Hivi sasa kuna kampeni kubwa ya kuwahamasisha wanawake kutumia vidhibiti mimba hapa nchini kwetu. Hali hiyo inatokana na hofu kuwa ongezeko la idadi ya watu ni kubwa ukilinganisha na uwezo wa serikali kuwahudumia watu hao. Mkutano uliofadhiliwa na Melinda Gates na serikali ya Uingereza na kufanyika nchini Uingereza Juni 2012 ulikuwa na lengo la kuongeza matumizi ya vidhibiti mimba kwa wanawake milioni 120 katika nchi za Afrika na nchi za Kusini mwa Asia. Mkutano huo ulidhamiria kukusanya dola za Kimerakani bilioni 4 ambazo zitatumika katika kufadhili kampeni hiyo. Viongozi kadhaa wa Kiafrika walialikwa na kushiriki mkutano huo. Viongozi hao walisifia mpango huo na kila aliyetoa hotuba alieleza umuhimu wa kutumia vidhibiti mimba kwa watu wa nchi zao na kuomba kupatiwa ufadhili ili kutekeleza azma hiyo.
Ni kwa msingi huo, kampeni kubwa hapa Tanzania imeanzishwa ikiratibiwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na mashirika ya hiari ya nje na ndani ya nchi. Hivi karibuni katika mkutano uliofanyika hapa Dar es Salaam na kuhudhuriwa na washiriki wapatao 450 kutoka ndani na nje ya nchi, kampeni ya Nyota ya Kijani ilizinduliwa upya na kutoa wito kwa wanawake kuchangamkia huduma za uzazi wa mpango. Katika kuzindua kampeni hiyo, watetezi wa matumizi ya vidhibiti mimba walihusisha vidhibiti mimba na faida zifuatazo:
Kwamba matumizi ya vidhibiti mimba yanapunguza vifo vya akina mama na watoto. Je ni kweli?
Umoja wa Mataifa katika kutekeleza Malengo ya Milenia 2000 - 2015, azimio la 4 na 5 linahusu kupunguza vifo vya watoto na kuimarisha huduma za mama waja-wazito. Azimio linasema kufikia 2015 kila nchi ihakikishe kwamba vifo vya watoto chini ya miaka 5 viwe vimepungua kwa kiwango cha theluthi mbili na vifo vya mama waja-wazito vipungue kwa kiwango hichohicho.
Hali ya sasa wanawake na wasichana 287,000 hufa kila mwaka kutokana na sababu zinazohusiana na uja-uzito, asilimia 99 kati yao ni wale wa nchi zinazoendelea. Kwa kadiri ya takwimu kutoka Shirika la Afya Duniani, (WHO) mwanamke 1 kati ya 3,800 hufa katika nchi zilizoendelea wakati 1 kati ya 39 hufa katika nchi zinazoendelea.
Sababu ya vifo hivyo ni
Kutoka damu nyingi [hasa baada ya kujifungua]
Maambukizo ya magonjwa [tena baada ya kujifungua]
Mkandamizo wa damu wakati wa uja-uzito [kifafa cha mimba]
Utoaji mimba usio salama.
NB: Kwa bahati mbaya hakuna utoaji mimba ulio salama kwani katika tendo la utoaji mimba, mtoto anauawa, mama anaumizwa kimwili na kisaikolojia na daktari, licha ya kulipwa, anapata madhara ya kisaikolojia.
Vingi ya vifo hivi vingeweza kuepukwa kama huduma za afya wakati wa uja-uzito zingepatikana. Magonjwa sita yanayosababisha vifo vingi kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 5 ni
Hali ya mtoto baada ya kuzaliwa na kabla ya kufikisha siku ya 28; (watoto wanaozaliwa kabla ya muda; kifafa cha mimba; uambukizo; pepo punda [tetanus]) huchangia kwa asilimia 37
Kichomi kikali; huchangia asilimia 19
Kuharisha; huchangia asilimia 18
Malaria; huchangia asilimia 8
Homa kali itokanayo na maambukizo ya vijidudu; huchangia asilimia 4
UKIMWI; huchangia asilimia 3
Utatuzi kwa vifo vya akina mama waja-wazito
Kuzuia mimba kwa kuweka mpishano wa uzao, [ingawa sioni kama huu ni utatuzi unaoendana na matatizo yaliyotajwa]
Upatikana wa huduma nzuri za wakungu wakati wa kujifungua
Upatikanaji wa huduma za dharura wakati wa kujifungua, kama vile upasuaji na upatikanaji wa damu
Uhamasishaji wa haki za wanawake, [kama vile haki za kijinsia, sioni uhusiano wake na matatizo yaliyotajwa]
Utatuzi kwa vifo vya watoto walio chini ya umri wa miaka 5
Upatikanaji wa chanjo
Kuzuia na kutibu kichomi, kuharisha, malaria na ukimwi
Kuzuia na kutibu hali zitokanazo na kizazi; kama vile huduma nzuri baada ya kujifungua, huduma nzuri wakati wa kujifungua, huduma bora kwa watoto waliozaliwa
Kuzuia na kutibu utapia mlo
Kwamba matumizi ya vidhibiti mimba yanapunguza vitendo vya utoaji mimba. Je ni kweli?
Hii ni hoja inayoleta mkanganyiko mkubwa kati ya watetezi wa vidhibiti mimba na wanaopinga matumizi ya vidhibiti mimba.
Baraza la Maaskofu Katoliki la Marekani katika taarifa yake kwa umma linasema matumizi makubwa ya vidhibiti mimba hayapunguzi vitendo vya utoaji mimba wakitoa hoja zifuatazo:
Katika matumizi yake ya kawaida vidhibiti mimba hushindwa kuzuia mimba. Katika miezi 12 ya kwanza ya matumizi ya vidhibiti mimba, 16.4% ya wasichana wanapata uja-uzito. Kama msichana anaishi tu na mshikaji, kiwango cha kushindwa hufikia 47%. Miongoni mwa wasichana wa kipato cha chini kiwango cha kushindwa ni 48.1% kwa vidonge vya majira na 71.7 kwa kondomu. Asilimia 48 ya wanawake waliopata mimba bila matarajio walitumia vidhibiti mimba na asilimia 54 ya wanawake waliotaka huduma za kutoa mimba walikuwa wanatumia vidhibiti mimba. Wakimnukuu mtaalamu wa vidhibiti mimba James Trussell wa Princeton wanasema vidonge vya majira ni njia ya zamani kwani haifanyi kazi inavyopaswa na ni vigumu kwa wanawake kuzingatia kanuni za kumeza kidonge kila siku. Ndiyo maana serikali zinahimiza matumizi ya vidonge vya tahadhari “emergemcy contraception” kama kinga mbadala.
Tafiti zinaonyesha kuwa upatikanaji wa vidhibiti mimba haupunguzi mimba zisizotarajiwa na utoaji mimba. Kuongezeka kwa matumizi ya vidhibiti mimba kunajenga usalama bandia na kupelekea watoto kujiingiza katika vitendo vya ngono katika umri mdogo na kuwa na wapenzi wengi kingono, mambo yanayochochea upatikanaji wa mimba. Utafiti uliofanyika huko Hispania kati ya 1997 na 2007 na kutolewa katika jarida la “Contraception”, Januari 2011 lilionyesha kuwa asilimia 63 ya matumizi ya vidhibiti mimba yalishabihiana na asilimia 108 ya ongezeko katika vitendo vya utoaji mimba.
Mnamo Julai 2009 yalichapishwa matokeo ya utafiti uliofanyika katika vituo 54 uliofadhiliwa na Wizara ya Afya ya Uingereza kwa ajili ya kupunguza mimba za utotoni kupitia masomo ya elimu ya ngono na ushauri kuhusu uzazi wa mpango kwa watoto wenye umri wa miaka 13-15. Hakuna ushahidi uliopatikana ukionyesha kucheleweshwa kwa vitendo vya ngono or kupungua mimba. Wasichana walioshiriki katika programu hiyo walitoa taarifa kuwa walipata mimba kwa kiwango cha asilimia 16 ukilinganisha na waliokuwa nje ya programu hiyo ambao walipata mimba kwa kiwango cha asilimia 11 na kwamba walikuwa wameshiriki vitendo vya ngono kwa kiwango cha asilimia 58 ukilinganisha na asilimia 33 ambao hawakushiriki programu hiyo.
David Paton, mwandishi nguli katika masuala ya idadi ya watu na vidhibiti mimba anasema hajaona ushahidi kwamba matumizi ya vidhibiti mimba yanapunguza mimba za utotoni au viwango vya utoaji mimba. Akifanya majumuisho katika utafiti uliofanyika Uingereza anasema kwamba ni wazi kuwa matumizi ya vidhibiti mimba, kinyume na hoja kwamba yanapunguza viwango vya mimba, badala yake viwango vya mimba vimeongezeka. Naye K. Edgardh aligundua kuwa licha ya ushauri juu ya matumizi huria ya vidhibiti mimba, uuzaji wa kondomu na vidonge vya majira kwa bei nafuu na upatikanaji wa viua-mimba [emergency contraception], viwango vya mimba za utotoni huko Sweden viliongezeka kutoka asilimia 17 hadi 22.5 kati ya 1995 na 2001.
Maaskofu hao wakitumia taarifa za tafiti 23 zilizotolewa na timu ya James Trussell kati ya 1998 na 2006 katika Chuo Kikuu cha Princeton zikionyesha ulinganifu wa matumizi ya viua-uhai [emergency contraceptives] na kuwepo kwa mimba zisizotarajiwa na utoaji mimba, wanasema hakuna hata moja kati ya tafiti hizo 23 ulioonyesha kupungua kwa mimba zisizotarajiwa au utoaji mimba. Angalia taarifa hizo katika mtandao huu, "Fact Sheet: Emergency Contraception Fails to Reduce Unintended Pregnancy and Abortion."
Kwa upande mwingine katika utafiti uliofanyika kati ya 1991 na 1995, kwa vijana kati ya miaka 15 na 19 ilionekana kuwa kupungua kwa vitendo vya ngono miongoni mwa vijana hupunguza mimba za utotoni na vitendo vya utoaji mimba. Nacho kituo cha kudhibiti magonjwa cha Marekani, [US Centers for Disease Control] kilitoa taarifa kuwa kutoka 1991 hadi 2001, asilimia 53 ya kupungua kwa mimba kulitokana na kupungua kwa vitendo vya ngono miongoni mwa vijana.
Huko Uganda, mafanikio makubwa ya kupungua kwa viwango vya maambukizo ya virusi vya ukimwi yanatoa fundisho kuwa kupungua kwa vitendo vya ngono ndiko kunaleta faida katika kupungua kwa mimba zisizotarajiwa na mimba miongoni mwa vijana. Programu za kuacha zinaa na kuwa mwaminifu kwa mwenzi asiyeambukizwa zimethibitisha kuwa na matokeo mazuri katika kuzuia maambukizo.
Watetezi wa vidhibiti mimba
Kwa upande mwingine, watetezi wa vidhibiti mimba wanadai kuwa matumizi huria ya vidhibiti mimba yanapunguza vitendo vya utoaji mimba, kwa kadiri ya taarifa ya Associated Press iliyochapishwa Oktoba 05, 2012. Lakini matokeo ya tafiti hizi yanatolewa kwa ajili ya kukidhi lengo fulani fichika. Kwa mfano huko Marekani, matokeo ya tafiti hizi yanatolewa ili kuhalalisha mpango wa Obama wa kulazimisha huduma za vidhibiti mimba kutolewa katika hospitali zote nchini humo kama sehemu ya huduma za afya. Mpango huo unazilazimisha hata hospitali na taasisi za dini ambazo zina msimamo tofauti kuhusu matumizi ya vidhibiti mimba.
Na hata hapa kwetu watetezi wa vidhibiti mimba wanaeleza uzuri wa matumizi ya vidhibiti mimba kwa sababu wana agenda ya siri, yaani, maliopo wanayopata kutokana na kusema uwongo huo kwa lengo la kupunguza ukuaji wa idadi ya watu. Kwa hiyo zinatolewa takwimu kuthibitisha kwamba matumizi ya vidhibiti mimba yanaleta faida kwa mtumiaji, familia na hata taifa. Kwa kawaida, kampeni za matumizi ya vidhibiti mimba, hayasemi ukweli kuhusu madhara yanayotokana na vidhibiti mimba, au hata kama utasemwa, basi ni kwa kufinyangwafinyangwa ili mradi lengo la hila linaloambatana na programu hizo linabakia kutoeleweka vizuri kwa watumiaji.
Lakini tutafakari kidogo jambo hili, kama matumizi ya vidhibiti mimba yanapunguza vitendo vya utoaji mimba, inakuwaje basi, kule ambako matumizi ya vidhibiti mimba yamekuwa makubwa sana kwa miaka mingi ndiko kulekule sheria za utoaji mimba zimetungwa? Karibu nchi zote za Magharibi zimetunga sheria za kutoa mimba, kwa nini basi wasingesema hawana haja ya kutunga sheria za kutoa mimba kwani matumizi ya vidhibiti mimba yanatosheleza. Hapa tunapata jambo jingine ambalo limejificha katika falsafa ya watetezi wa vidhibiti mimba, kwamba vidhibiti mimba na utoaji mimba ni vitendo mapacha, na kwa kweli, ndani ya vidhibiti mimba ndimo ilimo mizizi ya utoaji mimba. Kimsingi mtumiaji vidhibiti mimba anajenga katao dhidi ya uzazi na uhai mpya, kwa hiyo ni rahisi kwake kuua uhai mpya kwa sababu hakuupenda tangu akilini mwake. Kwa hiyo vidhibiti mimba ni viashiria vya vitendo vya utoaji mimba. Na vidhibiti mimba vingine vinatengenezwa mahususi kwa ajili ya kuharibu mimba changa.Watetezi wa vidhibiti mimba wanaongopa kuwa eti vinapanga uzazi. Tukumbuke kuwa kila palipo na kampeni kubwa ya matumizi ya vidhibiti mimba ndipo hapohapo sheria za kutoa mimba hutungwa. Kwa hiyo, tusije tukashangaa kwamba, baada ya kampeni hii kubwa ya matumizi ya vidhibiti mimba inayobeba jina ‘NYOTA YA KIJANI’ hapa nchini kwetu, inayoratibiwa na serikali yetu, miaka michache ijayo tutashuhudia serikali hii hii inayohamasisha kampeni hii itatunga sheria ya kutoa mimba. Huu ni ukweli wa kihistoria.Kwa hiyo yeyote anayesema matumizi ya vidhibiti mimba yanapunguza vitendo vya utoaji mimba ni mwongo, asiyepaswa kuaminika.
Mikakati ya kupunguza vifo vya watoto wachanga katika nchi zinazoendelea: tunajifunza nini kutoka historia ya nchi zilizoendelea za magharibi?
Miondoko ya kupunguza vifo vya watoto wachanga katika nchi zilizoendelea
Mnamo miaka ya 1870 uwiano wa viwango vya vifo vya watoto wachanga katika nchi zilizoendelea ulikuwa zaidi ya 600 katika kila watoto 100,000. Kwa mfano nchi za Sweden, USA, Uingereza na Wales zinaonyesha viwango tofauti katika kupunguza vifo hivyo. Viwango vya Sweden vilianza kupungua tangu 1870, kufikia vifo 250-300 katika kila watoto 100,000 kuelekea mwanzoni mwa karne; wakati huo huo viwango vya Uingereza na Wales vilikuwa bado vya juu 400-450, na kwa Marekani vilikuwa 600-800, viwango vilivyobaki kwa miongo minne. Lakini vilipungua kwa kasi kati ya 1937 kuelekea miaka ya 1960 na ndipo nchi hizo zikafikisha viwango vya sasa vya vifo 10 katika kila 100,000.
[Evolution of maternal mortality in Sweden, U.S.A. and England & Wales from 1870 to 1993. Sources: Howard 1921, Högberg et al. 1986, Högberg et al. (1986); Loudon 1992a, WHO (1996)]. Sweden
Katika nusu ya kwanza ya karne ya 18 Sweden ilikuwa nchi maskini na idadi ya watu wake ilikuwa ndogo na iliyotawanyika sana kimakazi. Utambuzi wa awali wa tatizo la vifo vya watoto wachanga liligundulika kwa sababu kuanzia 1749 na kuendelea Sweden ilikuwa na utaribu wa kuweka kumbukumbu za afya za kila mkazi katika ngazi ya parokia kwa kuorodhesha vizazi na vifo. Kutokana na utaratibu huo Kamisheni ya Afya ya Sweden (Sundhtskommissionen) iliweza kubaini kuwa vifo vingi vingeweza kuepukwa kama kungekuwa na wakunga wengi (Högberg et al. 1986).
Mamlaka za Afya zilitengeneza sera za kuwa na mafunzo ya wakunga wengi ili kuhakikisha kwamba wataalamu wanapatikana wa kuhudumia mama waja-wazito wanaojifungulia majumbani. Huo ulikuwa uamuzi wa busara na matokeo yalikuwa makubwa kutokana na utashi wa kisiasa. Mnano 1861 wakunga waliweza kuhudumia 40% ya mama wote waliojifungua. Kufikia 1900 idadi yao iliongezeka na kufikia 78%, na idadi ya wakunga wa jadi waliohudumia akina mama wanaojifungua ilipungua kwa viwango vya 60% mnamo 1861, 18% mnamo 1900. Huduma za wakunga waliosomea zilisaidiwa na madaktari ambao waliitwa kama kulikuwa na matatizo wakati wa kujifungua na waliwajibika kwa kuweka kumbukumbu za taarifa za vifo na vizazi. Idadi ya watoto waliozaliwa hospitalini ilikuwa kati ya 2% na 5%.
Vilevile mbinu za mpya zilianzishwa na wakunga wote [wataalamu] waliruhusiwa kutumia huduma hizo mahospitalini wakati wa kuwahudumia wanawake wanaojifungua tangu mishoni mwa miaka ya 1870, na kufikia 1881 kila mkunga alikuwa na ujuzi wa kutumia vifaa hivyo vipya. Ni njia hizi za kutumia utaalamu kwa wanawake waliojifungulia majumbani na matumizi ya vifaa vipya ndizo ziliwezesha Sweden kupata mafanikio makubwa katika kukabiliana na vifo vitokanavyo na uzazi amapo vilifikia 228 kwa kila 100 000 kufikia mwanzoni mwa karne ya 20 (Högberg et al. 1986).
Kwa kifupi tunaweza kusema kuwa mafanikio ya Sweden akatika kupunguza vifo vya watoto wachanga vilitokana na:
Utashi wa kisiasa
Matumizi ya mbinu na vifaa vya kisasa
Huduma bora iliyotolewa na wataalamu
Mafanikio yalionekana zaidi baada ya nchi nyingine kuiga – Uholanzi, Denmark na Norway ambazo zilipunguza vifo kufikia chini ya 300 kwa kila 100,000 kufikia 1920 (Loudon 1992b).
Uingereza na Wales
Huko Uingereza na Wales vifo vya watoto wachanga vilipungua kati ya 1850 na 1900 kutoka 600 kwa kila 100,000 kufikia 450-500 kwa kila 100,000 na viwango hivyo vilibaki hadi miaka ya 1930. Utambuzi wa tatizo ulitokea baadaye kuliko ilivyokuwa Sweden. Mnamo 1928 kamati maalumu iliyoundwa na Wizara ya Afya ilitoa kauli-mbiu ‘huduma msingi inawezekana’ na kuagiza kufanyika uchunguzi wa siri kwa kila kifo cha watoto wakati wa kujifungua. Mnamo 1932 Wizara ya Afya ilipeleka ujumbe Denmark, Uholanzi na Sweden kujifunza namna nchi hizo zilivyofanikiwa. Utambuzi wa tatizo uliwezesha kulifanya jambo la vifo vitokanavyo na uzazi kama agenda muhimu katika miaka ya 1930. Mnamo 1938 ulifanyika mkutano nchini Uingereza uliohudhuriwa na wanawake kutoka mashirika 60. Hata hivyo utaalamu katika masuala ya huduma kwa akina mama ulikuwa wa polepole. Wakunga wengi walikuwa bado hawajapatiwa mafunzo maalumu hadi karne ya 19. Sheria ya Wakunga ya 1902 ililenga kuwatumia wakunga waliosomea badala ya wakunga wa jadi ambao walionekana kutokuwa na utaalamu wa kutosha. Sheria hiyo ilifanya mafunzo ya ukunga kuwa ya lazima
Mnamo 1929, Vyuo vya ‘Royal College of Obstetricians na Gynaecologists’ vilianzishwa kwa lengo la kutoa huduma nzuri zaidi kwa akina mama waja-wazito. Kutokana na hiyo mnao 1935 vifo vya vya watoto wakati wa kujifungua vilianza kupungua. Ulikuwa mwaka 1949 taarifa za siri kuhusu vifo vya watoto wakati wa kujifungua vilionyesha kuwa zipo sababu nyingine, licha upungufu wa huduma za wakunga. Waligundua kuwa vifo vingi vingeweza kuepukwa kama wangetumia huduma za kudhibiti magonjwa na kutoa tiba. Kutokana na ujuzi huo na msukumo kutoka kwa jamii mfumo mpya katika utoaji wa huduma ulianzishwa, yaani kuboresha huduma za kudhibiti kutoka wa damu, matumizi ya vifaa vya ganzi, na huduma za dharura za upasuaji. Kutokana na huduma hizo vifo vilipungua kutoka 80 hadi to 25 kwa kila 100 000 kati ya 1950 na 1965 (Llewellyn-Jones 1974). Marekani
Kuduma za afya kwa wanawake waja-wazito zilichelewa na takwimu zake zilipatikana miaka ya 1920. Katika miji mingi viwango vya vifo vilikuwa vikubwa zaidi kuliko vile vya Sweden na Uingereza. Kwa mfano 1918, viwango vya vifo wakati wa kujifungua vilikuwa 885 kwa kila 100,000, vikiwa ni vya juu zaidi kuliko ilivyokuwa Sweden karne moja kabla yake. Utambuzi wa matatizo ulitokea katika miaka ya 1920 baada ya kuanzishwa ‘National Maternal Welfare Committee’. Lengo la kamati hii lilikuwa kuhamasisha utafiti wa vifo wakati wa kujifungua katika kila jimbo, mtaa na jumuia na kujaribu, kama inawezekana, kuzuia vifo hivyo kwa kuwaelimisha watu, wahudumu mahospitalini, jumuiya na wataalamu wa afya (Llewellyn-Jones 1974).
Uelewa wa tatizo ulipata msukumo kwa kuanzisha mchakato wa kuzuia vifo kwa kuhamasisha huduma kwa akina mama wakati wa kujifungua kisheria , kwa sheria iliyojulikana kama ‘Sheppard-Turner Act’, kati ya 1922 na 1929; Social Security Act 1935) (Schmidt & Valadian 1969). Wataaamu wa afya wa Marekani walijaribu kuhusisha vifo vya watoto wakati wa kujifungua na tabia za wanawake waja-wazito na huduma za wakunga na waganga. Na taarifa ya 1933, iliyoundwa na kamati iliyojulikana kama ‘Public Health Relations Committee’ ya Chuo cha Uganga cha New York [New York Academy of Medicine] ilitolewa ikionyesha kuwa 66% ya vifo vingeweza kuepukwa kama ‘huduma kwa mama zingekuwa nzuri katika hali zote’ (Porges 1985). Na mbaya zaidi, utafiti uligundua kuwa 61% ya vifo 1343 vilihusishwa na uzembe wa madaktari katika kutoa huduma ya ganzi, kutumia vifaa visivyotakiwa vya kuzalishia, hasa upasuaji, wakati 2% na 37% zilihusishwa na tabia ya wakunga na waja-wazito. Hatua muhimu katika kukabiliana na vifo vya watoto na akina mama wakati wa kujifungua
Awamu ya kwanza: kutambua ukubwa wa tatizo kwa kukusanya takwimu ambavyo vilifanyika katika karne ya 19 na kulikabili tatizo; na kwa kuanzisha na upatikanaji wa mbinu bora za ukunga (kwa mfano matumizi ya vifaa vilivyochemshwa), ambavyo vilitumiwa vizuri. Hii ilimaanisa kuzingatia utaalamu katika utuaji wa huduma za ukunga na nchi zilizofanikiwa kwa kiwango kikubwa zilikuwa Sweden, Uholanzi na Denmark
Awamu ya pili: ni kipindi cha 1900 – 1937 kilihusisha matumizi ya mbinu bora zaidi, yaani matumizi ya dawa za moto [antibiotics], upasuaji na uongezaji damu. Viwango vya utoaji huduma vilikuwa bora na vilizingatiwa kawa wanawake wote. Hizi ndizo mbinu ziliwezesha kupungua vifo vitokanavyo na uzazi [watoto na waja-wazito]
Je, hali ikoje hapa kwetu Tanzania?
Undugu, kufahamiana na rushwa ni vigezo vya kupata huduma za afya na uzazi
Matusi na hata kipigo kutoka kwa wakunga ndiyo huduma wanayopata akina mama wakati wa kujifungua
Akina mama waja-wazito wanatakiwa kwenda hospitali na vifaa vyao vya kujifungulia
Baadhi ya akina mama katika baadhi ya vituo vya afya wanaachwa bila kushughulikiwa kiasi kwamba wengine wanajifungua bila kuwepo mkunga
Damu inauzwa, hivyo mama mja-mzito au anunue au waje ndugu zake kumchangia
Uzembe wa baadhi ya wahudumu husababisha vifo vya watoto na waja-wazito
Kwamba matumizi ya vidhibiti mimba yanaweka mpishano mzuri katika kuzaa watoto
Ukweli kuhusu mimba zisizotarajiwa huko Marekani
Hapa tutatumia takwimu kuhusu mimba licha ya matumizi ya vidhibiti mimba
Mnamo 2006 mimba zilikuwepo mimba 52 ambazo hazikutarajiwa/hazikupangwa kwa kila wanawake 1,000 ambao umri wao ulikuwa kati ya miaka 15 na 44
Kufikia miaka 45 zaidi ya nusu ya wanawake wa Marekani wanakuwa tayari wamekumbwa na mimba zisizotarajiwa na mimba 3 kati ya 10 zinatolewa
Mimba zisizotarajiwa hutokea zaidi miongoni mwa wanawake wenye kipato cha chini, wale wenye umri wa kati ya 18 na 24, wale wanaoishi bila ndoa na wanawake waliomo katika kundi la pembezoni.
Kiwango cha mimba zisizotarajiwa miongoni mwa wanawake maskini waiokuwa na umri kati ya 14 na 44 mnamo 2006 kilikuwa 132 katika kila 1,000
Kiwango hiki kikubwa cha mimba zisizotarajiwa kinasababisha mimba nyingi kutolewa, [52 katika 1,000] na kuzaliwa watoto wasiotarajiwa [66 katika 1,000]
Njia za kuzuia
Theluthi mbili ya wanawake wa Marekani ambao wako hatarini kupata mimba zisizotarajiwa ni wale watumiao vidhibiti mimba mara zote na kwa uhakika na asilimia 5 miongoni mwao wanapata mimba zisizotarajiwa. Kwa upande mwingine asilimia 19 wanawake waliomo hatarini kupata mimba zisizotarajiwa ni wale wasiotumia vidhibiti mimba mara zote na kwa uhakika ambao hufanya wanawake wanaopata mimba bila kutarajiwa kuwa asilimia 45. Asilimia 16 ya wanawake waliomo hatarini kwa kutotumia vidhibiti mimba hufanya asilimia 52 ya mimba zote zisizotarajiwa.
Kwamba vidhibiti mimba vinapunguza uwezekano wa kutokeza baadhi ya magonjwa, kama vile saratani ya tumbo la uzazi na saratani ya kokwa
Matumizi ya vidhibiti mimba na uwezekano wa kupata saratani
Chachu za estrogeni na projestini zimeonekana kuathiri na kukua kwa baadhi ya saratani. Kwa jumla tafiti zimeonyesha kuwa matumizi ya vidhibiti mimba [vidonge vya majira] yameonekana kuongeza uwezekano wa kupata magonjwa ya saratani ya matiti, shindo ya kizazi na ini.
Vidonge vya majira husababisha saratani ya matiti
Matokeo ya tafiti nyingi kubwa zilizofanyika duniani yanonyesha vidonge vya majira vinaongeza hatari ya mtumiaji kupata saratani ya matiti. Uwezekano huo unatokana na historia ya matumizi yake na hali yake ya kizazi ambavyo ni pamoja na matiti kuongezewa kiwango kikubwa cha chachu, kwa mfano:
Kuingia balehe na kutumia vidhibiti mimba katika umri mdogo
Kukoma kizazi katika umri mkubwa
Kupata mimba katika umri mkubwa
Kutokuzaa
Utafiti wa mwaka 1996 katika majiribio 50 duniani na “Collaborative Group on Hormonal Factors in Breast Cancer” yaligundua kuwa wanawake wanaotumia vidonge vya majira walikuwa na kiwango cha juu cha kupata saratani ya matiti kuliko wale ambao hawakutumia. Hatari inakuwa kubwa zaidi kwa wanawake wanaoanza kutumia vidhibiti mimba [vidonge] katika umri mdogo.
Saratani ya kokwa
Kwa kadiri ya tafiti zilizofanywa na baadhi ya mashirika ya kitaalamu, tunaelezwa kuwa matumizi ya vidonge vya majira yanapunguza uwezekano wa kupata saratani ya kokwa. Katika tafiti 20 ziliofanyika 1992 iligundulika kuwa kwa kadiri mwanamke anavyotumia vidonge kwa muda mrefu ndivyo hivyo hatari ya kupata saratani ya kokwa hupungua.
Saratani ya tumbo la kizazi
Wanawake wanaotumia vidonge vya majira wameonekana kupunguza hatari ya kupata saratani ya tumbo la kizazi, na hudumu hivyo kadiri mwanamke anavyotumia kwa muda mrefu
Saratani ya shingo ya kizazi
Matumizi ya muda mrefu ya vidonge vya majira huongeza hatari ya kupata saratani ya shingo ya kizazi. Tafiti 24 zilizofanyika zilionyesha kuwa kwa kadiri wanawake wanavyotumia vidonge vya majira kwa muda mrefu ndivyo hivyo wanavyoongeza hatari ya kupata saratani ya shingo ya kizazi.
Taarifa ya tafiti 8 iliyotolewa na shirika la “International Agency for Research on Cancer” ambalo ni kitengo cha Shirika la Afya Duniani [WHO] ilionyesha kuwa wanawake wenye magonjwa ya zinaa, kama vile “human papillomavirus” [HPV] walikuwa katika hatari zaidi ya kupata saratani ya shingo ya kizazi.
Saratani ya ini
Matumizi ya vidonge vya majira yameonekana kuongeza hatari ya wanawake kupata uvimbe katika maini na vinaweza kusababisha maini kuvuja damu au kuchanika.
Kwamba vidhibiti mimba havina madhara kwa watumiaji
Kama kuna uwongo wa kiwango cha juu unaosemwa na kutetewa na wahamasishaji na wasambazaji wa vidhibiti mimba hapa kwetu Tanzania ni ule wa kuwaaminisha watumiaji kuwa eti vidhibiti mimba havina madhara yoyote.Huu uwongo unasemwa hapa kwetu Tanzania tu. Watengenezaji wa vidhibiti mimba na viwanda vitengenezavyo wanatoa tahadhari ya uwezekano wa watumiaji kupata madhara, mengine madogo na mengine makubwa yanayohitaji huduma ya mtaalamu wa afya. Lakini kwetu sisi watetezi uhai, hatushangai hatua hiyo ya watetezi wa kifo, wao wanafurahi wanapoona wanawake wanapata mateso, wao wanafanya biashara ili watajirike, wao wanachuchumia magari makubwa na kifahari ili waonekane kuwa ni watu muhimu katika jamii, wao wanafurahia utasa kwani lengo lao ni kupingana na amri ya Mungu ‘zaeni mkaongezeke mkaijaze nchi’.
Baadhi ya madhara tumekwishataja hapo awali, yaani matumizi ya vidhibiti mimba [vidonge vya majira] vinahusishwa na kuongezeka viwango vya saratani ya matiti, shingo ya kizazi na maini. Ingawa watetezi wa vidhibiti mimba wanadai eti matumizi ya vidonge vya majira vinahusika na kupunguza uwezekano wa kupata saratani ya tumbo la uzazi na kokwa. Lakini baadhi ya wataalamu kama vile, Dr. Ellen Grant, akiandika katika kitabu chake “Sexual Chemistry” (1995) anasema kuwa upo ushahidi wa kutokea kwa saratani ya kokwa na tumbo la uzazi kwa wanawake wanaotumia vidonge vya majira.
Wanawake wanaotumia vidhibiti mimba wanakabiliwa na moja au zaidi ya madhara [magonjwa] yafuatayo
(a)Madhara ya kiwango kidogo
1.Kichefuchefu
2.Kutapika
3.Kuumwa kichwa
4.Kizunguzungu
5.Kuongezeka uzito na maumivu katika matiti
6.Kutokwa damu kidogo
(b)Madhara makubwa yanayoweza kusababisha kifo, magonjwa ya kudumu au udhaifu wa afya na hivyo kuhitaji tahadhari kubwa:-
1.Maumivu makali ya tumbo
2.Maumivu makali ya kifua au kutopumua vizuri
3.Maumivu makali ya kichwa au kizunguzungu
4.Matatizo ya macho, kama kutoona vizuri, mianga mikali ya ghafla au upofu, yaani kutoona kabisa
5.Maumivu makali ya miguu au uvimbe.
Madhara mengine ni:
1.Kuganda kwa damu,
-ikiganda katika moyo itasababisha mshituko wa moyo,
-ikiganda katika mapafu husababisha mapafu kushindwa kufanya kazi,
-ikiganda katika figo itasababisha figo kushindwa kufanya kazi,
-katika mshipa wa macho itasababisha kushindwa kuona (kuwa kipofu).
2.Mkandamizo wa damu (BP)
3.Saratani ya matiti (breast cancer), hasa miongoni mwa wasichana wanaotumia dawa hizi kabla ya kuzaa, kansa yaweza kuwa
-kulainika kwa matiti,
-matiti kuwa makubwa,
-uvimbe na
-kutoka maziwa mfululizo.
4.Saratani ya mlango wa tumbo la uzazi (cervical cancer), ambayo hutegemea
-Idadi ya vidonge vilivyomezwa,
-kiasi cha wapenzi aliokutana nao mtumiaji,
-umri ambao mwanamke alianza kutumia,
-kama anavuta sigara au la,
-hali ya usafi wa wapenzi akutanao kingono na
-maambukizo ya magonjwa ya zinaa
5.Saratani ya tumbo la uzazi na saratani ya kokwa (endometrial and ovarian cancer) yaelekea kuwa ya kiwango kidogo na hutokea miongoni mwa wanawake waliotumia mchanganyiko wa vidonge vyenye chachu ya estrojeni na projestini). Kiwango cha saratani hii ni kidogo na hutokea hasa kwa wanawake waliopita umri wa kuzaa na wako kwenye miaka ya 50 na 60.
6.Saratani ya ini hutokea kwa wanawake vijana wenye umri kati ya 15 na 40.
7.Saratani ya ngozi (melanoma) hutokea kwa kuharibika ngozi ya juu inayokinga mwili. Matumizi makubwa ya vidonge huharibu kwa kiwango kikubwa ngozi hii na kumfanya mtumiaji akose kinga ya mwili.
8.Wanawake wengine wanaweza kutoka damu bila mpangilio au mabonge mabonge ya damu au wasipate kabisa hedhi, au kupata maumivu makali wakati wa hedhi (dysmenorrhea).
9.Magonjwa ya akili hata kufikia hatua ya kujiua au maelekeo ya kutaka kujiua
10.Kupungua au kupoteza hamu ya kujamiana
11.Magonjwa ya ukeni
12.Utasa wa muda au wa kudumu
NB: Kwa kifupi tunaweza kusema kuwa matumizi ya vidhibiti mimba hugeuza afya bora ya wanawake na kuwafanya wawe wagonjwa. Kwa kila mwanamke mtumiaji vidhibiti mimba ni mgonjwa, hata kama ugonjwa wake ukawa mdogo kiasi gani, ukweli utabaki kuwa yule mwanamke aliyekuwa na afya njema, sasa afya yake imetetereka.
Kwamba matumizi ya vidhibiti mimba yanawezesha kupungua idadi ya watu
Hoja kwamba matumizi ya vidhibiti mimba yanawezesha kupungua idadi ya watu ni ya kweli, na pengine ndilo lengo la kampeni inayoendelea hivi sasa.