyo wa shukrani kwa yale aliyokujalia katika maisha yako. Mshukuru hata kwa zawadi ya watoto ulio nao, mshukuru kwa kazi unayofanya, mshukuru kwa kupata mume mwema, na hata pale anapokupatia mume mkorofi mshukuru kwani ana sababu ya kufanya hivyo, anataka kwa njia yake uuelekee utakatifu. Daima kumbuka neema na baraka za Mungu hububujika kwetu bure ili mradi tumtafute kwa nia njema.
Uwe na matumaini ya kupona. Siri ya kupona na siri ya mafanikio katika maisha yetu ni moyo wa matumaini. Matumaini yanapotanguliwa na imani na mapendo, matunda ya kiroho huwa dhahiri kwetu.
Kujipatanisha na mtoto (watoto) uliyemwua
Daima ukumbuke kuwa tendo la kumwua mwanao linaambatana na udunishwaji wa binadamu, ugumu wa moyo na ukatili uliopea. Umeharibu mpango wa Mungu wa uumbaji kama yasemavyo maandiko: “Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujtoka tumboni, nalikutakasa, nimekuweka kuwa nabii wa mataifa” (Yer.1:5); “Je, mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe”? (Isa.49:15) “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa kuwa watu kama hao ufalme wa Mungi ni wao”? (Lk.18:16)
Jee utawezaje kujipatanisha na mtoto ambaye hayupo? Fanya yafuatayo:
Fikiria huyo mtoto umemzaa na unaye
Mkaribishe mtoto huyo maishani mwako ukisema ‘asante Mungu kwa zawadi hii ya mtoto mzuri’
Mshike mikononi mwako ili aonje ukarimu wa mama
Fikiria analia, basi mbembeleze ili aonje huruma ya mama
Mwongeshe na kumvika nguo ili aonje upendo wa mama
Mnyonyeshe ili aonje utamu wa maziwa ya mama
Kama ilivyo desturi katika imani mbalimbali, mpatie mtoto ubatizo wa kiimani ili aungane na wenzake katika ushirika na Kristo
Kwa vile mtoto huyu umemwua na hakupata mastahili yake ya mazishi ya heshima, basi unatakiwa sasa mzike kiishara kama ifuatavyo:
Mchimbie kaburi
Mnunulie sanda
Mchongee jeneza zuri na lipambe kama ilivyo desturi yetu
Laza mwili wa marehemu katika jeneza hilo kisha lifunge
Chukua jeneza na nenda mahali ulipochimba kaburi
Mzike mtoto wako kwa heshima zote kwa kadiri ya imani yako
Kwa vile huko nyumo uliweka msiba, ukalia na kuomboleza pamoja na wenzako, basi sasa anua matanga, ikimaanisha kuhitimisha msiba
Vunja ukimwa
Jambo moja gumu kulitekeleza kwa kila aliyetoa mimba ni kuwajulisha ndugu wa familia juu ya tendo lililofanyika la utoaji mimba. Yawezekana katika familia, mama akatoa mimba na asiwajulishe watoto wake waliosalia na hata mume wake. Yawezekana pia mke na mume wakashirikiana kutoa mimba, mume akatoa pesa au akamsindikiza mke wake kwa mwuaji. Wakati mwingine mama anampeleka binti yake katika tendo la utoaji mimba bila mume wake kufahamu. Au pengine, binti anaweza kuwa alitoa mimba katika umri wa usichana na baada ya kupata mume asimshirikishe mume wake tendo hilo. Inakuwa mbaya zaidi pale mke aliyetoa mimba kabla ya kuolewa anapopata matatizo ya kutozaa kutokana na kuharibika kizazi au kutolewa kizazi kulikosababishwa na utoaji. Katika ndoa hiyo yatazuka matatizo, na pengine hata kupelekea kuvunjia ndoa yenyewe. Kuvunja ukimwa ina maana kuwa mwanamke yeyote aliyetoa mimba, kama kweli anataka kupata uponyaji wa ndani inampasa kuwaeleza wanafamilia jambo hilo. Mama wa ndoa amweleze mume na watoto wake ili wafahamu kuwa walikuwa na ndugu yao mwingine ambaye hawanaye sasa. Na hata katika kuhesabu idadi ya watoto, mama huyo aseme kwamba ana watoto 5, wanne wako hai na mmoja amefariki. Hilo likifanyika, basi mama huyo atakuwa amejijengea mazingira ya amani ya moyo katika ndoa yake na familia yake. Kwa binti anayetaka kuolewa, kama alikwishakutoa mimba katika usichana wake, sharti amweleze huyo mchumba wake kuwa aliwahi kutoa mimba, hivyo kwamba anaingia katika ndoa akiwa mwenye amani, kama huyu mchumba atamsamehe na kumkubali. Ikiwa kuvunja ukimwa kutasababisha kutofungwa kwa ndoa, hilo litakuwa jema zaidi.
Sala
Kila mwanamke aliyetoa mimba asisahau sala. Sala ina nguvu kubwa, tena ina sifa ya uponyaji.Sali sala sa masifu, shukrani na maombi. Iko mifano mingi ya sala na kila mmoja asali kulingana na imani yake.