MJADALA kuhusu ndoa za jinsia moja, umezidi kulitikisa taifa, huku baadhi ya masheikh, maaskofu na makundi mengine ya kijamii, yakiitaka Serikali kuvunja uhusiano na Uingereza iliyotoa shinikizo la kutaka Tanzania iruhusu ndoa za jinsia moja.
Akitoa hotuba ya swala ya Idd katika Baraza la Idd El Hajj, lililofanyika kwenye Msikiti wa Al Faruok, Makao Makuu ya Baraza Kuu la Waislamu (Bakwata), jana Sheikh wa mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, alisema kama Uingereza imezoea ushoga, wasilete vitendo hivyo nchini kwa sababu tu ya kutupa misaada yao.
“Kama wao wamezoea vitendo vya ushoga ni huko huko kwao lakini si Tanzania na kwa uwezo wa Mungu hivi sasa bara la Afrika limekuwa kitu kimoja katika kupinga vitendo hivi vya ushoga,” alisema sheikh huyo wa mkoa.
Katika baraza hilo lililohudhuriwa na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, Sheikh Salum aliupongeza msimamo wa Serikali wa kupinga ushoga.
“Ushoga ni jambo zito hata Mwenyezi Mungu halimpendezi daima na kama Uingereza inataka kutuletea adha hii ni lazima Watanzania wote tuvikatae vitendo hivi kwani vitaliangamiza taifa letu,” alisema Sheikh Alhad.
Alisema kutokana na ukosefu wa maadili na kuacha kumcha Mungu, vitendo vya ushoga vimeshika kasi katika baadhi ya nchi, hali inayoharibu utu.
Kwa upande mwingine, Kurugenzi ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), imetoa mwito kwa Rais Jakaya Kikwete kutumia mazungumzo yake na Mtoto wa Mfalme wa Uingereza, Charles, na mkewe, anayetarajia kufanya ziara nchini hivi karibuni kuukataa ushoga katika Tanzania waziwazi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya CHADEMA, mazungumzo ya Rais Kikwete na Mtoto huyo wa Mfalme wa Uingereza, yatakuwa juu ya mambo mbalimbali, likiwemo suala la ushoga kwani linaweza kuathiri mahusiano ya nchi hizo mbili.
Pamoja na mambo mengine, CHADEMA kupitia taarifa hiyo, imemtaka Rais Kikwete kujadili kauli iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa Benard Membe kuwa Tanzania iko tayari kukubali kukosa misaada yote toka Uingereza ikiwa serikali ya nchi hiyo italazimisha kutungwa kwa sheria ya kuruhusu ushoga, usagaji na ndoa ya jinsia moja.
CHADEMA imesema kuwa inaunga mkono msimamo wa serikali kukataa kufanya mabadiliko ya sheria ya kuruhusu vitendo hivyo ambavyo ni kinyume cha sheria na utamaduni wetu.
“Kwa mujibu wa katiba ya CHADEMA kifungu 3.1.8, kwa falsafa yetu ya nguvu ya umma na itikadi ya mrengo wa kati CHADEMA inaweka umuhimu wa pekee katika familia kama moja ya taasisi muhimu za kijamii. Hivyo, tunapinga vitendo vya ushoga, usagaji na ndoa ya jinsia moja kwa kuwa vinakinzana na misingi ya maadili na uwepo wa familia.”
Kurugenzi ya Mambo ya Nje ya CHADEMA inataka ujumbe mahususi utolewe na Rais Kikwete kupitia ziara hiyo kwani wakati wa kujadiliwa kwa ripoti ya ndani ya mustakabali wa Jumuia ya Madola (Internal Report on the future relevance of Commonwealth) katika Mkutano wa Jumuia ya Madola uliomalizika karibuni, Rais Kikwete hakutoa ujumbe mkali kwa Serikali ya Uingereza wakati wa kujadiliwa kwa masuala ya haki za binadamu tofauti na kauli ambayo serikali iliitoa kupitia vyombo vya habari wakati ujumbe wake uliporejea Tanzania.
“Ni muhimu kwa Rais Kikwete kutumia mazungumzo hayo kufikisha ujumbe kamili wa kupinga masuala hayo kwa niaba ya watanzania,” ilisema taarifa hiyo ya CHADEMA iliyotolewa na Kurugenzi ya Masuala ya Mambo ya Nje.
Katika siku za karibuni, Serikali ya Uingereza imepunguza misaada yake ya kibajeti kwa Tanzania kwa asilimia 30 kutokana na kutoridhishwa na utendaji wa serikali hususan kuhusiana na masuala ya kuboresha mazingira ya kibiashara na kutoa fursa kwa wananchi kuwawajibisha viongozi.
Uamuzi huo wa Serikali ya Uingereza umeelezwa kupitia barua ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Nchi hiyo Andrew Mitchell ya Agosti 3 2011, kwenda kwa Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge la nchi hiyo kuhusu uchumi.
“Ni vizuri pande zote mbili Rais Kikwete na Mwanamfalme Charles wakawaeleza Watanzania kuhusu sababu za ziada za maamuzi haya. Vyanzo mbalimbali vinaeleza kuwa sababu halisi ni washirika wa maendeleo kutoridhika na kasi ya vita dhidi ya ufisadi kwa upande mmoja na kwa upande mwingine Ukanda wa Ulaya (Eurozone) kukumbwa na matatizo ya kifedha.”
Aidha Rais Kikwete atumie mazungumzo ya ziara hiyo kuwaeleza Watanzania mkakati wa nchi kupunguza tatizo la utegemezi ambalo linasababisha nchi kupewa misaada yenye masharti ya kibeberu, ikiwemo kulieleza taifa namna ambavyo nakisi ya bajeti inayotokana na wahisani kupunguza fedha zao kwa Tanzania itaweza kuzibwa kwa kuongeza uzalishaji, mauzo ya nje na kupunguza ubadhirifu katika serikali.
Kutoka Iringa, mwandishi Francis Godwin anaripoti kuwa viongozi wa dini ya Kiislamu na Wakristo mkoani hapa, wacharuka na kumuonya Rais Kikwete kwamba asikubali kulisaliti taifa kwa kupokea misaada yenye matakwa ya kudhalilisha utu wa Watanzania kwa ushoga.
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Iringa Dk. Owdenburg Mdegela, alisema kauli ya Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, ni ya udhalilishaji na imelishushia heshima taifa la Uingereza.
Akizungumza katika swala ya Idd El Haji, Sheikh wa mkoa wa Iringa, Juma Ally Tagalile, alimtaka Rais Kikwete kuulinda utu wa Watanzania kwa kuukataa ushoga.
Sheikh Tagalile alisema kuwa pamoja na misaada mbalimbali ambayo Uingereza imekuwa ikitoa kwa Tanzania, ni wakati muafaka wa Serikali kuikataa misaada yenye masharti ya kuvunja utu wa Mtanzania.
Aliwataka waumini wa dini zote kuungana kuliombea taifa ili lisiingizwe katika laana ya ushoga.
Wakati huohuo, Kaimu Mufti wa Tanzania, Sheikh Ally Mkoyogole, amewataka viongozi wa Serikali kutenda haki kwa kusoma alama na kujua nini wananchi wanahitaji ili kuliepusha taifa na machafuko yanayoweza kutokea kutokana na kushamiri kwa vitendo vya ufisadi.
Akizungumza katika Baraza la Idd El Hajj lililofanyika kwenye Msikiti wa Al Faruok, Makao Makuu ya Baraza Kuu la Waislamu (Bakwata) lililohudhuriwa pia na Makamu wa Rais Dk. Mohamed Gharib Bilal, Sheikh Mkoyogole, alisema kamwe amani iliyopo haiwezi kudumu kama hakuna haki na uadilifu kwa watu waliopewa dhamna ya kuongoza nchi.
“Ibada hii ya Hijja inatufunza mambo mengi lakini kubwa ni kwa viongozi kutambua kuwa kama hakuna uadilifu hakuna amani na mfano mzuri ni katika baadhi ya nchi ambazo machafuko yametokea ambapo viongozi wake wanashindwa kuelewa nini wananchi wanahitaji.
“…Ili nasi tuweze kudumisha utulivu huu ni lazima haki na uadilifu vizingatiwe, hasa kwa viongozi mliopewa dhamana ya kuiongoza Serikali mna wajibu wa kutenda haki bila kubagua, vinginevyo tutaweza kuishuhudia nchini yetu ikiingia katika machafuko na kupoteza amani yetu,” alisema Sheikh Mkoyogole.
Kwa upande wake, mgeni rasmi katika Baraza hilo la Idd El Hajj, Makamu wa Rais Dk. Bilal, alisema ni vema kwa mahujaji kutambua malengo ya Hijjah zao na kutokuwa na mawazo ya kwenda kutalii tu.
“Wakati taifa letu likiwa katika kuadhimisha kilele cha miaka 50 ya Uhuru ni vema Waislamu mliombee dua ili liepukane na machafuko yanayoweza kuzuilika kwa kuhubiri amani na mshikamano kwa Watanzania,” alisema Dk. Bilal.