SR. DR. BIRGITTA SCHNELL, O.S.B KAMA NILIVYOMFAHAMU
NA EMIL HAGAMU
Ni muda wa majuma machache tu yamepita tangu atutoke mpendwa wetu Sr. Dr. Birgitta Schnell, OSB. Nimeona nichukue muda kidogo kuandika, tena kwa uchungu mkubwa, ninavyomfahamu mpiganiaji gwiji wa uhai na familia hapa Tanzania. Sr. Dr. Birgitta Schnell, OSB alifariki alfajiri ya kuamkia Dominika, Oktoba 27, na kuzikwa Jumatatu, Oktoba 28 katika makaburi ya Abasia ya Ndanda.
Mimi binafsi nimemfahamu Sr. Birgitta kwa miaka 30, yaani tangu 1983 nilipohamishiwa Shule ya Sekondari Ndanda nikitokea Kigoma Sekondari nilikokuwa nafundisha. Mimi na mke wangu tulipata mafundisho ya uzazi wa mpango kwa njia ya maumbile kutoka kwake mnamo 1987 na tangu muda huo tumekuwa wafuasi waaminifu na mahiri katika kutumia njia hiyokwa ajili si tu ya kupanga uzazi, lakini zaidi sana kwa ajili ya kuimarisha familia yetu.Mke wangu aliamua kujifunza njia hii kwa kina zaidi kwa ajili ya kuwasaidia majirani na wengine waliohitaji msaada wake mnamo 2008 na mwaka huohuo alijifunza kozi ya walimu na kuhitimu vizuri. Kwa sasa amekuwa mwalimu mzuri kwa akina mama wanaomjia kutaka kujua na kutumia njia hii katika ndoa zao.
Akiwa mtaalamu na mkufunzi wa njia ya kupanga uzazi kwa kutumia maumbile iitwayo, Billings Ovulation Method, Sr. Dr. Birgitta alitunukiwa cheti cha umahiri katika ufundishaji na shirika la kimataifa la uzazi wa mpango liitwalo WOOMB International. Aliteuliwa kusukuma mbele njia hii hapa Tanzania na kwingineko Afrika na waliokuwa waanzilishi, mabingwa na watetezi kimataifa wa njia hiyo, Madaktari Bwana na Bibi John na Evelyn Billings wa Australia tangu 1952. Tangu kutunukiwa cheti cha ubingwa wa njia hiyo, Sr. Dr. Birgitta Schnell alijitoa kwa moyo wake wote kufundisha na kuendeleza njia hiyo hapa Tanzania na Afrika Mashariki, akiunganisha utume wa utetezi uhai na familia.
Amekuwa mstari wa mbele katika kupambana na falsafa na programu za utamaduni wa kifo ambazo aliziona zinainyemelea nchi yetu. Mnamo 1988 alialikwa na Chama cha Wanataaluma Wakatoliki, [Christian Professionals of Tanzania] kuwasilisha mada ya ‘udhibiti wa ukuaji wa idadi ya watu duniani’ katika kongamano la kitaifa lililofanyika kule Dodoma. Mimi nilikuwa mshiriki, mwanataalumawa ualimu kutoka Ndanda. Nakumbuka Sr. Dr. Birgitta alitugawia vijitabu na vipeperushi vingi vyenye kueleza mada mbalimbali kuhusu uhai, familia, elimu ya ngono, vidhibiti mimba, kutoa mimba, kufunga kizazi na udhibiti wa idadi ya watu.
Nikiwa mfuatiliaji mzuri wa kongamano hilo, na nikiwa msomaji mahiri wa vijitabu na vipeperushi alivyotugawia Sr. Birgitta, niliamua ‘kuokoka’ na kujiunga na harakati za utetezi uhai na kushirikiana na Sr. Birgitta katika kufundisha Injili ya Uhai nchini Tanzania. Mwishoni mwa mwaka uliofuata, 1989 nilimwaga manyanga ya ualimu na kutokana na wito huu mpya nikakubali kuajiriwa kufanya kazi kama Mratibu wa Taifa wa Christian Professionals of Tanzania. Na kwa kutumia nafasi hiyo, niliimarika zaidi katika harakati zangu za utetezi uhai na familia na nilitumia kila nafasi ya kujisomea, hasa nyaraka mbalimbali za Kanisa kwa lengo la kupanua uelewa wangu. Niliona kuwa utume wa uhai unanipatia zawadi za kiroho kwa vile unahusiana moja kwa moja na uokoaji wa uhai ulio zawadi na mali ya Mungu. Kwa hiyo ndani ya utume wa utetezi uhai niliona wito wa Mungu u dhahiri kwangu. Na kwa historia yangu ya kuwa mseminari katika Seminari Ndogo ya Likonde na halafu Seminari Kuu Peramiho, nilijiona natajirishwa zaidi na utume huu mpya wa uhai. Baada ya miaka mitatu ya huduma yangu kwa Christian Professionals of Tanzania, niliajiriwa kama Katibu Mtendaji wa Baraza la Walei Katoliki Tanzania na kwa nafasi hiyo nilijiimarisha zaidi katika mafundisho ya kanisa, Biblia Takatifu, katekisimu,nyaraka mbalimbali za kanisa, hasa ‘Humanae Vitae’ ‘Familiaris Consortio’, ‘Donum Vitae’ na ‘Evangelium Vitae’
Wakati natumikia Baraza la Walei Katoliki Tanzania [sasa Halmashauri Walei] katika ofisi zilizokuwa katika majengo ya jimbo kuu la Dar es Salaam, pale St. Joseph’s Cathedral, Sr. Birgitta alikuwa namazoea ya kunitembelea mara zote akiwa na ziara hapa Dar es Salaam. Tulikuwa tunashirikishana mambo mbalimbali ya kitaifa na kimataifa yanayohusu utaduni wa uhai na utamaduni wa kifo. Ni katika kubadilishana mawazo ndipo lilipozuka wazo la kuanzisha chama cha kuhudumia ‘utume’ wa uhai. Ilichukua muda wa miaka walao miwili katika kushauriana na ndipo shirika la kutetea uhai, kwa jina la ‘Pro-Life Tanzania’ lilipozaliwa mnamo Julai 22, 1994 katika ofisi ya Baraza la Walei Katoliki Tanzania. Nilimjulisha Sr. Dr. Birgitta, wakati huo akiwa Ndanda juu ya maendeleo haya. Sr. Dr. Birgitta alifunga safari kuja Dar es Salaam kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa kuanzishwa shirika hili, na alipoingia ofisini kwangu alionyesha furaha kubwa na kutamka maneno haya akimnukuu mzee Simeoni:
“Sasa, Bwana, umetimiza ahadi yako,
waweza kumruhusu mtumishi wako aende kwa
amani.
Maana kwa macho yangu nimeuona
wokovu utokao kwako,
ambao umeutayarisha mbele yawatu wote…” (Lk.2:29-31)
Sr. Birgitta alilipenda shirika hili kwa moyo wake wote. Alishiriki mikutano yote tuliyomwalika, akiwa mtoaji mada mkuu. Kwa njia yake tulijifunza mengi mno yasiyo na ukomo. Alitufundisha jinsi ya kumtambua adui wa uhai na kumkabili. Alitufundisha namna ya kufikisha ujumbe wa uhai kwa wakubwa wa kanisa na serikali. Alikuwa mstari wa mbele kuchangia utume wa uhai kwa njia ya fedha na hata machapisho mbalimbali. Na mwishoni mwa 1995 katika mkutano mkuu uliofanyika Msimbazi Center, Dar es Salaam, Sr. Dr. Birgitta alichaguliwa bila kupingwa kuwa Mshauri wa Taifa wa Pro-Life Tanzania, nafasi aliyoitumikia kwa uaminifu hadi Mungu alipomwita katika makao yake ya milele. Alitushauri katika mengi, namna ya kuandaa maandamano ya amani, namna ya kuwasilisha mawazo yetu serikalini na hata bungeni na namna ya kufanya kazi na viongozi wa kanisa.
Mapema 1998 Sr. Dr. Birgitta alifika ofisini, safari hii akiwa na wazo jipya. Aliniambia hivi, Bwana Hagamu, kwa vile sasa Pro-Life Tanzania imeimarika na inafanya kazi yake vizuri, nafikiri sasa tuanzishe shirika lingine ambalo litajizatiti katika kufundisha uzazi wa mpango na kuandaa walimu wa uzazi wa mpango, na nafikiri tukishirikiana tutasonga mbele zaidi”. Sikuwa na cha kusema, bali nilijawa na furaha kuona kuwa, kwa kuunganisha nguvu zetu tutakuwa imara zaidi katika kutetea uhai na familia hapa Tanzania, kama ambavyo Sr. Birgitta alisema, ‘kwa kadiri tunavyokuwa na mashirika mengi ya kutetea uhai na familia, ndivyo hivyo tunavyoimarika zaidi katika utume wetu’. Niliona kwamba wazo hilo halikua tu zuri, bali zaidi sana lilikuwa la kinabii nani Baraka kwa utume wa uhai hapa Tanzania.
Tulianza kupanga namna shirika hilo litakavyokuwa. Baada ya kushauriana kwa muda mrefu kidogo, Sr. Birgitta alirudi Ndanda akiwa na mawazo fulani tuliyoyaweka pamoja. Akiwa Ndanda alifanyia kazi mapendekezo tuliyotoa na kwa neema ya Mungu aliyaunganisha mawazo hayo pamoja na yale aliyopata kutoka kwa watetezi uhai wa hospitali ya Ndanda akafaulu kutengeneza rasimu. Aliporejea tena Dar es Salaam, tuliipitia rasimu hiyo nami niliridhika kuwa ni nzuri na kwa mguu wake aliipeleka Wizara ya Mambo ya Ndani na kusajiliwa kwa jina la UIMARISHAJI WA FAMILIA TANZANIA (Family Strengthening Association of Tanzania). Kwa hiyo ulipoanza mwaka 1999 tulikuwa na mashirika dada mawili yaliyoshughulikia uhai na familia hapa Tanzania. Tangu hapo alianza kozi za kufundisha uzazi wa mpango kwa njia ya asili [maumbile] kwa ‘nguvu zake zote’, kwa ‘moyo wake wote’ na kwa ‘akili zake zote’ bila kuchoka na bila kukata tamaa. Na hadi anaaga dunia tayari alikuwa amefundisha walimu wa uzazi wa mpango kwa njia ya maumbile zaidi ya 3000.
Changamoto kubwa aliyokabiliana nayo katika utume huu zilikuwa nyingi, kubwa ni mbili, moja uasi wa baadhi ya wale aliowafundisha, na pili upungufu wa fedha za kuendeshea utume. Kutokana na changamoto hizo, baadhi ya wale aliowafundisha, tena wengine wakiwa karibu sana naye, hata akawagharamia mafunzo nje ya nchi na kuwatuma kushiriki makongamano mbalimbali ya kimataifa, walimwasi na kumgeuka kabisa. Kuasi peke yake kusingemletea Sr. Birgitta maumivu makubwa, lakini kikubwa zaidi ni kwamba walimgeuka kabisa, yaani badala ya kutumikia utamaduni wa uhai, wakaenda kutumikia utamaduni wa kifo, wakishiriki katika vitendo vya utoaji mimba, ugawaji na uwekaji wa vidhibiti mimba na hata kufunga kizazi. Vilevile ukosefu wa fedha za kuendeshea utume umesababisha kusuasua kwa utekelezaji wa maazimio yanayofikiwa katika mikutano mikuu, hasa kuzoroto ufundishaji kwa wale waliopata mafunzo kama walimu wa ‘Billings Ovulation Method’, B.O.M. Ni wazi kabisa uasi huu unatokana na sababu mbili; mosi, uchu wa fedha ambazo wanazipata kutoka mashirika ya kutetea kifo; na pili, baada ya kununuliwa na Ibilisi, uasi wao unakuwa ni mkakati wa kudhohofisha nguvu za utetezi wa utamaduni wa uhai nchini. Kwa kadiri wanavyonaswa wengi katika mtego wa Ibilisi, ndivyo hivyo upinzani dhidi yetu unavyokuwa mkubwa na idadi ya wapinzani inavyoongezeka.
Sr. Dr. Birgitta alisimama imara katika kutetea uhai na familia. Ameandika na kufundisha kwa nguvu zake zote na kwa kiwango kikubwa kuhusu madhara ya utoaji mimba, vidhibiti mimba, ushoga, elimu ya ngono, utafiti katika viini tete na kutengeneza binadamu katika maabara. Katika kitabu chake, na ambacho ndicho kitabu cha kiada kwa kila mwalimu wa uzazi wa mpango kwa njia ya maumbile, “Uimarishaji wa Familia”, siyo tu kwamba anatufundisha njia ya ute ya kupanga uzazi, bali pia anatufundisha umuhimu wa maisha ya familia na madhara ya vidhibiti mimba. Katika kitabu chake, “Binadamu daima ni Binadamu si chombo kamwe”, Sr. Birgitta anatufundisha utakatifu wa uhai na kupingana na majaribia ya kufanyika katika mwili wa binadamu au kuuma binadamu wachanga. Akiwa bingwa wa upasuaji alitumia utaalamu wake wa kisayansi kuendeleza utamaduni wa uhai hapa Tanzania. Akitumia kila nafasi aliyopata, alipinga vikali vitendo vya utoaji mimba na hata sheria za kutoa mimba. Alikuwa alitutolea mifano ya huko Ulaya ambayo watu wake wamepukutika baada ya miaka mimba ya matumizi ya vidhibiti mimba na utoaji mimba. Alikuwa akitutahadharisha maendeleo mapya ya kisayansi ambayo yalikuwa yanapingana na uhai kama vile, kupitia chanjo, vidonge vya kuua uhai mchanga tumboni bila mama mwenye mimba kufahamu, na madawa hatari kwa mwanadamu.
Upeo wa Sr. Birgitta kukerwa na msukumo wa sheria za kutoa mimba, ni pale alipoungana na wanachama wengine 9 kutoka Pro-Life Tanzania ni 2010 wakati tulipokwenda Bungeni, Dodoma kupinga uwezekano wa kutunga sheria ya kutoa mimba, wakati huo ikijulikana kama “Maputo Protocol”. Pamoja naye tuliongea na wabunge, tukampatia kila mbunge makabrasha kuhusu uhai wa binadamu na tukaunda ushirika wa Wabunge Watetezi uhai, unaoongozwa na Mheshimiwa Gaudence Kayombo, Mbunge wa Mbinga Mashariki. Hata hivyo, jitihada za kuingia Bungeni karibu zikwame, kama siyo Sr. Birgitta. Yule Ofisa wa Bunge alituambia, “Shukuruni Mungu mnaye Bibi huyu [Sr. Birgitta] ambaye tunamheshimu sana, basi mnaweza kuingia”.Tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa uwepo wa Sr. Birgitta katika ziara ile, na pia kwa kutuwezesha kufanya kampeni yetu kwa mafanikio makubwa, ambapo mswada ule ulitupiliwa mbali.
Msukumo wa kutaka kutunga sheria ya kutoa mimba haukuishia hapo. Mnamo 2012 mswada mwingine wenye jina “Safe Motherhood Bill 2012” uliandikwa na kutaka kuwasilishwa Bungeni. Wakati huo afya ya Sr. Birgitta haikuwa nzuri, lakini kwa vile bado tulihitaji ushauri wake, Emma Kalunga, Katibu Mkuu Msaidizi na mimi tulifunga safari kumfuata Sr. Birgitta huko Ndanda. Tulikuwa naye kwa siku tatu, na siku zote tulikuwa tukijadili namna ya kuukabili mswada huo. Sr. Birgitta aliandika vipeperushi vingi ambavyo tulivitumia katika kampeni yetu dhidi ya mswada huo. Kwa hiyo, uone jinsi Sr. Birgitta alivyotupenda Watanzania, pamoja na afya yake kutokuwa nzuri, bado alijitoa kwa moyo wake wote kusaidia kuzuia kutungwa sheria ya utoaji mimba. Alionekana dhaifu kiafya, lakini akili na moyo wake vilikuwa imara kwa ajili yetu na kwa ajili ya kumtukuza Mungu.
Sr. Birgtitta alifanya kazi kwa karibu sana na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, akiwa kama mgeni mwalikwa katika kuwasilisha mada mbalimbali au kama mshauri katika masuala ya uhai na familia. Alikuwa akiwagawia maaskofu vipeperushi vilivyokuwa vinatahadharisha juu ya hatari mbalimbali zilizokuwa zinatukodolea macho, kama vile chanjo na madawa. Kwa mfano alionya juu ya chancho ya pepo punda, polio, vidonge vya kuharibu kizazi vya ‘quinacrin’ na hivi karibuni ‘garndasil’.
Akiwa katika mikutano ya vyama vya kitaaluma kama vile ‘Medical Association of Tanzania’ ambako masuala ya utaoji mimba yalikuwa yanajadiliwa, Sr. Birgitta alionekana kuwa mwiba kwa wenzake, kwani muda wote alipingana na wajumbe wenzake akatetea uhai wa mtoto kabla ya kuzaliwa bila woga. Katika ngazi ya serikali, Sr. Birgitta alionekana kuwa shujaa na jasiri asiyekuwa na woga kwani aliweza kusambaza vipeperushi vinavyotetea uhai na hata vile vinavyopingana na uhai kwa kila mmoja, raisi, mawaziri, makatibu wakuu na watu wenye ushawishi. Katika Bunge hakusita kupeleka ujumbe wa uhai na katika mahakama aliwaelimisha mahakimu umuhimu wa kutetea sheria zinazotetea uhai na kutoa sherika kali kwa anayeharibu uhai.
Tumempoteza mpiganaji mkuu katika tasnia ya uhai na familia, mtawa aliyejitolea maisha yake kuuhudumia uhai na kuwa mtiifu kwa mafundisho ya kanisa kuhusu uhai na familia. Kwangu mimi binafsi, Sr. Dr. Birgitta alikua mshauri wangu na familia yangu. Nimejifunza fadhila ya unyenyekevu uliotukuka. Kutoka kwake nimejifunza ujasiri na ushupavu kwa kila jambo jema linalompendeza Mungu. Amenifundisha mambo mengi, kubwa katika hayo ni kuwa unapokabiliana na adui mwenye nguvu kimataifa, mwenye fedha nyingi zisizokuwa na hesabu, mwenye mamlaka ya kukufunga gerezani au hata kukunyonga yafaa kumkabili kitaalamu na kisomi, lakini zaidi sana mwache Mungu afanye kazi ndani yako, ushindi ni wako.
Kwa Pro-Life Tanzania, Sr. Dr. Birgitta alikuwa mfano mkubwa wa kuigwa. Ujasiri wake, nguvu zake na utaalamu wake daima vitabaki kuwa hazina isiyoweza kusahaulika kwa watetezi uhai wote Tanzania. Alikua ananiasa daima kubaki imara katika imani, kuwa na msimamo usioyumba katika kutetea uhai na mwenye kuondoa woga katika kukabiliana na nguvu za utamaduni wa kifo. Katika jambo muhimu sana alikuwa anatumia Kiswahili katika kuleta ujumbe. Kwa mfano aliniambia, “Tukishindwa, shetani atafurahi, tusikubali, tupigane hata tumshinde”. Pro-Life Tanzania daima itamkumbuka kwa majitoleo yake makubwa na mchango wake mkubwa katika kudumisha utamaduni wa uhai hapa kwetu Tanzania. Tumashukuru Mungu kwa zawadi ya mtawa huyu imara na shujaa katika kuwatumikia Watanzania. Tuige mfano wa shujaa huyu aliyefanya kazi kwa uaminifu hadi kufa na bila makuu, na kwa kweli alikuwa mnyenyekevu na mkarimu kwa kila mmoja. Tunaungana na shirika la UFATA kwa kuifanya Oktoba 27 kuwa SIKU YA SR. BIRGITTA.
Mungu aipokee roho yake katika makao yake ya milele.