1.1
Mswada una sehemu 9. Sehemu inayohusu “Uzazi Salama” [Safe Motherhood] imetokea mara moja tu, Sehemu ya 3 tu. Sehemu kubwa ya mswada huu inahusu masuala yanayohusiana na Upatikanaji wa Vidhibiti Mimba na Uzazi wa Mpango kwa watoto [2]; Afya ya Ujinsia na Afya ya Kizazi kwa watoto [4]; Kutoa Mimba [5]; UKIMWI na Magonjwa ya Zinaa [6]; Vitendo Viovu na Afya ya Ujinsia na Afya Kizazi kwa watoto [7]; Utekelezaji wa Sheria [8]; Maelezo ya Awali [1] na Mengineyo [9]. Kwa hiyo msukumo wa Mswada huu hauhusu kuwasaidia wanawake waja-wazito kupata huduma zinazostahili, bali kusukuma masuala ya kudhibiti kizazi, matumizi ya vidbibiti mimba, kutoa mimba na sheria kali na za kimabavu zitakazotumika ili kuhakikisha kwamba idadi ya Watanzania inapungua. Uzito umewekwa vile vile katika kuharibu afya za wasichana kwa njia ya vidhibiti mimba ili wapoteze uwezo wao wa kizazi kwa kadiri wanavyoendelea kutumia. Tena mswada unalenga kuwaondolea wazazi mamlaka katika malezi na makuzi ya watoto wao. Jambo kubwa zaidi na ni siri kubwa iliyofichika katika mswada huu ni nia ya mashirika ya kimataifa ya Ulaya na Marekani ya kuhalalisha utoaji mimba. Ndani yake imo fikra kwamba utoaji mimba iwe ni sehemu ya haki za wanawake na eti vitendo hivyo vitadumisha afya ya kizazi ya wanawake. Mpango wa Umoja wa Mataifa, ni kuhakikisha kwamba malengo ya milenia yanatimia, na moja ya malengo hayo ni kuhakikisha kwamba kila nchi duniani inapitisha sheria za kutoa mimba ifikapo 2015.
1.2
Mswada huu umekwepa kutumia maneno na dhana ambazo ndizo zingekuwa msingi katika kutekeleza kanuni za uzazi salama. Hatuoni maneno kama vile, mama, umama, baba, mume, mke, ndoa, familia. Katika sheria inayohusu uzazi salama, tulitegemea ungekuwepo mwingiliano mkubwa katika maisha ya mume na mke katika ndoa. Tulidhani kuwa katika uzazi salama, hatuzingatii tu afya ya mama na mtoto ambaye atazaliwa au aliyekwishazaliwa, bali tunaangalia pia nafasi ya mume na watoto waliotangulia kuzaliwa kwani kila mmoja katika familia anachangia ustawi wa mwingine. Mswada ulikwepa nini kutumia maneno baba na mama katika kutoa idhini kama mtoto atumie au asitumie vidhibiti mimba? Badala yake mswada unatumia tu maneno “wazazi” bila kusema bayana kwamba wazazi hao wako katika ndoa. Haidhuru kama watoto wamepatikana nje ya ndoa au kabla ya ndoa, basi nafasi ya baba na mama wa watoto hao inabaki palepale, kwani hatimaye, lawama kwa maisha duni au mabaya ya watoto ukubwani wanabebeshwa wao. Inaonekana mswada huu umesukumwa na wanawake wenye itikadi kali za umame, ambao kwao, ndoa, mume, watoto na familia ni machukizo. Hawataki kusikia maneno hayo kwa sababu, katika fikra zao wanataka kufutilia mbali dhana ya ndoa, mume na familia. Kwao hawa dhana za umama na ubaba na ndoa ni sumu kwani zinafikiriwa ndio msingi wa ukandamizaji wa wanawake. Ndiyo maana suala la malezi ya watoto badala ya kuliacha mikononi mwa wazazi, yaani baba na mama, wao wamewaondolea madaraka wazazi hao, kwa kuwajengea kiburi watoto kwa kusema “eti watoto wanaweza kutumia vidhibiti mimba bila ridhaa ya wazazi”.
1.3 Mswada huu unaibebesha mzigo serikali. Serikali inaagizwa isimamie vitendo vyote viovu vilivyomo katika mswada huu, kama vile, kuhamasisha na kuhakikisha upatikanaji wa vidhibiti mimba na uzazi wa mpango kwa watoto. Serikali inaagizwa kutengeneza miundo ya kusimamia utekelezaji wa huduma za uasherati kwa vijana, ambazo mswada unasema zipatikane kwa bei inayowezekana, na kwamba huduma hizo ziwe rafiki kwa vijana. Mswada unataka serikali kulipia gharama za vifaa vya kutolea mimba pamoja na huduma za ushauri nasaha kwa wanawake watakaokuwa wameumizwa na utoaji mimba. Serikali inaagizwa kulipia watendaji wa Mahakama itakayoundwa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba programu za kudhibiti idadi ya watu nchini mwetu zinafanikiwa bila vipingamizi vyovyote vile. Ndani ya mantiki hii ipo dhana kwamba mashirika au taasisi itakayopingana na dhamira hii ya kudhibiti kizazi basi wapelekwe katika mahakama hiyo ili waadabishwe.
1.4
Mswada wenyewe unajipinga. Wakati mswada unahusu uzazi salama, tulitegemea mswada uzungumzie masuala yanayohusu wanawake wenye stahili ya kuzaa, yaani wale waliomo katika ndoa, na hata kama hawajabahatika kuwa na ndoa, basi wanawake hao wawe wale waliofikia umri wa utu uzima. Hatuelewi kwa nini mswada unawazungumzia pia watoto walio chini ya umri wa utu uzima, yaani miaka 18 na kuendelea. Mswada unawataka watoto hao watumie vidhibiti mimba, kupanga uzazi. Je katika umri huu wa ujana, watoto watumie vidhibiti mimba kwa lengo gani? Kama nia ni kudhibiti mimba za utotoni, kwa nini tusiwafundishe fadhila za kujiheshimu, kujishinda na za usafi wa moyo? Hawa watoto wanapanga uzazi, je wameolewa? Mbona mswada huu unatamka kuwa kama mtoto ataolewa chini ya umri wa miaka 18, huyo atakayemwoza na huyo atakayefungisha ndoa watakuwa wametenda kosa linalostahili kulipa faini au kufungwa? Vilevile kama mswada unahusu uzazi salama, sasa suala la kutoa mimba limeingizwaje? Kwani mwanamke anayetolewa mimba anaupata wapi uzazi salama? Je huyo mtoto anayeuawa katika tendo la kutoa mimba anakuwa salama? Kama mswada huu unahusu uzazi salama, kwa nini basi umeandikwa katika lugha kali, yenye vitisho, adhabu na kuwekewa vyombo vya utekelezaji ikiwa ni pamoja na mahakama? Kwa nini serikali ibebeshwe mzigo wa kuhamasisha na kugharamia upatikanaji wa nyenzo za kudhibiti kizazi? Kama mswada unahusu uzazi salama, dhana za kudhibiti kizazi zimejitokezaje? Tulitegemea badala ya kudhibiti kizazi mswada ungehamasisha uzazi salama, ukihimiza wanawake kupata huduma nzuri wakati wa kuzaa, na sio kuua watoto wao au kuharibu kizazi chao kwa vidhibiti mimba. Ikiwa mswada unahusu uzazi salama, mbona hatuoni nafasi ya baba katika mswada huu, badala yake mswada unasema, wanaume nao watumie vidhibiti mimba?
2. Sehemu ya kwanza
Mswada unatoa tafsiri ya dhana mbalimbali kulingana na mahitaji ya aliyeuandika. Kwa bahati mbaya sana, baadhi ya tafsiri za dhana zinaficha ukweli wa jambo, au kwa makusudi zinakengeusha maana halisi. Kwa mfano, “uzazi wa mpango”- tafsiri iliyotolewa ni jitihada za makusudi za majozi au watu binafsi au wanawake kupanga kwa uhuru na kupata idadi ya watoto wanaowataka, na kuweka mpishano na muda wa kuzaa kwa kutumia au kwa kutotumia vidhibiti mimba. Mtego uliopo hapa, umo katika neno wanawake. Haielezi wanawake hao wanaoweza kutumia vidhibiti mimba wana umri gani kwa maana hata msichana wqa miaka 15 ni mwanamke. Hapa ni wazi tafsiri imewekwa pana kiasi hicho ili kuwahusisha hata wasichana ambao bado shuleni.Badala ya kutumia maneno “kutoa mimba”, mswada umekwepa maneno hayo na kutumia maneno “kukatisha mimba”, na tafsiri yake ni kutenganisha na kuondoa, kwa njia za kikemikali au upasuaji, vitu vilivyomo ndani ya tumbo la mwanamke mja-mzito. Tafsiri hii imekwepa kabisa kutamka neno mtoto [ambaye bado hajazaliwa] na kwa kweli binadamu huyu mdogo amedunishwa sana. Na hii imefanyika kwa makusudi ili kuwezesha tendo la kumuua ili kufutilia mbali dhamiri inayopingana na vitendo hivyo viovu. Je kinachotenganishwa ni nini? Hivyo vipande vipande ni vitu gani? Kinachotolewa nje ni nini? Je kama mtoto ndani ya tumbo la mwanamke mja-mzito amekatwakatwa na kutenganishwa, huyo mwanamke bado ni mja-mzito. Tafsifri nzuri ya kutoa mimba, kwa kila mtu ambaye hajabutushwa utashi na akili yake ni – kumwua mtoto ndani ya tumbo la mama kwa kumkatakata na kutoa nje vipande vipande; au pia ni kumwua mtoto kwa njia za kikemikali na kumtoa nje akiwa mfu.
2.1
Tafsiri nyingine ya ulaghai ni ile inayoitwa “ukubalifu wa hiari”, au “ridhaa huru”. Mswada unatafsiri dhana hiyo kuwa ni ukubalifu au ridhaa inayotolewa bure bila kitisho au kudanganywa baada ya kupata taarifa sahihi na inayoeleweka katika muundo na lugha inayoeleweka kwa mgonjwa. Hapa kuna mtego mkubwa. Jee maelezo ya taarifa yatatofautiana kutoka mgonjwa hadi mgonjwa, kwa vile uelewa wa watu unatofautiana? Maelezo atakayopatiwa mgonjwa A yatakuwa tofauti na maelezo atakayopatiwa mgonjwa B kuhusu, kwa mfano, sindano ya depo provera. Kwa vile mgojwa A amesoma hadi kidato cha nne na mgojwa B ameishia elimu ya shule msingi au hajasoma kabisa, basi uelewa wao utakuwa tofauti. Huu ni udanganyifu mkubwa kwa watu. Na kwa kweli dhana ya ukubalifu au ridhaa imeletwa kama kisingizio tu, kamwe hapatakuwa na jambo hilo. Na wanawake watakaonunua, au watoto wa shule watakaonunua vidonge vya majira katika maduka ya madawa nani atawapatia taarifa sahihi ya utendaji wake, madhara yake ili wanunue kwa ridhaa yao? Au wahudumu wa afya, wanaotajwa katika mswada huu wataajiriwa hata katika maduka ya madawa au katika zahanati za vichochoroni? Wanawake waelewe kuwa kifungu hiki kimewekwa kama mtego kwao – watakapotumia vidhibiti mimba – washindwe kulalamika kwa vile “walitakiwa watumie baada ya kushauriwa, nao wakubali kwa ridhaa yao”. Kwa hiyo, kama vidhibiti mimba vitawasababishia kupata saratani ya matiti au upofu wa macho, au kunenepa, au magonjwa ya moyo, itakuwa shauri yao.
2.2
Mtego mwingine umo katika tafsiri ya maneno “haki ya afya ya kizazi” [reproductive health rights]; humaanisha haki ya kila mtu kupata afya ya ujinsia na afya ya kizazi kwa kiwango cha juu kabisa na kufanya uamuzi ulio huru kuhusu maisha yao ya kizazi, idadi na mpishano wa kuzaa watoto bila ubaguzi, kulazimishwa na matumizi ya nguvu. Tafsiri hii inawatega wazazi ambao wanatakiwa wasiingilie maamuzi ya watoto wao masuala yanayowahusu – yaani matumizi ya vidhibiti mimba na kutoa mimba. Vile vile inatega wanandoa kwa vile tunahubiriwa kwamba mke ndani ya ndoa anatawaliwa na mume wake kiasi kwamba hana maamuzi yake binafsi. Katika tafsiri hii, mke ndani ya ndoa anawekwa huru kutumia vidhibiti mimba kadiri aamuavyo, asiingiliwe na mume wake; anaweza hata kutoa mimba bila ridhaa ya mume wake. Suala la kuamua idadi ya watoto linaweza kufanywa na mke peke yake, bila kuingiliwa na mume. Nadhani pia, hata haki ya tendo la ndoa, mume asimlazimishe mke wake. Kwa maneno mengine, mke awe huru kukubali au kukataa masuala ya unyumba. Watoto wasikatazwe, yaani wasibaguliwe, katika haki yao ya kufanya maamuzi wayapendayo.
3. Sehemu ya pili
3.1
Mkazo katika sehemu hii unahusu kudhibiti kizazi na hivyo kudhibiti ukuaji wa idadi ya watu. Njia zinazotajwa katika mswada huu ni zile zinazowahakikishia wanawake utasa kwa kuharibu kizazi chao, zinazowaletea mateso na hatimaye zinazowafanya waukane umama kwa kuuona kama ugonjwa na kuwaona watoto kama balaa linalopaswa kuepukwa. Ingawaje mswada unasema juu ya kupanga uzazi, hakuna taifa duniani lililojizatiti kutumia vidhibiti mimba likawa bado na idadi kubwa ya vizazi. Taifa lolote lililokumbatia matumizi ya vidhibiti mimba limeshuhudia kukataa uzao wa watoto, na kama watazaliwa basi hawazidi mmoja au wawili tu. Taifa lolote lililoamini katika kutumia vidhibiti mimba limeshuhudia kukauka vizazi kiasi kwamba wanandoa na wasio na ndoa wanalazimika au kutafuta watoto kutoka nchi zile zinazozaa watoto wengi, au wanalazimika kutumia njia mbadala wa kupata watoto, ndio ikazuka sayansi ya watoto wa chupa. Lakini pia, mataifa hayo yameshuhudia kushamiri kwa saratani ya matiti miongoni mwa wanawake wao. Saratani ya matiti, kwa kiasi kikubwa husababishwa na matumizi ya vidhibiti mimba na vitendo vya utoaji mimba.
3.2
Ili kufikia azma hiyo mswada unasema fimbo ya kumaliza vizazi vya Watanzania ishikwe na serikali yao kwa kuhakikisha kwamba vidhibiti mimba pamoja na mazao yake vinapatikana kwa kila mmoja, bila kujali kama ameolewa au la. Na kuondoa uwezekano wa bughudha, hasa kwa watoto, mswada unasema, katika kutoa huduma za uzazi wa mpango lazima kuhakikisha haki ya mtu binafsi na usiri. Mashirika au taasisi ambazo zitatakiwa kufyata mkia, kwani mswada unasema lazima serikali iondoe vipingamizi vya matumizi ya vidhibiti mimba ikiwemo pamoja na vizuizi vya kisheria na vizuizi katika kusambaza habari kuhusu vidhibiti mimba. Hapa ndipo unapolala utashi wa wale walioandika mswada huu, kwamba lengo lao sio “kupanga uzazi”, bali kukausha vizazi. Kama lengo lao lingekuwa jema, wasingediriki kusema kwamba serikali iwazuie wale wanaosema ukweli kuhusu madhara yatokanayo na matumizi ya vidhibiti mimba. Mbona hawasemi kwamba waondoe vizuizi vinavyowekwa katika kuhimiza matumizi ya njia za asili/maumibile katika kupanga uzazi? Hawa wanajua, maadui wao wakubwa ni mashirika ya kutetea uhai na familia na Kanisa Katoliki. Ni Kanisa Katoliki ndilo linazuia usambazaji wa vidhibiti mimba katika mahospitali na vituo vya afya vilivyo chini yake. Ni mapadre ndio wanaofundisha kwamba ni dhambi kutumia vidhibiti mimba. Ni mashirika ya kutetea uhai na familia ndiyo yenye kueleza ukweli kuhusu madhara ya kutumia vidhibiti mimba. Na ni mashirika hayo ndiyo yanafundisha na kuhamasisha kuweka mpishano wa uzao kwa kutumia mwenendo wa uzazi katika mwili wa mwanamke. Watetezi wa vidhibiti mimba, ambao ndio pia waandishi wa mswada huu, wanaelewa kuwa ukweli unaosemwa na Kanisa Katoliki na mashirika ya kutetea uhai na familia ni kikwazo kikubwa kwao. Ndugu hawa wanathamini zaidi fedha kuliko afya za wanawake wanaoumia kwa kutumia vidhibiti mimba. Hebu tuwaulize, ni mara ngapi wamejitokeza kuwasaidia wanawake waliodhurika kwa kutumia vidhibiti mimba? Hebu tuwaulize nyinyi wanawake mnaokubaliana na matumizi ya vidhibiti mimba, mara ngapi mmesaidiwa na yule aliyewapatia vidhibiti mimba, wakati mlipoumizwa na vidhibiti mimba hivyo?
3.3
Mswada unaposema eti, wahudumu wa afya watalazimika kutoa maelezo kabla ya kutoa vidhiviti mimba, ni uwongo mtupu. Waulizeni wanawake wanaohudhuria kliniki watawaambieni kinachotoka midomoni mwa wahudmu wa afya. Na kama nilivyosema hapo awali, kifungu hiki kimewekwa kama kinga kwa mtoa huduma hiyo. Waandishi wa mswada huu wanaelewa kwamba kama sheria itatungwa, itakuwa ni lazima kwa wanawake wote kutumia vidhibiti mimba, na wanajua pia kuwa wanawake hao watadhurika. Kwa hiyo ili kujikinga na malalamiko, na hata uwezekano wa kushitakiwa kwa kuwaletea wanawake maumivu na majeraha, wanajihami kuwa watoa huduma za afya watoe maelezo na mwanamke achukue na kutumia baada ya uelewa. Je, wahudumu wa afya watakuwa tayari kusema kwa ukweli na kwa dhamiri safi kuhusu madhara ya kutumia vidhibiti mimba? Kama wanawake watapata ukweli wote na wakagoma kutumia, nani ataadhibiwa? Je patawekwa mfumo gani wa utekelezaji kuhakikisha kwamba kila mhudumu wa afya atatekeleza wajibu wake wa kumweleza mwanamke ukweli wote kuhusu vidhibiti mimba? Je, ni kweli kwamba mhudumu wa afya ataeleza hasara ya vidhibiti mimba? Kabla ya mswada huu wahudumu wa afya walizuiwa kueleza madhara ya vidhibiti mimba, na wale walioeleza madhara, baadhi yao walipoteza kazi zao. Kuna baadhi ya mashirika ya hiari yaliweka kanuni ya kutoajiri Wakristo Wakatoliki kwa kuhofia kuwa “siri” itafichuka. Wanaume katika sehemu hii wametajwa tu, kwa kweli hawakudhamiriwa. Kwa muda mrefu wanaume wamelaumiwa kwamba ndio wanaoweka vipingamizi katika matumizi ya vidhibiti mimba.
4. Sehemu ya tatu
Sina matatizo na sehemu hii, isipokuwa nina wasiwasi na malengo fichika yaliyomo katika sehemu ya 12 (a) inayoitaka serikali kuhakikisha kuwa kila kijiji kinakuwa na zahanati na kila kata inakuwa na kituo cha afya na kila wilaya inakuwa na hospitali. Kama waandishi wa mswada huu wana nia njema na matatizo ya kiafya yanayowasibu akina mama wetu, naunga mkono wazo hilo. Lakini kama zahanati hizo, vituo vya afya na hospitali katika ngazi husika vitatumika kama vituo vya kugawa vidhibiti mimba na kutolea mimba, basi mswada huo hautakuwa na nia njema kwa watu wa Tanzania.Sina hakika na nia iliyomo katika kuiagiza Wizara kugharamia mfuko maalumu unaohusu ushiriki wa wanaume katika maeneo yote yanayouhusu huduma za kiafya za kizazi.
5. Sehemu ya nne
Sehemu hii ndiyo inayoniletea kichefuchefu, kwa vile inakiuka wajibu wa malezi ya watoto katika maadili mema na badala yake mswada unaiagiza serikali kwa kushirikiana na wadau wengine kuhakikisha kuwa watoto wanapatiwa huduma rafiki za afya ya ujinsia na afya ya kizazi. Sielewi maana ya huduma ‘rafiki’ zinazohusu habari na elimu kuhusu afya ya ujinsia na afya ya kizazi. Je watoto watapewa habari na watafundishwa matumizi ya vidhibiti mimba? Je kwa nini mswada unawaondoa wazazi katika wajibu wa malezi ya watoto wao? Kipindi cha ujana katika makuzi ni kipindi mwafaka kwa wazazi kuwaelekeza watoto wao katika tunu za stadi za kazi, kuwajengea misingi bora ya maadili, kuwaelekeza kumjua Mungu na mahusiano mazuri kati ya vijana na kati ya vijana na wazazi wao. Mswada unazungumzia kuondoa vizuizi vyote kuhusu upatikanaji wa huduma za afya ya ujinsia na afya ya kizazi kwa watoto? Je, mswada unataka kutuambia, sisi wazazi, walezi na viongozi wa kidini tusiwaeleze watoto wetu hasara zinazopatikana kwa kujiingiza katika masuala ya ngono katika umri mdogo? Je, mswada unataka kutuambia tusiwaeleze watoto wetu madhara yatokanayo na matumizi ya vidhibiti mimba na utoaji mimba? Mswada wa aina hii una lake jambo, ambalo waasisi wake hawataki kulisema bayana. Jambo lenyewe ni hili: mswada unataka kuharibu kizazi cha vizazi vijavyo; unataka kuharibu maadili yaliyofaulu kuwajengea watu utu wema tangu kale; unataka kuwadhohofisha watoto wetu kiafya na kiakili ili tuendelee kuwa taifa tegemezi na ombaomba; unataka kuvunja misingi ya kidini na taifa lisilomjua Mungu na hatima yake ni kustawisha vitendo vya ushoga na ndoa za watu wa jinsi moja. Mataifa yote yaliyokumbatia sera za vidhibiti mimba na utoaji mimba ya nchi za Magharibi yameharibikiwa kimaadili, idadi ya watu wao kupungua, kupuuzia taasisi ya ndoa na familia na hatimaye kuendeleza vitendo vinavyokwenda kinyume na ubinadamu wetu.
Nashangaa kuona kuwa mswada unataka kuwaburuza wahudumu wa afya hata wasizingatie kanuni za dhamiri zao eti watahesabika wamevunja sheria kama watakiuka kipengele cha 14 (2). Jee, mswada unataka kuwaburuza wahudumu wa afya kiasi hicho? Jee, wahudumu wa afya wavunje kanuni na wajibu wa msingi wa wazazi katika malezi ya watoto wao? Je mswada unataka kuwaadhibu wahudumu wa afya kama watawaeleza watoto madhara ya vidhibiti mimba na utoaji mimba? Hii itakuwa ni sheria ya ajabu na ya kikatili sana duniani; maana sheria inayomnyima mhudumu wa afya uhuru wa kutenda kulingana na dhamiri yake ni sheria ya kibabe. Nadhani pia sheria hii inakusudia kuondoa uhuru na haki ya watu katika kueleza hasara za kiafya na kisaikolojia wanazopata watu wote wanaotumia vidhibiti mimba na utoaji mimba.
Jambo baya zaidi ni pale mswada unapoibebesha serikali majukumu mazito, baada ya kwamba umewaondolea wazazi na wajibu na haki katika malezi ya watoto wao; ya kugharamia huduma za afya ya ujinsia na afya ya kizazi kulingana na umri wa watoto. Kwa maneno mengine, badala ya wazazi kuwafundisha watoto wao katika masuala ya ujinsia na afya ya kizazi, sasa serikali inaagizwa ilipie huduma hizo ambazo zitafanywa na walimu waliofundishwa kwa lengo hilo. Kwa maneno mengine, mswada unavunja mila na desturi za watu wa makabila mbalimbali ambayo yalikuwa yanatoa elimu hiyo kulingana na umri, jinsi na mahali. Mswada huu ukiwa sheria, basi, mshikamano wa kikabila utapotea, maana hapatakuwa tena na mila za Kingoni, Kindengereko, Kisukuma, Kihaya, Kinyamwezi, Kinyakyusa na kadhalika. Na taifa lisilokuwa na mizizi katika mila na desturi zake, ni taifa mfu, lenye kuzaa watu wa hovyo. Ndiyo maana, tusishagae huko mbeleni kuona watu wanauana hovyo, wanachinjana hovyo, wakubwa wanafanya mapenzi na watoto wadogo, watu wa jinsi moja wanakaa kinyumba.
6. Sehemu ya tano
Mswada unapingana na Katiba ya Jamhuri ya Mwungano, ibara ya Ibara ya 14 juu ya haki ya kuishi na kupata kutoka jamii hifadhi ya maisha yake na Sheria ya Kanuni ya Adhabu [the Penal Code] vifungu vya 150, 151, 152 zinazomtia hatiani mtu anayefanya jaribio, kusaidia na kutumia vifaa kwa ajili ya kutoa mimba na kifungu cha 219 kinachozuia utoaji mimba isipokuwa katika mazingira maalumu. Sehemu hii ya mswada inaonyesha ukatili uliopea katika mawazo ya wale walioandika. Mswada unatoa ruhusa kwa mwenye mimba kumwendea mhudumu mmoja tu wa afya na kumwomba kumwua mtoto anayekua tumboni mwake; ili mradi mhudumu huyo awe yule aliyesomea kazi hiyo na anavyo vyeti vya kumruhusu kufanya hivyo. Maskini mhudumu huyu wa afya, badala ya kwenda kusomea taaluma ya kutibu watu magonjwa yao ili kuwarudishia afya yake, mhudumu huyu atakwenda kusomea utaalamu wa kuua watoto kabla hawajazaliwa. Kiapo kile waapacho wenzake wanapohitimu juu ya kuhudumia afya na kutomdhuru au kumwua mgonjwa, mhudumu huyu atakuwa ameapa kiapo kingine, bila shaka kipya, kile cha kuua watu kikemikali au kwa kuwachija wakiwa matumboni na kuwatoa nje wakiwa wafu. Bila shaka wahudumu hawa watakuwa wamejifunza pia, namna ya kuwazika watoto wanaowaua.
Hebu fikirieni, mswada unasema mwanamke anaweza kumwambia mhudumu wa afya amuue mtoto wake kabla hajazaliwa kama mtoto huyu analeta hatari au majeraha kwa afya ya mama huyo kimwili na kiakili.Hebu niambieni ninyi wanawake mliopata kuzaa, ni nani miongoni mwenu hapati mabadiliko ya kimwili au kiakili anapopata uja uzito? Je hayo ni mabadiliko ya kudumu? Hakuna mama mja-mzito asiyepata mabadiliko. Tena wanawake wengine wanaumwa sana wakiwa waja-wazito. Na wengine wanaweza kufanya vitendo visivyo vya kawaida kwa waume zao au watu wengine. Kweli wewe mama umwue mtoto wako kwa vile umekonda, au umenenepa, au tabia yako imebadilika?
Ole wetu sisi wenye ulemavu wa aina yoyote ile. Kama mswada huu ungeandikwa kabla hatujazaliwa, basi leo tusingekuwapo hapa duniani, maana wote tungewindwa kama mnyama kwa ajili ya kitoweo na kuuawa. Mswada unasema kama mimba inaonekana kuwa itakuwa na ulemavu wa kimwili au kiakili basi mimba hiyo iuawe. Sijui nani mlemavu mkubwa zaidi kiakili; yule mtoto ambaye bado hajazaliwa au yule ambaye ameandika mswada huu? Kwa maana haiingii akilini kukaa chini na kuandika kuwa watoto wote wanaogundulika kuwa ni walemavu wauawe. Wenzetu waliopitisha sheria za kutoa mimba miaka mingi huko nyuma, sasa wameingia hatua nyingine, inayoitwa “selective abortion”, maana yake, patakuwa na vipimo katika zahanati, vituo vya afya, na hospitali ili kuangalia watoto waliomo matumboni. Wale watakaogundulika kuwa na ulemavu wowote ule, basi watauawa. Kwa bahati mbaya, sisi tunaburuzwa katika hatua hii ya pili; hata kabla hatujaona madhara ya hatua ya kwanza; yaani ile ya kutoa mimba. Sisi tunaunganishiwa, sheria ya kutoa mimba na kuua mimba walemavu. Kwa hiyo, walioandika mswada wanatarajia kuwa baada ya kizazi hiki kupita, patatokea kizazi kisichokuwa na walemavu; isipokuwa walemavu wanaowatungia wengine sheria za kuwaua watoto wao kabla ya kuzaliwa. Nadhani kuna haja ya kutunga sheria ya kuwaua walemavu wa aina hii.
Vilevile mswada unatoa hukumu ya kuuawa watoto waliotokana na ubakaji na wale waliotokana na ndugu wa damu moja. Mswada huu ulivyokuwa wa ajabu, unamwacha mbakaji huru, ili aendelee kubaka wengine na kumwua mtoto ambaye, kwanza hakuamua mwenyewe kuwepo; pili, hana hatia; na tatu hawezi kujitetea. Huu ni udhalimu mkubwa. Mswada unafumbia macho ukweli kwamba, kitendo cha ubakaji ni kitendo cha udhalilishwaji na cha kikatili. Lakini anafumbia macho ukweli mkubwa zaidi kwamba kitendo cha kutoa mimba nicha udhalilishwaji wa mwanamke na cha kikatili kwa mwanamke mwenyewe na mtoto aliyemo tumboni mwake. Kwa hiyo, mswada unapendekeza tutibu jeraha kwa kumweka jeraha zaidi huyo mwanamke na mtoto wake. Isitoshe ipo sheria inayoshughulikia makosa ya aina hiyo; kwa nini mswada usihimize matumizi yasheria hiyo? Vile vile kuhusu mtoto aliyepatikana kutokana na ndugu wa damu. Kama nilivyosema hapo juu, mswada unamwacha mkosaji na kumwadhibu mtu asiyekuwa na makosa. Katika mazingira kama hayo, mswada ungependekeza, wale ndugu wanaosababisha uja-uzito wa aina hiyo, waadhibiwe kwa kuwataja hadharani ili vitendo hivyo vikomeshwe. Ni kweli, msichana aliyefanyiwa vitendo hivyo na hata yule aliyehusika na uja-uzito huo watapata aibu katika jamii, lakini ni mbaya zaidi kwa msichana kwani atapitia mateso makubwa – ya kupata uja-uzito wa ndugu na kumwuua mtoto wake na yeye mwenyewe kudhurika kimwili na kisaikolojia.
Kwamba mja-mzito mwenyewe kutokana na hali yake ya ulemavu wa kiakili atashindwa kuihudumia mimba hiyo; ni sababu isiyokuwa na msingi. Tumepata kushuhudia watoto wakizaliwa na akina mama wenye hali hizo, wakalelewa au na wao wenyewe ama katika vituo vya kulelea watoto na wakakua vizuri tu. Kama wanawake wengine wenye shida za uzazi wanatafuta watoto, kwa nini mswada usipendekeze kuwa watoto wanaozaliwa na akina mama walemavu wa akili wachukuliwe na wale wenye shida ya uzazi?
Lazima tufahamu kuwa hakuna sababu yoyote ya msingi ya mama kwa kushirikiana na mhudumu wa afya kumwua mtoto wake. Na jamii ielewe kuwa katika kila tendo la utoaji mimba, mmoja anauawa, mmoja anaumizwa na mmoja analipwa. Kwa hiyo, utoaji mimba ni biashara kubwa duniani. Watu wanatajirika, wanasomesha watoto wao kutokana na biashara hii haramu. Vilevile, jamii ikumbuke kuwa utoaji mimba ni vitendo vya vya kimabavu - vinavyotumia nguvu kubwa dhidi ya mama na mtoto; ni vitendo vinavyomwaga damu nyingi ya binadamu – mama na mtoto; vitendo vya kikatili, vinavyovuka mipaka ya fikra ya binadamu, yaani ni vitendo vya kinyama. Hakuna anayeweza kufikiri kuwa binadamu atamwinukia binadamu mwingine na kumwua.
Hatimaye tukukumbuke kuwa utoaji mimba ni vita visivyo vya haki dhidi ya binadamu asiye na hatia, asiyeweza kujitetea na ni mdogo kabisa.
Mbaya zaidi, kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu tutashuhudia uwepo wa vituo vya kutolea mimba hadharani. Huko nyuma utoaji mimba ulikuwa wa siri sana, na haikuwa rahisi kuvitambua vituo vya kutolea mimba. Mswada unamwaagiza Waziri kuteua vituo vya kutolea mimba. Kwa mara ya kwanza Waziri katika Serikali ya Tanzania anabebeshwa jukumu la kuteua vituo vya kuchinjia watoto wetu, na hivyo kuhakikisha kwamba kizazi cha baadaye kinapotea kabisa. Kwa nini mswada unambebesha dhambi Waziri wetu ambaye tunamwamini na kupewa dhamana ya uhai wetu? Inakuwaje Waziri ambaye yuko madarakani kwa uteuzi wa Raisi apokee majukumu ya kikazi kutoka chombo kingine ambacho hakina uhalali kisheria? Je, na sisi wananachi tuliyemchagua ndugu huyo kuwa mbunge wetu tukubali apangiwe majukumu na chombo kingine, tena majukumu ya kutuulia watoto wetu?
Na waandishi wa mswada wakijua kuwa kila mwanamke anayetolewa mimba anakabiliwa na madhara ya kiafya na kisaikolojia, anaiagiza serikali kuhamasisha upatikanaji wa huduma ya ushauri nasaha baada ya mwanamke na watoto wa kike kutolewa mimba. Jamani, kama tunajua kitendo fulani kinaleta madhara, kwa nini basi tukitungie sheria? Kwamba eti utoaji mimba utafanyika kufuatia ridhaa ya mwanamke mwenyewe, ni kauli ya kutudanganya. Mbona katika kifungu kinachofuatia, 19 (2) mswada unasema kwamba hata kama ridhaa haitatolewa kutokana na hali ya mja-mzito basi mimba hiyo itolewe tu? Mbona mswada unasema, mhudumu wa afya atakayekataa kutoa mimba atahesabika kuwa ametenda kosa, na akipatikana hatia ataadhibiwa? Sheria hii ni kali kuliko sheria zote za utoaji mimba zilizowahi kutungwa duniani na haina tofauti na ile ya Afrika ya Kusini, ambapo mhudumu afya akikataa kutoa mimba, basi anapata kifungo cha miaka kumi. Hapa kwetu mswada unapendekeza faini ya shilingi milioni moja au kifungo cha miezi sita au vyote kwa pamoja.
7. Sehemu ya sita
Sehemu hii inahusu virusi vya ukimwi, ukimwi na magonjwa mengine ya zinaa. Sina tatizo kubwa na sehemu hii, isipokuwa natilia mashaka adhabu zilizopendekezwa chini ya kifungu cha 23(3). Pamoja na adhabu zilizopendekezwa, mswada utambue kuwa kuna haki za msingi za kibinadamu ambazo zinapaswa ziheshimiwe. Mtu anayo haki ya kukataa jambo fulani, iwapo anaona jambo hilo halina manufaa kwake.
8. Sehemu ya saba
Sioni sababu ya sehemu hii kuwepo katika mswada kwa sababu, mengi ya yaliyoandikwa yanaweza kushughulikiwa na sheria zilizotangulia, kama ile ya Sheria ya Makosa ya Kujamiiana. Kama waandishi wa mswada waliona Sheria ya Ndoa ya 1971 haitoshelezi, basi ingefaa wangeandika maoni ya marekebisho ya sheria hiyo. Kwa vyovyote, kwa kadiri ya maoni yangu, si vema kutunga sheria juu ya sheria. Kama sheria zilizopo hazijafutwa, sioni uhalali wa sheria hii mpya.Au labda kama waandishi walikusudia kuweka vipengele vya adhabu kwa wale watakaokiuka.
9. Sehemu ya nane
Zipo mahakama nyingi hapa nchini ambazo zinashughulikia makosa ya aina mbalimbali. Mswada unapendekeza uundwaji wa Mahakama ambapo watendaji wake watalipiwa na fedha za walipa kodi wote. Ni makosa ya aina gani ambayo, waandishi wa mswada wanaona hayataweza kushughulikiwa na mahakama zilizopo? Kama wanataka Mahakama hiyo itushughulikie sisi tunaosema ukweli juu ya madhara ya vidhibiti mimba, au wanataka kututia magerezani sisi watetezi uhai tunaopinga kwa nguvu zetu zote vitendo vyovyote vya utoaji mimba na sheria yoyote ya kutoa mimba, basi Mahakama itatufunga wengi. Kwa vyovyote vile, Mahakama hiyo itawafunga wengi, pamoja na nasi, watafungwa pia maaskofu wote, mapadre wote, mashehe wote na wachungaji wote ambao wanafundisha kuwa utoaji mimba ni dhambi kubwa mbele ya Mungu na jamii. Vile vile mahakama hiyo itawafunga mapadre wote na baadhi ya wachungaji na mashehe wanafundisha kuwa ni dhambi kutumia vidhibiti mimba. Na nadhani, sheria inadhamiria kuliadabisha zaidi Kanisa Katoliki kwa misimamo yakethabiti juu ya maadili ya binadamu yanayofunuliwa na dhamiri safi na imani juu ya nafasi ya Mungu katika maisha ya wanadamu. Na ndivyo ilivyo, hata huko Marekani, kwa sasa Raisi Obama amepitisha sheria ya kuvilazimisha vituo vyote vya afya kuweka vidhibiti mimba kama moja ya huduma muhimu ya kiafya. Kanisa Katoliki lilipopinga, sheria hiyo imelegezwa kidogo, ili kuheshimu dhamiri za wahudumu wa Kikatoliki ambao kwa mafundisho yao hawapaswi kutoa vidhibiti mimba.
10. Hitimisho
Katika ulimwengu wetu wa leo ambapo maadili yamekengeushwa, vitendo vilivyokuwa vinaonekana kutofaa hapo kale, sasa vinaonekana kufaa, na anayepinga vitendo hilo anaonekana mbaya. Ndiyo maana tangu kale tulijifunza na kila mmoja alijua kuwa vitendo vya utoaji mimba ni vibaya, kwani vinakiuka haki ya msingi ya binadamu ya kuishi. Na aliyetokea kumwua mwingine alionekana kutenda kosa na akipatikana na hatia alikuwa anatupwa jela, tena miaka mingi. Leo hii, dhamiri zimebutushwa na sheria za kuua binadamu wengine zinatungwa, na anayepinga sheria hizo anaonekana ametenda kosa na ndiye anayetupwa jela. Kwa hiyo, kuua sasa ni haki ya kisheria na mahakama zitekeleze wajibu wake wa kuwahukumu na kuwafunga wale wanaotetea uhai wa binadamu. Huko nyuma, jamii zilikemea sio tu mauaji ya watoto kabla ya kuzaliwa, hata mauaji ya watu wenye ulemavu, wazee, na wagonjwa. Leo hii, sheria zinatungwa ili kuwaua wagonjwa, walemavu na hata wazee. Tena sheria zinataka kuwatambua watu hao tangu wakiwa matumboni mwa mama zao, wakigundulika kuwa wana-ulemavu wa kimwili au wa kiakili, basi wauawe kabla hawajaliona jua.
Huko nyuma vitendo vya uasherati na umalaya vilikemewa na hata kumchukulia hatua za kisheria mhusika. Leo hii vitendo vya uasherati na umalaya vinaruhusiwa kama haki ya binadamu. Kila anayepinga vitendo hivyo anaonekana ndiye mkosaji na siyo ajabu akatupwa jela. Huko nyuma makuzi mema yaliangaliwa katika kujiheshimu, kutunza usafi wa moyo na hata ubikira hadi siku ya ndoa. Leo hii, watoto wanahamasishwa kujiingiza katika vitendo vya kutojiheshimu, vitendo vya ngono na hata kuwalazimisha kutumia kemikali zenye kuwadhuru kiafya na kisaikolojia. Sisi watetezi uhai na viongozi wa dini tunaposimama na kupinga elimu na vitendo hivyo kwa watoto wetu, tunaonekana tumetenda kosa na wenye kustahili kusulubishwa. Huko nyuma wazazi walikuwa na haki na wajibu juu ya malezi ya watoto wao. Leo hii wazazi wanaambiwa hawana mamlaka juu ya watoto wao, na sheria zinatungwa kuwazuia wazazi kuingilia faragha ya watoto wao.
Dunia ya leo imegeuka sana. Yale mambo yote ya Ki-Mungu na utu bora sasa yametupwa kando, na badala yake dunia ya leo inachuchumia yale mambo ya Ki-Shetani, ambaye ni mwongo na mwuaji tangu kale. Shetani ndiye mwanzilishi wa kifo duniani. Shetani ndiye amesababisha magonjwa kwa binadamu. Shetani ndiye mwasisi na mhamasishaji wa vitendo vya utoaji mimba. Sababu yake ni moja tu, shetani anafurahia kunywa katika damu za binadamu, tena zaidi sana damu za binadamu wadogo kabisa wasiozaliwa na wasio na hatia.
Emil Hagamu
Mkurugenzi wa Pro-Life Tanzania
February 28, 2012