Upo uhusiano mkubwa kati ya matumizi ya vidhibiti mimba na utoaji mimba. Mtumiaji wa vidhibiti mimba akipata mimba ataiondoa kwani lengo lake halikuwa kupata mimba. Matumizi ya vidhibiti mimba huwagawa watoto katika wale wanaotakiwa na wasiotakiwa. Mwanamke anayetumia vidhibiti mimba hujenga dhana ya kutomtaka mtoto kwa wakati ule na yule anayetakikana ni yule anayepatikana baada ya kuacha kutumia vidhibti mimba na majozi walipenda kwa wakati ule kupata mtoto mwingine. Yule asiyetakikana kwa wakati ule huuawa kwa kutoa mimba. Kwa hivyo matumizi ya vidhibiti mimba husababisha dhambi ya uuaji, hupingana na matashi ya Mungu ya kumpatia binadamu uzima tele. [Kut. 20:13; Yoh. 10:10]
Vita dhidi ya umama
Mtumiaji wa vidhibiti mimba huwatendea watoto kama balaa ambalo linapaswa kuepukwa kwa namna yoyote ile na uzazi wake kama laana ambalo angetamani kutopewa na Mungu. Vidhibiti mimba havithamini uzazi ambao ndio chanzo cha uhai mpya – mtoto. Mtumiaji anajitahidi sana kuepuka mtoto kwa kuuharibu uzazi wake. Hali hiyo inapingana na amri ya Mungu aliyoitoa katika Biblia Takatifu – ‘zaeni mkaongezeke mkaijaze nchi’ [Mwa. 1:28]
Vita dhidi ya ubaba
Matumizi ya vidhibiti mimba huondoa mshikamano wa upendo wa kindoa kwa wanandoa. Mwanamke katika tendo la ndoa hajitoi kwa dhati kwa mumewe kwa sababu anakuwa ameuharibu uzazi wake na anamtendea mume wake kama adui. Mume anaonekana kutoa sumu ambayo itamdhuru mke wake [uzazi wa mume ni sumu, na mtoto atokanaye na mwunganiko wa mbegu, yai na roho ya Mungu ni balaa]. Kwa hiyo watumiaji wa vidhibiti mimba hutangaza uadui dhidi ya ubaba.
Uasi dhidi ya zawadi ya uzazi
Mtumiaji wa vidhibiti mimba hujiona mgonjwa daima. Kwa hiyo lazima atumie vidhibiti mimba, [ambavyo kwa sasa anaviona kuwa dawa], kila siku ili kutibu ugonjwa, yaani uzazi wake, na matokeo yake ni uasi dhidi ya zawadi azizi ya uzazi ambao Mungu ameutoa bure kwa wanadamu kwa lengo la kupasisha kizazi.
Vita dhidi ya afya
Pengine jambo moja ambalo watengenezaji, wahamasishaji na wauzaji wa vidhibiti mimba wamefaulu ni kuwafanya watumiaji waamini kuwa kutopata mimba ni jambo la kiafya zaidi kuliko kudhohofisha afya zao wakati wanatumia. Magonjwa yatokanayo na matumizi ya vidhibiti mimba ni mengi na baadhi yake ni makubwa sana. Baadhi ya magonjwa hayatibiki na mengine husababisha kifo. Lakini watumiaji wanaendelea kuvitumia, licha ya madhara [magonjwa] wanayoyapata. Nao wahamasishaji na wauzaji wanawalaghai watumiaji kuwa magonjwa hayo ni ya muda mfupi na yatapita. Na pengine wanaelezwa kuwa madhara hayo ni hali ya kwaida, na siyo ugonjwa.
Ni ubatili mtupu
Kufanya tendo la ndoa na mwanamke ambaye ni mgonjwa kiafya na mwili wake umejaa sumu za dawa ni kitendo haramu na batili. Tendo la ndoa linapaswa kutokana na maridhiano ya kweli ya wanandoa, kila mmoja akiwa na akili timamu na akiwa na afya njema na hivyo tendo lenyewe lina nguvu ya kudumisha furaha, amani, mshikamano na upendo wa kweli. Kama mmoja ni mgonjwa na mwenzake akamlazimisha, au hata mwanamke akakubali kwa hiari yake ili hali akijua kuwa yu mgonjwa, tendo la ndoa litendekalo katika hali hiyo ni batili.
Tangazo la uasherati
Vidhibiti mimba huwajengea wanawake ujasiri wa kufanya uzinzi na uasherati bila mipaka [na hivyo kutimiza lengo la mwasisi wake, Margaret Sanger aliyesema wanawake wafurahie ngono upeo bila hofu ya mimba]. Watetezi wa vidhibiti mimba wanawarubuni wanawake kupitia matangazo na vipeperushi vyao eti, wanaotumia vidhibiti mimba ni wanawake wenye heshima na wenye ndoa. Kama hilo lingekuwa kweli, kwa nini basi wanafunzi katika ngazi zote za elimu wanahamasishwa kutumia vidhibiti mimba? Waanzilishi wa vidhibiti mimba, Margaret Sanger na Marie Stopes walieleza wazi kuwa matumizi ya vidhibiti mimba vinawaweka wanawake kuwa huru kutoka vifungo vya ndoa, mimba na magonjwa ya zinaa kwa baadhi ya vidhibiti mimba.
Waraka wa kinabii
Mtu aliyelipatia tatizo hilo ufumbuzi wa kweli ni Papa Paul VI katika waraka wa ‘‘Humanae Vitae’’ - ‘Kwa ajili ya Uhai’ alipotabiri kuwa kwa vile vidhibiti mimba hutenganisha sifa ya mshikamano wa upendo na uzazi katika tendo la ndoa, basi vitaharibu tabia ya ubaba ya wanaume na kuwadunisha wanawake hadi kuwa vyombo vya starehe.
Papa Paul IV alisema vidhibiti mimba vitasababisha mmomonyoko wa maadili katika jamii na kudhoofisha ndoa. Papa aliona waziwazi hali hiyo, aliangalia katika maslahi ya jamii, jamii yenye maadili, dhamiri safi na hadhi ya wanawake. Matokeo ya vidhibiti mimba ni kuwafanya wanawake wapatikane kwa urahisi kwa vitendo vya ngono.
Kwa vile wanawake wamefanywa sasa kuwa vitu vya kuchezewa na kutupwa sio ajabu tena kuona hata watoto ambao wangali matumboni wanatendewa kama vitu vinavyoweza kutupwa. Kama uja-uzito ni ugonjwa, kama ambavyo mtazamo wa vidhibiti mimba unatuonyesha na vidhibiti mimba ni dawa itolewayo na tabibu basi, utoaji mimba ni dawa itolewayo pindi vidonge vinaposhindwa. Kwa hiyo mauaji kwa njia ya utoaji mimba yana mizizi yake katika kuhalalisha na kukubalika kwa vidhibiti mimba.
Tendo la ndoa linalolazimishwa kwa mwenzi bila kujali hali yake ya kiafya na utayari wake katika tendo hilo haliwezi kuwa tunda la upendo wa kweli. Hilo ni tendo la kubaka lenye kukiuka misingi ya maadili yahusuyo tendo lenyewe. Hali hiyo ikizoeleka, basi inasababisha kudai talaka na kuvunjika kwa ndoa.
NI DHAMBI KUTUMIA VIDHIBITI MIMBA
Utangulizi
Kutumia vidhibiti mimba kama njia ya kupanga uzazi ni kuamua juu ya mpishano wa miaka ya kuzaliwa watoto na juu ya idadi ya watoto ambao familia inapenda kuwazaa. Njia zitumikazo ni chachu bandia [za estrojeni na projestini] zinazowekwa katika vidonge vya majira, vipandikizi, sindano ya depo provera, lunelle, vidonge vya tahadhari [kama vile emergency contraceptives; RU486]; ili zifanye kazi dhidi ya chachu asilia zitolewazo na mwanamke katika kipindi cha uzazi; vitanzi; kondom na kutoa mimba.
Vidhibiti mimba vitumiavyo chachu hufanya mayai yasikomae; huharibu mirija ya uzazi na hivyo kupunguza mwengo wa kusafirisha mbegu na mimba; huharibu ngozi nyororo ya tumbo la uzazi kwa namna kwamba mimba iliyokwishatungwa hushindwa kujipandikiza na hivyo hufa; hufanya ute wa uzazi kuwa mzito na hivyo kuzuia mbegu za kiume kupita kuelekea tumbo la uzazi. Vitanzi hukaa katika tumbo la uzazi kama kitu kigeni ambacho kazi yake ni kumzuia mtoto kujipandikiza na hivyo humwua katika umri wake mdogo. Kondomu huweka uzio katika tendo la ndoa na hivyo kuzuia uwezekano wa mbegu kukutana na kijiyai. Wanawake wakereketwa wa falsafa za umame hupigania vitendo vya utoaji mimba kama njia moja wapo ya kupanga uzazi na wanasema jambo hilo lionekane kama haki ya mwanamke – ni uhuru wake.
Pro-Life [HLI] Tanzania, japokuwa ni shirika lisilo la kiserikali linafanya kazi yake katika misingi ya mafundisho ya Kanisa Katoliki. Kutokana na mafundisho hayo, tunaweka bayana kwa ni dhambi kutumia vidhibiti mimba kama njia ya uzazi wa mpango. Tunafundisha hivyo kutokana na kweli za kiimani zilizomo katika Biblia Takatifu, mapokeo ya mababa wa kanisa na hati au nyaraka mbalimbali za kichungaji, kama vile hati za Mtaguso Mkuu wa II wa Vatikano, hati “Juu ya Uhai wa Binadamu” (Human Vitae), na “Injili ya Uhai” [Evangelium Vitae]. Kweli hizi za kiimani zinatufundisha kuwa binadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu (Mwa.1:26). Uwepo wa binadamu mpya hutegemea kuwepo kwa muunganiko halisi wa mbegu ya baba, yai la mama na roho ya Mungu. Baada ya mwunganiko huo, uhai unakuwa kitu kitakatifu. Ndiyo maana tunaamriwa na Mungu tusiue (Kut.20:13). Amri hii haihusu tu uhai wa watu waliokwisha zaliwa bali inahusu pia, tena zaidi, watoto wasiozaliwa bado kwani hawa hawawezi kujitetea.
Kila binadamu ni wa pekee na kila mmoja ameumbwa kwa ajili maalumu. Tangu tukingali katika matumbo ya mama zetu, Mungu amepanga na kutuwekea majukumu tutakayofanya katika uhai wetu wa hapa duniani (Isa. 49:1-3, 5).
Dhambi itokanayo na matumizi ya vidhibiti mimba ni ipi?
Dhambi ya kuua: Chachu bandia za estrojeni na projestini zilizomo kwenye vidonge vya majira, vipandikizi, sindano ya depo provera, vidonge vya tahadhari, RU 486, na nyingine, zinaua uhai mpya kabla mwanamke hajajua kama ana mimba. Kwa kadiri ya Dk. Bogomir Kuhar, vita dhidi ya uhai wa watoto kupitia vidhibiti mimba husababisha vifo vya watoto kati ya millioni 8.1 na 12.75 kila mwaka katika mataifa ya Ulaya na Marekani. Hapa kwetu Tanzania idadi ya watoto wachanga wanaouawa na vidhibiti mimba haijajulikana bado, lakini tukichukua kuwa katika kila wanawake 10, wanawake 7 hutumia vidhibiti mimba, basi idadi yao inaweza kuwa kati ya milioni 2 na 3 kila mwaka. Kuuawa kwa watoto hao kunasababishwa na kuharibika ngozi nyororo ya tumbo la uzazi na hivyo kushindwa kumpokea binadamu huyo mpya na halafu kutoka nje baadaye pamoja na damu ya mwezi.
Dhambi ya kuua: Kutoa mimba kunakotokana na uja uzito unaopatikana wakati vidhibiti mimba vinatumika. Kila njia ina kiwango fulani cha kushindwa kuzuia mwunganiko wa kijiyai na mbegu. Kwa vile lengo la tendo la ndoa halikuwa kupata mtoto, na mtoto amepatikana kwa bahati mbaya, mtoto huyo atauawa, na tumezoa kuita njia ya kuua watoto wa aina hiyo, kutoa mimba. Kwa hiyo njia hizo ni chanzo kikubwa cha utoaji mimba. Mwanamke anayetumia njia hizo, akipata uja–uzito licha ya matumizi yake, ataita mimba (mtoto) hiyo isiyotakikana (unwanted). Na kitu kisichotakikana huondolewa; kwa hiyo mwanamke anayetumia njia za hizo huwa anaua hata kama ni kwa kutojua. Na adhabu ya kosa la kuua kwa kadiri ya Katekisimu ya Kanisa Katoliki ni kutengwa na Kanisa moja kwa moja (Iba, 2272). Utoaji mimba na uuaji wa watoto ni maovu ya kuchikiza mno (GS. 51 aya 3 na Katekisimu Iba. 2271).
Dhambi nyingine kubwa ya matumizi ya vidhibiti mimba ni kuwa vinatenganisha shabaha mbili za tendo la ndoa, yaani la kupasisha uhai wa binadamu mpya na kujenga umoja wa upendo wa kindoa. Kufunga ndoa kwa lengo la kukataa uzao ni kupinga amri ya Mungu aliyoiweka tangu kuumbwa binadamu “Zaeni mkaongezeke, mkaijaze chi” (Mwa. 1:28). Kuwakataa watoto kwa makusudi kuna matokeo mabaya katika jamii, ndiko kuzuka kwa fikra za kumkana Mungu na kupuuzia malezi ya watoto. Pia kuwakataa watoto huzaa vitendo vya ubinafsi na tama mbaya. Ndipo hapo huzuka nadharia na umame, ushoga na umama bandia. Wanawake wanakosa tunu azizi ya upendo na huruma kwa watoto wachanga.
Matumizi ya vidhibiti mimba huondoa mshikamano wa kindoa. Mwanamke anamwambia mume wake, “nakupenda lakini uzazi wangu sitakupa… nauharibu”. Mume naye anamwambia mke wake, “nakupenda lakini uzazi wangu sitakupa … nauweka ndani ya mpira”. Dhambi hapa ni kwamba watu wa ndoa hawawezi kujitoa kila mmoja kwa mwenzake Wanandoa hao wanakuwa wamejenga uhusiano wa katao. Kwa dhati yake matumizi ya vidhibiti mimba hujenga chuki kati ya mume na mke – hakuna anayempenda mwenzake. Katika hali hiyo upendo wa kweli huvuurugika na misigano huanza katika ndoa. Misigano inapoendelea matatizo mengine huanza kuwa makubwa na kisha kuishia kwenye talaka. Kwa hiyo matumizi ya vidhibiti mimba kwa kiasi kikubwa husababisha au kuvurugika au kuvunjika kwa ndoa.
Dhambi nyingine ya vidhibiti mimba ni kule kuharibu uzazi ambao unatendewa kama ugonjwa. Wanawake wanaotumia vidhibiti mimba hujengeka kifikra kuwa wao ni wagonjwa wanaohitaji tiba. Natumia dawa … natibu…? Kukataa watoto? Kutibu uzazi wako? [Je uzazi wako unaumwa?]. Ndiyo maana katika jitihada za kutibu ugonjwa ambao kwa kweli haupo, wanawake wanajiletea magonjwa juu ya miili yao, juu ya akili zao na zaidi sana juu ya roho zao. Wanawake wanajipatia adhabu kwa sababu ya kuzingatia falsafa na programu za watetezi wa kifo. Je mwanamke anayeharibu uzazi wake au afya yake hatendi dhambi? Mbona mtu anayejiua tunasema anatenda dhambi isiyosameheka? Ni dhambi dhidi ya Roho Mtakatifu [KKK Iba 2297]. Madhara / magonjwa wayapatayo wanawake kutokana na vidhibiti mimba ni mengi, baadhi yake ni magonjwa ya moyo, mvujo wa damu ndani ya mishipa ya ubongo, shinikizo la damu, kupofuka macho, na maumivu makali ya kichwa, kutoka damu ukeni, sarakani ya matiti, saratani ya mlango wa tumbo la uzazi, saratani ya kokwa, magonjwaya maini, mimba nje ya mji wa mimba, kupata utasa wa muda au kudumu, kupata hedhi bila mpangilio, kutoka damu nyingi kwa muda mrefu, kunenepa, kukonda, kichefuchefu, kunyonyoka nywele, n.k.
Dhambi nyingine ya vidhibiti mimba ni pale watumiaji wa vidhibiti mimba wanapomtendea mwenzi kama vile angekuwa adui wa kuepukwa na hivyo kujenga uhusiano wa kiuhasama katika ndoa. Mke anamtendea mume wake kama adui. Kwa hiyo, tendo la ndoa liwadiapo mke anakosa amani; na hiyo lazima amweke pembeni mume wake kwa kutumia vidhibiti mimba. Magonjwa anayoyapata kutokana na kutumia vidhibiti mimba yanazidi kumweka mbali zaidi na mume wake, kwani wakati huu hata tendo la ndoa ama halifanyiki ama linafanyika kwa taabu sana. Hali hiyo humjengea mwanamke huzuni tupu. Mume naye, kwa kudhani anampenda mke wake, anatumia vidhibiti mimba, asifahamu kuwa, huo sio upendo bali ni utengano. Katika hali ya utengano, akili ya mwanaume humwona mke wake kama chombo tu cha starehe yake. Anapomwitaji mke wake anapatikana, bila kipinganizi chochote kile. Lakini anapoumwa kutokana na kutumia vidhibiti mimba, mwanaume huyu humtelekeza mkewe na kutafuta wanawake wenye afya. Je katika hali hiyo, vidhibiti mimba vinaleta upendo au utengano?
Dhambi nyingine ya vidhibiti mimba ni kule kuwaona watoto kama ugonjwa. Wazazi wanajitahidi kuwazuia watoto kuzaliwa, kwani kwa kuzaliwa watakuwa mwiba katika maisha yao –hali ngumu ya maisha, ada za shule, mavazi, chakula … nk. Uja-uzito katika jamii ya leo huonekana ni jambo la huzuni badala ya kuliona kuwa jambo la furaha. Uja-uzito baada ya ya mtoto mmoja au wawili hutendewa kama vile lingekuwa kosa la jinai, ambalo kila mmoja anachukua tahadhari kulikwepa baadaye. Biblia Tatifu inatufundisha kuwa watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu. Uwepo wa watoto wengi ni ishara ya upendeleo wa pekee wa Mungu [Zab.127:3-5; 128:3,6]. Je sisi binadamu tuna haki gani ya kuwakataa? Badala ya mtazamo wa dunia ya sasa kwa kuwaona watoto kama bughudha inayotuzuia kustarehe, utajiri hauwezi kuwa na maana bila watoto ambao watarithishwa. Utamaduni wa uzao wa mtoto mmoja au wawili ni wa uchoyo, ubinafsi; ndani yake zimepandwa mbegu za chuki.
Mwanamke anapotumia vidhibiti mimba yeye na mume wake wanaikwaa dhambi nyingine, ndiyo ile ya kuukataa uzazi, yaani ule uwezo wa mwanamke kuwa mja-mzito, kumpokea na kumtunza mtoto ndani ya tumbo lake na kumlea. Uwezo pekee unaopasisha uhai mpya, kuunda familia na jumuiya ya kitaifa unakataliwa na kuonekana ni mzigo. Kwa hiyo mtazamo wa kukumbatia matumizi ya vidhibiti mimba una matokeo yake katika kuporomoka kwa vizazi duniani na hivyo kupungua idadi ya watu. Idadi ya watu ikipungua uwezo wa taifa kufikiri katika masuala ya ugunduzi na nguvu kazi ya taifa hupotea. Ndiyo maana leo hii tunahangaishwa magonjwa na matukio mbalimbali yanayopita uwezo wetu kwa sababu wale binadamu waliopewa majukumu ya kuyakabili magonjwa na matukio hayo ama wamezuiwa kuzaliwa au wameuawa wakingali matumboni mwa mama zao. Dunia ya leo inavuna ilichopanda. Watu wa mataifa walipanda chuki, tukavuna kifo.
Dhambi nyingine ya vidhibiti mimba ni kueneza uasherati na uzinzi katika jamii. Vidhibiti mimba huwafanya watumiaji washindwe kuwa waaminifu katika maisha yao. Hali hii inahusu wanawake walioolewa na wale ambao bado hawajaolewa. Mwanamke akijua kuwa anaweza kufanya zinaa bila kuwa na hofu ya kupata uja-uzito anaanza kujiona huru na kuvunja heshima iliyolinda utakatifu wa tendo la ndoa kwa miaka mingi. Vijana wa kike na kiume wanahimizwa kutumia vidhibiti mimba hivi kwa lengo la kukwepa mimba ambazo zingekatisha masomo yao, au zingeleta aibu kwa familia. Matokeo ya kushindwa kuwa waaminifu katika ndoa na katika maisha ni kuongezeka kwa magonjwa ya zinaa pamoja na UKIMWI. Waasisi na watetezi wa vidhiti mimba, Margaret Sanger na Marie Stopes, walisema bayana kuwa lengo la vidhibiti mimba ni kuwaweka wanawake huru kutoka vifungo vya ndoa na hivyo kufurahia ngono bila mipaka.
Hitimisho: Vidhibiti mimba huwakilisha kifo, na mdhamini wake ni yule Mwovu, Shetani, Ibilisi ambaye ni mwongo na mwuaji tangu kale (Yoh: 8:44). Kazi ya huyu Mwovu ni kuufanya ulimwengu kuwa mahali rahisi pa kustarehe bila jasho. Ndani ya starehe hizo vimo visima vya upotofu na kifo. Ibilisi anapingana na maadili bora katika jamii, anapingana na utakatifu wa ndoa, anapingana na mahusiano mazuri katika familia na jamii. Je wewe unamfuta Mungu au Yule Mwovu, Ibili/Shetani aliye mwongo na mwuaji tangu kale?