Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimetoa taarifa ya nusu mwaka, Januari – Juni 2013 kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Tanzania. Kwa jumla taarifa ya kituo hicho ni nzuri kwani imetokana na utafiti makini. Sisi katika Shirika la Kutetea Uhai [Pro-Life] Tanzania tumepokea na kuunga mkono mengi yaliyotolewa na taarifa hiyo.
Hata hivyo kipengele kinachohusu ‘haki ya kutoa mimba kiusalama’ [safe abortion] hatukubaliani nacho na tunakipinga kwa nguvu zetu zote. Kwa bahati mbaya sana kipengele hicho kimetolewa katika muktadha wa ‘haki ya kuishi’. Katiba ya Jamhuri wa Tanzania [1977], ibara ya 14 inasema, “Kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka kwa jamii hifadhi ya maisha yake…”
Ukizingatia ibara hiyo, jambo la kwanza tunalopaswa kulielewa ni tasfiri ya ‘mtu’. Kwa kadiri ya tafsiri ya watetezi uhai, ‘mtu’ ni binadamu yeyote aliye hai. Katika maumbile asilia, uhai wa mtu huanza tangu wakati wa kutungwa mimba na unadumu hadi kifo chake cha kawaida. Kwa hiyo haki ya kuishi ni haki ya kila mtu, yule aliyezaliwa na yule ambaye bado hajazaliwa. Na kwa kweli mtu hawezi kuzaliwa, na kupata haki ya kuishi, kama kwanza hakuwepo kabla yake akiwa hai. Ndiyo kusema, ‘mimba ni binadamu [mtu] hai katika tumbo la mama. Mtu huyo, kwa hiyo, anayo “haki ya kuishi na kupata kutoka kwa jamii hifadhi ya maisha yake…” Jamii inayomzunguka mtu [binadamu] huyu ni kwanza wazazi wake, ndugu zake, majirani, taasisi mbalimbali na miundo ya sheria na taratibu mbalimbali za kimila na za kiserikali.
Kila tumwonapo mama mja mzito, mwenye mimba, tunafahamu kuwa wapo watu wawili – mama [mwanamke] mwenye kubeba hiyo mimba, yaani mwenye mtu [binadamu] ndani ya tumbo lake na mtu [binadamu] huyo ndani ya tumbo la mama yake. Kila mmoja kati ya hao wawili wana haki ya kuishi. Mama ana haki ya kuishi na huyo aliyomo ndani ya tumbo lake ni mtu mwenye haki ya kuishi sawa na mama yake. Hakuna mwenye haki zaidi kuliko mwingine. Wote wana haki sawa ya kuishi na kupata kutoka jamii hifadhi ya maisha yao. Haki ya kuishi haitegemei sheria yoyote. Sheria zipo kwa sababu binadamu [watu] wapo. Kwa hiyo siyo sahihi kuufaya uhai wa mtu utegemee sheria kama inavyosema Katiba ‘kwa mujibu wa sheria’. Uhai wa mtu upo hata kama sheria haipo. Na katika historia binadamu alianza kuishi kabla ya kuwepo kwa sheria. Sheria zilikuja ili kuweka utaratibu na kuwezesha mahusiano bora ya kibinadamu na kulinda amali za jamii na taifa.
Maana ya kutoa mimba ni ipi? Hata kama hutaki kukubali, ukweli msingi utabaki kuwa, ‘kutoa mimba maana yake kumwua kwa makusudi binadamu [mtu] ambaye bado hajazaliwa’, yaani, aliyemo katika tumbo la mama, kwa ajili ya kutimiza hamu ya kusudio fulani. Na tukimwangalia mtu [binadamu] katika mgawanyo wa kirika; yaani, utoto, ujana, utu-uzima na uzee, mtu aliyemo katika tumbo la mama ni mtoto mdogo, aliye hai ambaye ameanza safari ya kuishi wake kuelekea hatua nyingine za kuzaliwa, utoto, ujana, utu-uzima na uzee. Umri wako wa leo unahesabika tangu siku ile ya kutungwa mimba, na wala sio tangu siku ya kuzaliwa kama ambavyo wanadamu wamejidanganya. Siku ya kuzaliwa ni moja ya matukio muhimu katika uhai wa binadamu. Nataka kusema kuwa, huwezi kuwepo leo, kama hukuwapo kwanza katika tumbo la mama yako, ambapo ulijulikana kama ‘mimba’. Kumbe, kama mama yako angeamua ‘kutoa mimba’, yaani kukuua wewe ulipokuwa mimba, usingalikuwapo leo.
Haki ya kutoa mimba kiusalama maana yake nini? Kwa kadiri ya mashabiki na watetezi wa vitendo vya utoaji mimba, utoaji mimba salama humaanisha kuwa, wakati mtoto anauwa katika tendo la utoaji mimba, mama yake anakuwa salama, ikimaanisha kuwa hapati madhara wala hafi. Lakini je upo utoaji mimba salama? Wanazuoni mbalimbali waliobobea katika taalumu ya mimba wanatujulisha kuwa hakuna utoaji mimba ulio salama. Katika kila kitendo cha utoaji mimba, mmoja anauawa, mmoja anadhurika na mmoja analipwa. Ndiyo kusema kuwa, katika tendo la utoaji mimba, mtu [binadamu] aliyemo katika tumbo la mama anauawa; mama mwenyewe anayemtoa mtoto huyo kafara kwa mwuaji anadhurika na mwuaji halisi, yaani daktari, nesi au mtu mwingine yeyote yule anapata malipo, ujira kwa kazi yake ya kuua. Katika vitendo vya utoaji mimba, kwa hiyo, hakuna aliye salama. Mtoto anakufa. Mama anadhurika kimwili na kisaikolojia. Daktari licha ya kupata ujira wake anadhurika kisaikolojia. Kwa vile, vitendo vya utoaji mimba vinaelekezwa kwa binadamu, aliye mdogo sana na asiyeweza kujitetea, na kwa vile utoaji mimba huhusisha umwagikaji wa damu nyingi, na kwa vile vitendo hivyo vinafanywa na binadamu walio na nguvu kuelekea kwa binadamu dhaifu, basi, vitendo vyote vya utoaji mimba ni vya kikatili, vya kimabavu tena vyenye kumwaga damu nyingi na vya kinyama. Katika hali ya kawaida akili ya ya binadamu inaelekezwa katika kuhifadhi uhai wa mwingine, na si kuundoa. Ndiyo sheria za nchi humwadhibu vikali mtu anayemwua mwingine, kwa kifungo cha maisha na pengine kunyongwa. Kama hiyo ndiyo adhabu apataye mtu anayemwua mwingine, basi kila mtoaji mimba anastahili adhabu hiyo.
Watetezi wa kifo wanatumia pia dhana ya utoaji mimba salama, wakimaanisha utoaji mimba holela unaofanywa bila utaalamu na katika mazingira hatarishi. Katika baadhi ya nchi matangazo huandikwa yenye ujumbe “hapa utapata huduma ya utoaji mimba iliyo salama, isiyokuwa na maumivu, inayochukua muda mfupi na ya gharama nafuu”. Hoja zitolewazo kuwa utoaji mimba wa aina hiyo ni kuwa hausababishi maumivu na vifo kwa akina mama. Lakini takwimu kutoka nchi zile zilizoruhusu utoaji mimba kiusalama, yaani kitaalamu zinaonyesha kuwa wanawake wanaokufa kwa utoaji mimba salama ni wengi zaidi kuliko katika nchi ambazo sheria zake zinazuia kabisa utoaji mimba, na ambako ndiko wanadai kuna utoaji mimba usio salama. Vilevile tukumbuke kuwa siyo kwamba wanawake wakiruhusiwa kuua watoto wao kiusalama, basi hawatakufa. Wanawake watoao mimba kiusalama watakufa na wakati huo huoa wale watoa mimba pasipo salama watakufa kwani siyo kila mwanamke mwuaji atakuwa na uwezo wa fedha za kumwulia mtoto wake kiusalama. Kwa hivyo vifo vya wanawake watoaji mimba vitaongezeka.
Isitoshe, upiganiaji utoaji mimba salama unapofanywa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, unakiuka lengo la uwepo wa kituo hicho. Tulitegemea Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kingepigania kuunga mkono sheria zinazolinda haki ya kuishi, kama ambavyo Katiba ya Jamhuri ya Mwungano wa Tanzania [1977] inasema. Haki ya kuishi ni haki ya mwanzo na ya msingi kwa kila mtu [binadamu] na ambamo haki nyingine zote husimama. Na hii ni haki ya kila mtu, yule ambaye amezaliwa na yule ambaye hajazaliwa. Hakuna mwenye mamlaka wala uhalali wa kukiuka haki hiyo. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinapotetea haki ya kutoa mimba kiusalama kina maana kuwa mtu [mama] ana haki ya kuishi na mtu[mtoto] ndani ya tumbo la mwanamke ana haki ya kuuawa ili mradi mauaji hayo yafanyike kiusalama, yaani mtu [mtoto] afe na mtu [mama] apone. Kama hivyo ndivyo inavyomaanisha, basi Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kitakuwa kinakiuka lengo msingi la uwepo wake, yaani kupiganiana haki za kila mtu [binadamu].
Vitendo vya utoaji mimba ni viovu kwa asili na tabia yake. Kukubali kuwa mtu mmoja anaweza kumwua mwingine, ili mtu huyo anayeua asidhurike au kufa ni vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu vinavyopaswa kulaaniwa na kila mtetezi wa haki za binadamu. Na kwa tabia ya uovu, ukisharuhusu uovu mmoja, basi utazaa uovu mwingine na hivyo kuyafanya mauaji ya watu wasioweza kujitetea kuwa sehemu ya utamaduni kengeushi wa binadamu. Wanawake watakuwa wamefunguliwa milango ya kuua watoto wao [mimba] hata kwa visingizio vidogo tu, kama vile afya mama, uhai wa mama, ulemavu wa mimba, mimba za ndugu hata mimba za ubakaji. Katika undani wake vitendo hivyo vitabadilisha misingi ya maadili iliyolinda jamii kwa miaka mingi ya kulinda na kutetea uhai wa binadamu, sasa tutageuza vitendo vya mauaji ya watoto kama tiba kwa akina mama wajawazito. Itakuwa kama hivi, “kwa kuogopa vitendo vya kutoa mimba visivyo salama, dawa yake ni kuruhusu utoaji mimba ulio salama; kwa kuhofia mimba zinazohatarisha afya ya mama au uhai wa mama, tiba yake ni kuua hiyo mimba ili mama apone; kwa ulemavu wa mimba, mimba za ndugu na mimba za ubakaji, tiba yake ni kuziua hizo mimba ili kukwepa aibu katika familia. Hatudhani kwamba hilo ni suluhisho la kweli. Suluhisho la kweli ni kuwatia hatiani wauaji wote. Daktari atumie utaalamu na karama yake kumhudumia mama mgonjwa ili hali ni mja mzito au mama atishiwaye na kifo kutokana na mimba aliyonayo. Daktari akiamua kumwua mtoto ili mama yake apone atakuwa amekiuka misingi ya maadili ya tiba. Hapa nchini kuna sheria itokanayo na makosa ya ubakaji na hata mimba za ndugu. Tunakishauri Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kuhimiza utekelezwaji wa sheria hizo.