Tuanze mada yetu kwa nukuu kutoka Maandiko Matakatifu:
“Kumbuka kwamba, katika siku za mwisho kutakuwa na nyakati za taabu. Watu watakuwa na ubinafsi, wenye tamaa ya fedha, wenye majivuno, wenye kujiona, wenye kumtukana Mungu, wasiowatii wazazi wao, wasio na shukrani na waovu; watatokea watu wasio na upendo moyoni, wasio na huruma, wachongezi, walafi na wakali; watachukia chochote kilicho chema; watakuwa wahaini, wakaidi na waliojaa kiburi; watapenda anasa kuliko kumpenda Mungu…” (2Tim.3:1-5)
Je hayo yasemwayo na Maandiko Matakatifu hayapo hizi nyakati zetu? Katika mada yetu kama watetezi uhai, ninapenda kuchukua machache tu katika hayo –
‘watu watakuwa na ubinafsi’; ‘wenye tamaa ya fedha’; ‘wenye kumtukana Mungu’; ‘wasio na shukrani na waovu’; ‘watatokea watu wasio na upendo moyoni’; ‘wasio na huruma’;’ watachukia chochote kilicho chema’; ‘watapenda anasa kuliko kumpenda Mungu’.
Nimeanza na nukuu hiyo kwa sababu mtakumbuka miaka kama mine iliyopita tulisimama kidete kupinga uwezekano wa serikali yetu kutunga sheria ya kutoa mimba kama ilivyokuwa inashinikizwa katika ITIFAKI YA MAPUTO (Maputo Protocol) iliyoandaliwa na mashirika ya kutoa mimba huko London, Uingereza. Mnakumbuka jinsi tulivyokusanya maoni ili kupata msimamo wa Watanzania kuhusu jambo hilo. Mnakumbuka tulivyokwenda Bungeni kuliomba Bunge kutotunga sheria ya kuua kizazi cha baadaye cha taifa letu. Tunamshukuru Mungu, kwa neema zake tulifaulu kuzima njama zile.
Miaka miwili baadaye, njama hizohizo za kutaka kuilazimisha serikali yetu kutunga sheria ya kutoa mimba iliibuka tena kupitia Mswada wa Uzazi Salama (The Safe Motherhood Bill, 2012). Kwa kweli ni Mungu tu aliyetuwezesha kufaulu kushinda njama hizo tena. Sasa hivi njama hizo zimezuka tena, tena kwa chinichini zikitumia taasisi za afya katika kufanikisha jambo hilo. Katika kupitia mitandao ya intaneti nimefaulu kusoma njama hizo zinazofanywa kwa msukumo kutoka mashirika ya nje ya nchi yetu yakishirikiana na taasisi na mashirika ya ndani ya nchi. Katika kutafakari kwa kina, nimegundua kuwa tangu enzi za Itifaki ya Maputo, kisha Mswada wa Uzazi Salama, na sasa njama za chini chini zinazoendelea, watu wanaosukuma ajenda ya kutungwa sheria ya utoaji mimba hapa nchini kwetu, wanachukia sana sheria zetu zinazolinda na kusimamia uhai wa binadamu. Wanatamani siku moja sheria hizo zibadilishwe ili wanawake waweze kuua watoto wao kabla ya kuzaliwa kwa kibali cha Bunge letu.
Ndugu Watanzania mtambue kuwa msukumo huu wa kutungwa sheria za kutoa mimba unaasisiwa na watu wa nchi za Magharibi na Mashariki. Katika bara la Ulaya kwa mfano, nchi zote isipokuwa Malta na Poland ndizo hazijatunga sheria za kutoa mimba. Wananchi wa Ireland walikataa katakata kutunga sheria ya kutoa mimba. Lakini baada ya mabadiliko ya ungozi wa kiserikali, ambapo chama chenye mlengo wa kushoto (kiliberali) kutwaa madaraka, kilifanya kila lililowezekana na hatimaye Bunge la Ireland limesalimu amri kwa kutunga sheria ya kutoa mimba mwaka huu. Mnafahamu Marekani ilitunga sheria ya kutoka mimba mnamo 1973, ikitanguliwa na Uingereza 1967 ambayo nayo ilitanguliwa na Urusi 1922. Kwa sasa mataifa hayo yanalishambulia bara la Afrika ambalo nchi nyingi zina sheria za kulinda uhai, ili zibadilishwe na kuruhusu utoaji mimba. Katika kufanikishwa azma hiyo wanawatumia vibaraka na waganga njaa waliomo ndani ya nchi za Kiafrika.
Wakati naandika mada hii nilipigiwa simu na Mkurugenzi wa shirika la kutetea uhai la Uganda, ‘Human Life International Uganda’, Padre Jonathan Opio, akinieleza kuwa, mashambulizi ya kubadilisha sheria za kutetea uhai huko Uganda yamepamba moto. Na kwa sasa wanatumia taasisi za afya katika kufanikisha jambo hilo. Mara moja nami nikagundua kuwa hata hapa kwetu Tanzania, msukumo wa utoaji mimba sasa umehamia katika taasisi za afya, ambapo wakuu na washirika wa taasisi hizo wanaulizwa kama ipo haja ya kubadilisha sheria za Tanzania kuhusu utoaji mimba. Kwa sasa, wanasema, sheria ya Tanzania inaruhusu utoaji mimba kama mimba hiyo inahatarisha uhai wa mama. Kwa kutumia takwimu za wanawake ambao mimba zimetoka, na madhara yatokanayo na vitendo hivyo, wanataka kusukuma ajenda ya utoaji mimba salama. Tutajadili zaidi hapo baadaye jambo hili.
Ndipo nikakumbuka kumbe wenzetu watetezi wa kifo, hata kama wameshindwa kwa hoja, hawalali na wala hawakati tamaa, bali wanaibua mikakati mingine, ili mradi inatimia kiu yao ya kuona kuwa damu za watoto wachanga waliomo katika matumbo ya mama zetu inamwagika kwa gharama yoyote ile. Ndoto zao ni kuona kuwa siku moja Tanzania inatunga sheria ya kutoa mimba. Kama hilo litatimia basi ufahamu kuwa wametumia uvivu wetu wa kufikiri au wametumia kisingizio cha umaskini wetu wakatujaza mapesa, wakatupatia na magari, wakatupatia na ofa za kusafiri kwenda katika nchi zao, au hata wametumia ulimbukeni wetu wa kuiga kila kitu kutoka kwao hata kama ni cha kipuuzi kiasi gani. Mfano kama Serikali itapeleka mswada Bungeni wa kuua kizazi chetu cha baadaye na Bunge letu likaridhia na kutunga sheria hiyo, ni moja ya upuuzi ninaouzungumzia. Watetezi uhai na watu wenye mapenzi mema popote mlipo chukueni tahadhari, jitayarisheni kupinga chochote kilicho kibaya kwa taifa letu.
Na hapa nikakumbuka tena Maandiko Matakatifu, ambapo Mtume Petro anatutahadharisha kuhusu jambo hilo:
“Muwe macho; kesheni! Maana adui yenu, Ibilisi, huzungukazunguka kama simba angurumaye akitafuta mawindo. Muwe imara katika imani na kumpinga, mkijua kwamba ndugu zenu pote duniani wanapatwa na mateso hayohayo” (1Pet.5:8-9)
Hilo ni kweli, kwani adui yetu Ibilisi anataka kutushawishi kuwa ipo haja ya kurekebisha sheria kuhusu utetezi wa uhai ili kuruhusu utoaji mimba. Waraka huu wa Mtume Petro unatuhusu sote tunaoitakia mema nchi yetu. Kwa karne na karne Watanzania wameuenzi uhai, wakaulinda kwa nguvu zao zote na wakaustawisha ili tuongezeke. Sasa kwa vile Ibilisi anafahamu kuwa akiomba moja kwa moja sheria ya kutoa mimba atashambuliwa na watetezi uhai na wapenda uhai wengine, basi anaomba kidogokidogo na hatua kwa hatua kwa saikolojia ya huruma kwa wanawake. Ndani ya ‘huruma’ hiyo ipo hila ya mauaji yanayoelekezwa kwa watoto wachanga ambao bado hawajazaliwa. Kwa kuanzia anajenga hoja hivi, ‘Kwa kutambua kuwa wanawake wengi wanajihusisha na utoaji mimba usio salama ambao unahatarisha afya na kuwasababishia vifo, je, hamwoni kuwa ni wakati mwafaka sasa kurekebisha sheria ili kuruhusu utoaji mimba salama’? Akiwa anafahamu kuwa hilo litapingwa vikali, basi anaomba kwa upole wa hila; Je, isingekuwa vema kubadilisha sheria zenu juu ya uhai, ili kuruhusu utoaji mimba kwa wanawake wenye kukabiliwa na mazingira yafuatayo:
a. Kama afya ya kimwili ya mwanamke ipo katika hatari
b. Kama mwanamke ana tatizo la afya ya akili
c. Kama afya ya akili ya mwanamke ipo katika hatari
d. Kama msichana/mwanamke bado yuko shule
e. Sababu za kiuchumi (mfano, hawezi kutunza mtoto)
f. Kama mwanamke/msichana hajaolewa
g. Kama ujauzito unatokana na kubakwa
h. Kama ujauzito umetokana na ndugu wa karibu
i. Kama ujauzito umetokana na vidonge vya uzazi kushindwa kufanya kazi
j. Kama mtoto atakuwa kilema
k. Kama mwanamke hataki ujauzito
l. Kama kuna sababu nyingine zaidi ya hizi
Ukisoma orodha ya sababu hizo kwa makini, unaweza kutambua kuwa watetezi wa sheria ya utoaji mimba wanasema utoaji mimba uruhusiwe kwa sababu yoyote ile. Maana yake ni kuwa hata kama mwanamke atapata mabadiliko ya kimahusiano na mume wake kutokana na uja-uzito, basi mwanamke huyo atoe hiyo mimba kwani watetezi wa mauaji watakuambia kuwa ‘akili ya mwanamke ipo hatarini’.
Na kwa lugha ya ujanja kabisa, mashabiki hao wa maangamizi ya watoto kabla ya kuzaliwa wanatueleza kuwa tayari maandalizi ya kufanikisha ukatili huo yamekwishafanyika. Njia za kufanikisha mkakati huo zimetajwa:
1. Kuwa na chumba cha faragha kwa ajili ya huduma baada ya mimba kutoka
2. Kuimarisha/kukuza miundo mbinu
3. Kuwa na watu waliopata mafunzo zaidi
4. Kuwa na ngazi za chini za vituo vyenye uwezo wa kutoa huduma baada ya mimba kutoka
5. Upatikanaji wa vifaa/dawa (kifaa cha MVA, antibiotiki, damu, dawa za maumivu)
6. Kutoa taarifa juu ya uzazi wa mpango na njia zilizopo
7. Kutoa utaratibu wa kutoa huduma kwa mgonjwa baada ya mimba kutoka
8. Kutoa kifuta jasho/motisha kwa wafanyakazi (mf. fedha, kozi ya kupiga msasa, na vifaa)
Na tena hata vifaa vya kutolea mimba vipo na tayari vinafanya kazi. Kinachosubiriwa ni sheria ya kutekeleza hayo pasipo kipingamizi, na mpinzani atakayejitokeza basi ahesabike kuwa amevunja sheria. Yaani, wauaji watalindwa na sheria na watetezi uhai wataonekana wahaini kwa kupinga sheria hizo za mauaji na hivyo watatupwa magerezani. Na vifaa hivyo vimetajwa kuwa ni pamoja na:
1. Kifaa cha ncha kali (sharp curette, D&E, D&C)
2. MVA (manual vacuum aspiration)
3. Electric vacuum aspiration
4. Misoprostol tu
5. Misoprostol na mifepristone (Mifegyne)
6. Vidonge vya uzazi wa mpango au dawa nyingine za vichocheo
7. Antibiotic
8. Dawa ya kuchoma (uterotonic, e.g. Oxytocin, ergometrine)
Kama nilivyosema hapo awali watetezi wa utoaji mimba wanatumia mbinu ya kisaikolojia ya kujenga huruma kwa wanawake kutokana na matatizo ya utoaji mimba, ndiyo maana wanaona kuzungumzia huduma na tiba kwa wanawake ambao mimba zimezotoka au zilizotolewa kienyeji pasipo usalama. Wanafahamu kuwa Watanzania sio wadadisi, na kwa kweli kwa vile huduma hii ni muhimu wakati huu ambapo wanawake wengi na wanajihusisha na vitendo vya utoaji mimba, wito wa kuwasaidia wanawake watesekao baada ya kutoa mimba ni jambo muhimu kwa sasa. Ni katika muktadha huu natoa tahadhari kuwa tusipokuwa makini, tukakubali mtego wao, basi ajenda yao ya siri itapita bila kupingwa. Hapa ndipo tunapotahadharishwa na Mtume Petro kuwa tuwe macho, tukeshe kwani adui yetu halali yuko macho wakati wote akizungukazunguka kutafuta mawindo. Na watu hao wa Ibilisi ndio wanaosemwa na mwandishi wa barua kwa Timotheo - ‘watatokea watu wasio na upendo moyoni’; ‘wasio na huruma’; watachukia chochote kilicho chema’
Watu hao wanajitokeza kwetu kama wanawapenda sana wanawake, kwamba eti wanajali sana afya na uhai wa wanawake, kumbe ndani ya mioyo yao zimejaa hila za kuangamiza watoto ambao bado hawajazaliwa. Hawatakuwa na huruma kwa mauaji yatakayotokea kwa watoto hao. Hawapendi yaliyo mema, yaani kutunza uhai, kilicho kitu chema na chenye thamani kubwa kabisa kupita kitu kingine chochote. Wao wanapenda kifo, yaani kitu kilicho kibaya; ni ajabu iliyoje. Kwa asili yao watu hao hawana shukrani kwa zawadi ya uumbani na ni waovu wa kupindukia.