When used “correctly”, condoms have a 10% failure rate, and their distribution encourages a false sense of security about the inherently risky nature of promiscuity. They also bring a host of physchologically damaging effects, increasing the allure of adultery and extra-marital sex and creating the incentive for more abortions when such methods inevitably fail, as well as elevating the level of out of wedlock births and the rate of divorce, particularly devastating consequences for continent already mired in poverty.
Maana
Kondomu ni kifaa/zana iliyotengenezwa mahususi kuvalisha uume au kuwekwa ukeni wakati wa kujamiiana. Kwa kawaida kifaa/zana hiyo hubana kufuatana na umbile la uume au uke.
Historia
Matumizi ya kondomu yamefahamika tangu miaka mingi iliyopita, japokuwa hatuna hakika kama ilitumika kuzuia magonjwa ya zinaa, kupanga uzazi au kama ilihusishwa na matumizi ya juju, [yaani kichawi] au mapambo.
Awamu I: Mwanasayansi, raia wa Italia, Gabrielo Fallopio (1523-1562) aliandika katika kitabu chake “De Morbo Gallico”, [juu ya ugonjwa wa Kifaransa yaani, kaswende] akipendekeza matumizi ya kondomu kama kinga dhidi ya maambukizo ya vimelea vya ugonjwa huo. Baadaye Hercules Saxona aligundua kondomu iliyotengenezwa kutokana na mimea na iliyokuwa na uwezo wa kufunika uume wote.
Awamu II: Daktari Condom, wengine walimwita Cundum au wengine Quondam anafamihamika kwa ugunduzi wa kondomu zilizotengenezwa kutokana na utumbo wa kondoo. Inaelezwa kuwa Dk. Condom alikuwa daktari wa Mfalme Charles II wa Uingereza. Yasemekana kutokana na Mfalme Charles II kuwa na wanawake wengi nje ya ndoa yake, Dr. Condom alimshauri kutumia kondomu ili kujikinga na magonjwa ya zinaa. Wakati huo huo kondomu zilifahamika kutumika pia kama kidhibiti mimba. Kwa hiyo neno “kondomu” limetokana na jina la daktari huyu wa Mfalme Charles II wa Uingereza.
Awamu III: Kondomu zilizotengenezwa kutokana na mpira ziligunduliwa. Hizi zilitengenezwa kwa urahisi na kwa wingi na zikawa ndizo pekee zenye uwezo wa kudhibiti mimba hadi miaka ya 1960 vilipogunduliwa vidonge vya majira.
Leo hii zipo aina tatu za kondomu katika soko;
Aina ya kwanza ni zile zilizotengenezwa kwa utumbo wa kondoo ambazo zinasemekana kuwa hazina uwezo mkubwa zikitumika kama kidhibiti mimba, wala hazina uwezo wowote wa kuzuia maambukizo ya magonjwa ya zinaa na virusi vya ukimwi.
Aina ya pili ni zile zilizotengenezwa kutokana na mpira wa latex. Watengenezaji, wahamasishaji na wasambazaji wanazisifia kuwa na ubora mkubwa zinapotumika, ama kama kidhibiti mimba au kwa lengo la kudhibiti kuenea kwa maambukizo ya magonjwa ya zinaa vikiwemo virusi vya ukimwi.
Aina ya tatu ni kondomu zilizotengenezwa kutokana na mchanganyiko wa mpira na vitu vingine (synthetic) ziitwazo “polyurethane”. Hizi zinasemekana kuwa hazina uwezo mkubwa kama zile za latex. Pamoja na hayo, inafahamika kuwa kondomu hazina uwezo kabisa wa kuzuia kuenea kwa baadhi ya magonjwa ya zinaa. Soko la kondomu limepata umaarufu zaidi kuanzia miaka ya 1980 kufuatia kuzuka na kuenea kwa janga la ukimwi.
Je kondomu ni salama?
Tunaelezwa kuwa kondomu hutengenezwa kwa ustadi mkubwa kiasi kwamba haziwezi kuruhusu kitu chochote kupita. Lakini tafiti mbalimbali zilizofanyika zinaonyesha kuwa kondomu zaweza kuvuja kutokana na mazingira halisi ya utengenezaji wa latex. Wengine wanadai kuwa ili kuzifanya imara kondomu zimetengenezwa kwa kupishanisha pande mbili ili kuziba udhaifu wa kila upande. Hata hivyo watengenezaji walisahau kuwa mazingira ya matumizi ya kondomu katika ngono hayalingani na majaribio waliyofanya ya kujaza maji au kujaza hewa ili kupima kama maji na hewa vinapita. Katika tendo la ngono ipo misuguano ya yamna mbalimbali inayosababisha kubadilisha mazingira ya kondomu na kuidhohofisha.
Kutokana na tafiti hizo imefahamika kuwa kondomu hazina uwezo wa kuzuia mbegu za kiume kupenya wakati wote. Upana wa kipenyo cha mbegu ni maikroni 5 wakati upana wa kipenyo cha kirusi cha ukimwi ni maikroni 0.1. Kwa maneno mengine mbegu ya kiume ni kubwa mara 50 ya kirusi cha ukimwi. Vile vile tafiti zimeonyesha kuwa kondomu haina uwezo wa kuzuia maambukizo ya magonjwa ya zinaa vikiwemo virusi vya ukimwi kwa kiwango cha asilimia mia moja. Tunaweza kusema, kutokana na majibu ya tafiti hizo kwamba kondomu sio salama kwa asilimia mia moja. Kondomu zina kiwango cha kushindwa cha kati ya asilimia 10 na 15 na wengine wanasema hata asilimia 20. Wasambazaji na wahamasishaji wa matumizi ya kondomu hawapendi kusikia ukweli huo na wanafanya jitihada kubwa ya kuficha ukweli huo. Matangazo yatolewayo kupitia mabango ya barabarani, katika televisheni, radio na hata magazeti yanawarubuni watu yakiwaaminisha kuwa kondomu humkinga mtumiaji kwa kiwango cha asilimia 100%. Huko ni kukengeusha ukweli na kukiuka maadili ya kitaaluma. Wengi, kama sio wote wateteao matumizi ya kondomu hufanya hivyo kwa sababu ya maslahi ya kifedha na kibiashara. Tukiongozwa na dhamiri safi, lazima tukiri ukweli uliopo na tuwaeleze watumiaji, ili tusije kuwa sababu ya kifo chao. Kila kondomu inaposhindwa [itumikapo kama kinga dhidi ya maambukizo ya virusi vya ukimwi] humaanisha kifo.
Udhaifu wa kondomu
Udhaifu wa kondomu unatokana na sababu tatu: udhaifu utokanao na sababu za kiufundi [utengenezaji]; udhaifu utokanao na matumizi; na udhaifu utokanao na mazingira.
Udhaifu wa kiufundi
Wasambazaji wanatueleza kuwa kondomu zililotoka kiwandani zikiwa na ubora unaotakiwa zikitumiwa wakati wote na kwa usahihi zina uwezo wa kukinga kwa kiwango hadi cha asilimia 97. Zisipotumika vizuri zina kiwango cha kushindwa cha asilimia 14. Kiwango cha kushindwa kwa kondomu kuzuia maambukizo ya magonjwa ya zinaa hutofautiana kutokana na aina ya magonjwa ya zinaa. Kondomu zaweza kuzuia kwa kiwango fulani maambukizo ya magonjwa ya zinaa yanayosafiri kwa njia ya ute, lakini haziwezi kuzuia magonjwa ya zinaa yanayoambukizwa kwa mgusano wa mwili kama vile “herpes” na “human papillomavirus”; au magonjwa yanayoambukizwa kutokana na vidonda au malengelenge yaliyoko kwenye via vya uzazi kama vile kaswende. Hali hiyo inatokana na:
Watengenezaji wameruhusu udhaifu wa kiufundi kama zao la kiwandani lililotengenezwa na kazi ya mikono ya binadamu [acceptable quality limit] kwa viwango fulani kwa nchi mbalimbali. Marekani kiwango kilichoruhusiwa ni asilimia 99.6 kwa kutoruhusu kondomu kuvuja; huko Uingereza kiwango chake ni asilimia 97; na huko Uholanzi kiwango chake ni asilimia 96.5. Hii ni kusema kuwa katika kila idadi ya kondomu itumikayo kwa wakati mmoja kuna kiwango cha kuvuja kati ya asilimia 0.4 (USA); asilimia 3 (Britain) na asilimia 3.5 (Holland).
Kondomu huzeeka. Kwa kadiri kondomu zisivyotumika kwa muda mrefu ndivyo hivyo zinaendelea kuzeeka. Kwa hiyo mtumiaji kondomu wa miaka 3 au 4 baada ya kondomu hiyo kutengenezwa yumo katika hatari zaidi ya kuambukizwa kuliko anayetumia kondomu mara tu baada ya kutoka kiwandani. Utafiti mmoja umeonyesha kuwa kiwango cha kupasuka kwa kondomu kiliongezeka kutoka asili mia 3.6 kwa kondomu mpya hadi asilimia 18.6 kwa kondomu zilizotumika miaka kadhaa baadaye.
Kondomu hupasuka. Kiwango cha kupasuka kwa kondomu hutegemea aina ya kilainisho kilichotumika na aina ya kondomu. Majibu ya tafiti 15 zilizokusanywa na “Contraceptive Technology” yalionyesha kuwa katika kondomu 25,184 zilizotumika asilimia 4.64 zilipasuka.
Ingawaje kondomu za latex zinasemekana kuwa na kiwango kidogo sana cha kupitisha virusi vya ukimwi, hatari kubwa ya matumizi yake imo katika uwezekano wa kondomu kupasuka, kuchanika na kuteleza. Kwa hiyo hata kama ni virusi vichache tu vinaweza kupenya, kiwango cha maambukizo kitakuwa kikubwa kadiri kondomu zinavyosambazwa kwa wingi na kadiri watu wanavyojihusisha na vitendo vya ngono wakiamini katika matumizi ya kondomu.
Udhaifu katika matumizi
Matumizi mabaya: ikimaanisha kutovaa vizuri, kugeuza nje ndani, aina ya misuguano na aina ya ngono; urefu wa muda wa ngono. Vilevile matumizi mabaya yanatokana na uelewa mdogo hasa kwa watu wasiojua kusoma na kuandika na wale wakaao mbali na miji.
Kuteleza na kuvulika kutokanako na hali ya uume kuwa mdindifu au la; upana au wembamba; mrefu au mfupi. Vile vile kuvulika kunatokana na hali ya tendo la ngono na hali ya mtumiaji na mazingira ya matumizi. Kuvulika kunatokana pia na umri wa mtumiaji, kama ni mtoto, kijana kama mtu mzima au mzee.
Kutumia kondomu ambazo muda wake umepita. Siyo rahisi kwa watu watumiao kondomu gizani, katika hali ya ulevi, kutokujua kusoma, kuchunguza na kugundua kama muda umepita. Mazingira ya kingono yakishawekwa, watu wanatawaliwa na mihemuko ya juu ya ngono kiasi kwamba hawawezi kuchunguza tarehe ya ukomo wa matumizi ya kondomu. Japokuwa watengenezaji na wasambazaji wanaelekeza kutotumia kondomu iliyobadilika rangi au iliyokauka, tabia za watumiaji hazina nafasi ya kuzingatia ushauri huo.
Lengo la mtumiaji laweza kusababisha matumizi kuwa mabaya. Mtu mwenye virusi vya ukimwi, anajiwekea lengo kwamba hataki kufa pekee yake, atafanya jitihada za kutotumia vizuri ili mwenzake [ambaye anaamini hajaambukizwa] aweze kuambukizwa ili, “nisife peke yangu”. Vile vile katika siku hizi za dawa za kupunguza makali ya kuzaliana virusi vya ukimwi, mtu anaweza kuonekana mwenye afya nzuri kabisa, na anaweza kumshawishi mwenzake kuachana na kondomu kwa vile “wanaaminiana”. Kwa hiyo maambukizo yanaweza kuwa makubwa kutokana na kutowadhibiti wale waliokwisha ambukizwa.
Udhaifu wa kimazingira
Udhaifu huu unahusu kwa upande mmoja hali za kibinadamu na kwa upande mwingine hali ya maumbile. Hali za kibinadamu ni pamoja na usafirishaji na hifadhi. Hali ya kimaumbile ni pamoja na hali ya hewa na jiografia ya mahali.
Hali za kibinadamu:
Udhaifu wa kondomu waweza kusababishwa na usafirishaji, yaani muda unaotumika kusafiri kutoka sehemu zinapotengenezwa hadi mahali zinapotumika; vile vile vyombo vya usafirishaji na usalama wa vyombo hivyo. Kondomu zinazosafirishwa katika meli, zikiwa baharini kwa miezi kadhaa kabla hazijafika katika nchi lengwa na katika hali ya joto ndani ya makontena zinakuwa na kiwango hafifu katika ubora wake.
Udhaifu wa sehemu ya kuhifadhi kondomu pamoja na vyombo vya kuhifadhia kondomu ni mkubwa sana. Baadhi ya kondomu huhifadhiwa katika sehemu zisizofaa kama vile katika mikebe, mapochi, mifuko, makabati au katika majokofu. Kondomu zinadhohofishwa ubora wake kwa kiasi kikubwa kama zinahifadhiwa sehemu hizo.
Hali za kimaumbile:
Hali ya joto kali au baridi kali huharibu ubora wa kondomu na hivyo kuzifanya zisifae kwa matumizi. Hali ya joto ya nyuzi joto 25 ‘centigrade’. ndiyo inayotakiwa kwa matumizi mazuri ya kondomu. Hali ya joto inayozidi hapo au iliyo chini ya hapo huharibu kondomu.
Hali ya unyevunyevu, kama vile mazingira ya mvua huharibu pia ubora wa kondomu.
Hali ya vumbi vumbi nayo pia huchangia kuharibu kondomu. Kondomu zinazowekwa katika maduka ya vyakula au ya dawa zinaweza kuharibiwa na vumbivumbi kama usafi hauzingatiwi
Mionzi mikali ya jua huharibu sana kondomu na kuzifanya zisifae kwa matumizi yake.
Kiwango cha kushindwa
Kiwango cha kushindwa kinategemea yote tuliyosema hapo juu. Tafiti mbalimbali zinatuthibitishia kuwa kiwango cha kushindwa zikitumika kama kidhibiti mimba na kuambukizwa kwa magonjwa ya zinaa pamoja na virusi vya ukimwi ni kati ya 10 hadi 15 au 20. Wengine wanasema katika kila kondomu kumi na mbili zinazotumika kujikinga na kuambukizwa virusi vya ukimwi, moja hufeli. Yaani katika kila watumiaji 12 wa kondomu mmoja huathirika.
Hata hivyo ieleweke kuwa takwimu za kushindwa au kufaulu kwa kondomu katika kudhibiti magonjwa ya zinaa pamoja na virusi vya ukimwi zinatokana na kuwafanyia utafiti wapenzi ambapo mmoja alikuwa na virusi [au ukimwi] na mwingine hakuwa nao. Bila kufanya majaribio ya aina hiyo, huwezi kupata usahihi wa kufaulu au kushindwa kwa kondomu katika kudhibiti maambukizo. Kuhimiza matumizi holela ya kondomu kwa kila mmoja bila kuzingatia kanuni ya msingi halafu kutangaza kuwa matumizi ya kondomu yanapunguza maambukizo ni kuwadanganya wananchi. Kuwaeleze tu kuwa kila mtu atumie kondomu kila wakati na kwa usahihi bila kujua kama ameathirika au hapana ni kutowatendea haki watumiaji. Ingependeza na tunapendekeza kama jambo hili lisingepingana na kanuni za maadili kuwa ili tuwe na uhakika wa kile tunachosema, wahamasishaji na wasambazaji wahimize matumizi ya kondomu katika mazingira ambapo mmoja ni mwathirika na mwingine siyo mwathirika.
Kondomu inaposhindwa kumkinga mtu dhidi ya maambukizo ya virusi vya ukimwi ina maanisha mtu huyo ataambukizwa na anaanza safari ya kifo cha polepole na chenye maumivu makali. Picha tuliyoiweka mwanzoni mwa ukurasa inaeleza hatima ya maambukizo hayo. Idadi ya maambukizo inategemea kiwango cha matumizi na idadi ya kondomu zinazotumika. Sera ya kuhimiza matumizi ya kondomu na kuzuia au kupuuzia njia za kweli za kudhibiti maambukizo ni sera zenye kujikita katika utamaduni wa kifo. Kampeni za mapambano dhidi ya maambukizo ya ukimwi zilenge katika kuondoa maambukizo (Risk Elimination) na siyo kupunguza maambukizo. (Risk Reduction)
Masuala ya kimaadili na kiteolojia kuhusu kondomu
Hoja ya jumla:
Hata kama kondomu ingekuwa na kiwango cha kufaulu kwa asilimia 100 au hata kama itatokea baadaye kuwa imewezekana kutengeneza kondomu zenye uwezo wa kuzuia virusi vya ukimwi kwa asilimia 100, msimamo wetu dhidi ya matumizi ya kondomu kamwe hautabadilika.
Matumizi ya kondomu katika tendo la ndoa [kwa lengo la kuzuia mimba au kudhibiti magonjwa ya zinaa vikiwemo virusi vya ukimwi], huweka kipingamizi na utenganishi kati ya mtu mume na mtu mke. Kwa msingi huo matumizi ya kondomu huvuruga umoja wa miili. Vilevile inaingilia na kuharibu utakatifu wa tendo lenyewe na hivyo kuvunja umoja wa roho. Na pia matumizi ya kondomu hujenga uhusiano wa katao kati ya mwanamke na mwanaume; hakuna anayejitoa kwa mwenzake na hivyo kuharibu umoja wa mioyo.
Kwa asili yake tendo la ndoa lina madhumuni mawili yasiyotenganishwa daima: yaani kujenga na kudumisha upendo kati ya mtu mke na mtu mume; na, uwezekano wa kupasisha uhai mpya. Matumizi ya kondomu huharibu na kutenganisha madhumuni hayo mawili – kuzuia mwunganiko wa upendo wa wanandoa; na kuzuia uwezekano wa kupasisha uhai mpya.
Kondomu hudhalilisha uzazi na nia njema ya tendo la ndoa. Mume humwambia mke ‘nakupenda lakini uzazi wangu sitakupa, nauweka katika huu mpira na nitautupa katika jalala au chooni’. Mke anamwambia mume, ‘nakupenda lakini uzazi wako siutaki, ni uchafu, weka katika mfuko na katupe katika jalala au chooni’. Uzazi wa binadamu, zawadi pekee ya kupasisha uhai mpya, hutendewa kama uchafu na kutupwa mahali pachafu.
Matumizi ya kondomu huharibu uwezo wa utashi wetu katika kushinda matamanio ya mwili. Watumiaji wa kondomu wanatendewa kama vile watu wasiokuwa na akili na utashi, au kwamba kila mmoja ni mwasherati; kila mmoja anafanya, basi kila mmoja atumie kondomu. Ndiyo maana sheria zinatungwa kulinda na kutetea matumizi ya kondomu; kuongea kinyume chake au kutoishabikia kondomu kunachukuliwa kama upinzani na kwamba kunatoa ujumbe tatanishi katika mapambano dhidi ya ukimwi.
Mhamasishaji, mtetezi, msambazaji na muuzaji wa kondomu anatenda dhambi tatu kwa mara moja:
Anashuhudia dhambi ya uongo: kwa kuwadanganya watu kuwa kondomu ni kinga madhubuti; ili hali inajulikana kuwa kuna kiwango cha kushindwa cha asilimia kati ya 10 hadi 20, ni kuwadanganya wananchi; ni kinyume na maadili ya mtu yeyote mwungwana
Anachangia dhambi ya uzinzi na uasherati. Kwa vile tendo la ndoa ni halali ya wanandoa. Kusambaza kondomu kwa wanafunzi mashuleni na vyuoni ni kuwajengea mazingira ya uasherati. Matumizi holela ya kondomu huifanya dhambi ya uzinzi kuwa butu, ni kama haipo.
Anachangia dhambi ya mauaji. Kushindwa kwa asilimia 10 hadi 20 sio jambo la kupuuzia: lina maanisha maafa – kifo. Fikiria kondomu milioni hamsini zinatumika kwa wakati mmoja, asilimia 10 yake ni watu milioni tano wanaoambukizwa kwa wakati mmoja, Na kwa tabia ya kondomu ya kuchochea vitendo vya ngono, hao walioambukizwa nao wataambukiza wengine, na hao wataambukiza wengine, na wengine. Mwisho wake ukimwi unatangazwa kuwa janga la taifa.
Lengo na dhana ya watengenezaji, watetezi na wasambazaji limo katika fikra zao, na kamwe hawalisemi bayana. Lengo hilo ni udhibiti wa idadi ya watu duniani, hasa watu wa dunia ya tatu. Kwao kondomu ni silaha na zana bora sana. Inapozuia mimba kondomu inadhibiti kizazi. Inaposhindwa kuzuia maambukizo ya virusi vya ukimwi, watu wanakufa kwa magonjwa yatokanayo na UKIMWI. Kwa hiyo, watetezi, wahamasishaji na wasambazaji kondomu wanafaulu katika kutimiza lengo lao kwa kuwazuia binadamu wapya kuzaliwa na wale waliozaliwa wanakufa.Hivyo shabaha iliyofichika katika kampeni ya matumizi ya kondomu inakamilika. Na wale wanaolaghaiwa, bila kudadisi hata kidogo, wanafikiri kweli kondomu huzuia maambukizo ya virusi vya ukimwi na kinga dhidi ya uzao wa binadamu. Kumbe, wahenga walipata kusema miaka mingi ya nyuma, KONDOMU NI MWOKOZI MLAGHAI. Anafanya kazi yake sawasawa na Ibilisi katika bustani ya Adeni. Tunapohangaika na namna ya kudhibiti kuenea kwa virusi vya ukimwi, tukiwa tunafahamu fika kuwa asilimia kubwa ya maambukizo hupitia ngono, Ibilisi anatumia ngono hiyo hiyo, akiihamasisha kwa matumizi ya kondomu, ambayo anajua uwezo wake wa kuzuia maambukizo sio wa kiwango cha asilimia mia moja. Tunamsikia akisema “nitumieni mimi nanyi hamtakufa”. Baadhi ya wale waliotumia kweli wamekufa. Kwani hatusomi katika maandiko kuwa mshahara wa dhambi ni mauti? Tukipenda kutokomeza ukimwi tuache dhambi; tubaki waaminifu katika maisha yetu – wale wenye ndoa na wale wasio na ndoa.
Rejea:
Brian Clowes; The Facts of Life, An Authoritative Guide to Life and Family Issues, 2nd Ed. Human Life International, 2001
Brian Clowes & Trujillo Alfonso Cardinal Lopez, The Case Against Condoms, The Scientific and Moral Basis of the Teaching of the Roman Catholic Church on Preventing the Spread of Disease, Human Life International, 2006
Hagamu Emil, Dumisha Utamaduni wa Uhai, Pro-Life Tanzania, 2004