Katika dunia hii yenye mkanganyiko wa mawazo, dhana ya familia inaweza kuelezwa kwa namna mbalimbali kutegemeana na mwelekeo wa falsafa, taaluma na lengo la mfasiri. Katika mada hii tutaeleza familia kama mwunganiko wa mwanaume na mwanamke katika ndoa takatifu na kwa njia ya upendo wa kindoa wanapatikana watoto ambao pamoja na wazazi wao, yaani baba na mama ndio wanaunda familia. Katika mapokeo, mababa wa kanisa na wanatauhidi wameieleza familia kama ile taasisi inayoundwa na mtu –me na mtu –ke. Familia kwa hiyo, ndiyo taasisi ya msingi ya kijamii na ilikuwapo hata kabla ya mamlaka za kijamii kuwapo na ambazo zinapaswa kuitambua. Familia kwa hiyo, ni muunganiko wa watu ambao kuishi na kukaa kwao pamoja ni kwa njia ya "komunioni", yaani ushirika wa kujengana na kukamilishana. Katika familia kila mwanafamilia ana majukumu na wajibu zake ziendanazo na silika yake na umri wake.
Sifa ya familia kwa kadiri ya barua ya Baba Mtakatifu Yohane Paulo II
Familia halisi ni taasisi ya msingi ya jamii inayojengwa katika uhalisi wa binadamu, na yenye kujikita katika muunganiko wa hiari wa mwanaume na mwanamke katika agano la maisha ya ndoa kwa ajili ya:
Kushibisha hamu za moyo wa binadamu za kutoa na kupokea upendo
Kujenga mahusiano ya upendo wa kindoa na kupasisha kizazi kipya
Kuwapokea na kuwalea watoto katika maendeleo yao kimwili, kiroho na kiakili
Kutoa huduma kwa wahitaji mbalimbali, kama vile walemavu, wagonjwa na wazee
c) Wajibu wa wanafamilia
Mwandishi wa barua kwa Waefeso anatujulisha wajibu wa kila mmoja wa watu wanaounda familia – mume, mke na watoto. Mwandishi anatukumbusha kuwa wajibu wa msingi ni ule wa mahusiano, "Kila mmoja amstahi mwenzake kwa sababu ya kumcha Kristo" (Efe.5:21). Huu ndio wajibu wa msingi kwani unatutambulisha na kutushirikisha maisha yetu na Kristo. Baada ya kueleza wajibu huo wa msingi, mwandishi wa barua hiyo anafafanua wajibu wa mume, mke na watoto. Kimsingi wajibu zote zinaegemea tunu za upendo, utii na heshima. Kwa kuzingiatia tunu hizo wanafamilia hukubaliana, huchukuliana, hujengana, kila mmoja kwa manufaa ya mwenzake na kwa manufaa ya pamoja.
Wajibu wa familia kwa jamii unaelezwa vizuri kwa kutambua uhusiano asilia uliopo kati ya familia, ambayo ni sehemu, na ndiyo inayounda jamii kwa upande mmoja, na jamii ambayo huundwa na mkusanyiko wa familia mojamoja kwa upande mwingine. Kwa hiyo bila familia hakuna jamii na kwa upande mwingine familia inaihitaji jamii kwa ajili ya ustawi wake.
2. Upendo na Ukarimu katika familia
Upendo ni tunu na ni nguvu inayowawezesha watu kukua. Katika mpango wa Mungu wa uhai ambao unawakilisha wito wa kila mmoja, upendo ni chanzo azizi cha kujitoa kila mmoja kwa mwenzake ambapo wanaume na wanawake wanaalikwa kutenda kwa ajili ya kujitambulisha wenyewe na kujiletea furaha. Kwa kumwumba mtu kwa mfano wake, Mungu ameandika ndani ya ubinadamu wa kila mwanaume na mwanamke wito, na kwa hiyo uwezo na wajibu wa upendo na ushirika. Upendo kwa hiyo ni wito wa ndani wa kila binadamu. Kila mmoja ameitwa kupenda na kujitoa nafsi. Kila mtu amehuishwa kutoka maelekeo ya kibinafsi kwa kupenda wengine, kwanza wazazi, au wale wenye kuchukua majukumu, hasa Mungu ambaye kutoka kwake upendo wa kweli hububujika. Wanafamilia wanaalikwa kuwa wakarimu kwa zawadi ya upendo wa Mungu kwa binadamu, yaani uhai. Uhai ni zawadi aliyopokea binadamu ili naye aitoe.
Upendo na ukarimu kwa uhai mpya
Katika familia Injili ya Uhai itekelezwe kwa namna kwamba wanafamilia wanajengeka katika upendo na ukarimu kwa uhai mpya. Kwa njia hii wanafamilia watatekeleza amri ya Mungu, "Zaeni mkaongezeke na kuijaza nchi na kuitiisha" (Mwa.1:28). Kila uzao mpya ni zawadi azizi kwa familia. Siyo tu kwamba uzao wa mtoto huongeza idadi ya watu wa Mungu, bali pia kila mtoto huja na baraka na faraja tele, kwani hakuna mtoto anayefanana na mwingine, na wala hakuna atakayezaliwa sawa naye baada yake. Ndiyo maana Mama Bikira Maria alilipokea agizo la Mungu kwa ukarimu, "Ndimi mjakazi wa Bwana, nitendewe ilivyonenwa", (Lk.1:38). Uzao wa mtoto huambatana na furaha na sherehe kwani amekuja duniani binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kwa sababu hiyo wachungaji walishangilia kuzaliwa kwa Yesu, "Utukufu kwa Mungu juu mbinguni na duniani amani kwa watu wenye mapenzi mema" (Lk.2:13-14). Ndiyo, uzao wa mtoto mwingine huleta furaha na amani katika familia. Kila mwanafamilia anapaswa aseme, "Asante Mungu kwa zawadi azizi ya uhai mpya katika familia yetu".
Upendo na ukarimu kwa watoto
Akitafakari upendo na ukarimu kwa watoto katika familia Mzaburi anasema kwa furaha:
"Tazama, wana ndio urithi wa Bwana, Uzao wa tumbo ni thawabu. Kama mishale mkononi mwa shujaa, Ndivyo walivyo wana wa ujanani. Heri mtu yule Aliyelijaza podo lake hivyo Naam, hawataona aibu Wanaposema na adui langoni" (Zab.127:3-5)
Na tena mahali pengine anasema,
"Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao, Vyumbani mwa nyumba yako; Wanao kama miche ya mizeituni Wakiizunguka meza yako, Tazama atabarikiwa yule amchaye Bwana", (Zab.128:3-4)
Jee, katika familia zetu tunaona fahari juu ya watoto tuliowazaa, au tunawaonea aibu? Je, tunajivunia kuwa na watoto wengi, au tunajivunia kuwa na ukame wa watoto. Tunaogopa kuitwa "Bwana Makusanya", au tunaogopa kejeli za "kuzaa kila mwaka". Je watoto tulio nao "wanaizunguka meza?" Au tunaaminishwa kuwa watoto ni balaa ambalo linapaswa kuepukwa kwa njia na gharama yoyote? Tunaifuata amri ya gani; ya Mungu au ya Ibilisi?
Upendo na ukarimu katika malezi ya watoto
Mazingira ya familia ndiyo ya kawaida na halali kwa malezi ya watoto na vijana ili kuimarisha tunu za upendo, kiasi, ujasiri na usafi wa moyo. Kama kanisa la nyumbani familia ni shule iliyojaa utajiri wa ubinadamu.
Katika tafiti za kisayansi zilizofanyika zinaonyesha kuwa mazingira ya nyumbani ndiyo pekee, bora, yenye uwezo wa kutoa elimu kamilifu katika masuala ya ujinsia, katika miaka ya mwanzo ya ukuaji wa mtoto na hasa katika kipindi cha kabla ya kuzaliwa kwa sababu vionjo vya mtoto hujengeka zaidi katika vipindi hivi. Thamani muhimu kwa wazazi wakati huu ni: amani, kukubaliana na kuelewana. Vilevile inahimizwa umuhimu wa mahusiano ya karibu ya mume na mke, kukaa pamoja katika vipindi hivi vya makuzi ya mtoto. Kukosekana kwa mzazi mmoja katika vipindi hivi kunaathiri sana malezi ya watoto. Wakati mwingine matatizo ya watoto yatokanayo na malezi yasiyo kamilifu yanaweza kudumu maisha yao yote. Katika vipindi hivi watoto ni muhimu zaidi kuliko kazi au starehe. Familia ni shule ya mwanzo ambamo maisha ya jumuiya huanza: kama jamii ya upendo, inaonekana katika kanuni ya kujitoa nafsi ambayo huiongoza na kuifanya ikue.
Mazoea ya kujiheshimu na kiasi katika maongezi, matendo na mavazi ni muhimu katika kujenga mazingira mazuri ya makuzi katika usafi wa moyo, lakini hiyo itatawaliwa na nia ya mtu kutawala mwili wake na kuwaheshimu wengine. Wazazi wawe waangalifu kwa mitindo na mitazamo inayoweza kuharibu malezi ya watoto. Matumizi ya vyombo vya habari, kama vile televisheni yadhibitiwe.
Upendo na ukarimu kwa zawadi ya uumbaji
Kila binadamu ameumbwa kipekee na kila mmoja ameumbwa kwa mfano na sura ya Mungu. Mungu amempatia kila mmoja vijenzi vyote vinavyomfanya awe mtu kamilifu – mwenye hadhi na utu kwake mwenyewe na machoni pa wengine. Kwa hiyo ni wajibu wa kila mwanafamilia kuhakikisha kuwa anautunza uumbaji huu wa Mungu bila kuutendea vibaya kwa namna yoyote ile. Wazazi wana wajibu wa pekee katika kuwaelekeza watoto kupambanua kati ya matendo na tabia njema na mbaya. Wanafamilia wasiruhusu uumbaji uingiliwe au uharibiwe na vitu au matendo yaliyo nje ya uumbaji ambayo matokeo yake ni kuvuruga au kuharibu Injili ya Uhai. Katika hili Mzaburi anafurahia na kushukuru juu ya uumbaji wa Mungu kwa maneno haya:
"Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa Kwa jinsi ya ajabu ya kutisha… Mifupa yangu haikusitirika kwako, Nilipoumbwa kwa siri, Nilipoungwa kwa ustadi pande za chini za nchi" (Zab.139:14-15)
Jee, katika familia zetu tunamshukuru Mungu kwa uumbaji wake wa ajabu? Au, je, tunajitahidi kumsahihisha Mungu, tukavuruga Injili ya Uhai kwa matendo yanayoleta madhara, au tukajikatalia ustadi wa Mungu wa uumbaji wake kwa nafsi zetu. Je, hatupendi kuwa kama "fulani", "nywele" hizi alizonipa Mungu sizitaki, nitanunua nyingine kutoka dukani, kwani nitaonekana mzuri"; "ngozi" hii inanipa kinyaa, ningependa ngozi nyingine; "jinsi" hii aliyonipa Mungu inanitesa, ningetamani kuwa jinsi tofauti? Je umeupokea uumbaji wa Mungu kwa upendo na ukarimu?
Upendo na ukarimu kwa uzazi
Mungu amempatia kila binadamu zawadi azizi ya uzazi ambayo kwayo, katika wakati mwafaka na kwa makubaliano ya kiupendo kati ya mtu mume na mtu mke katika ndoa takatifu, unawawezesha kushiriki na Mungu katika uumbaji wa binadamu, mwendelezo wa kizazi. Kwa tendo hili wanadamu wanaitii ile ya amri ya Mungu ya "zaeni mkaongezeke, mkaijaze nchi". Utaratibu wa uzazi katika mwili wa mwanaume na mwanaume umewekwa kwa jinsi kwamba unahitaji ushirikiano na mkamilishano kwa ajili ya kuwezesha tendo la ndoa kutendeka na kuleta uzao. Hata hivyo, Mungu, katika matashi yake, hakupenda wanadamu wazae "kila mwaka" kama ambavyo wengine wamesikika wakisema. Kwa hiyo, katika mwili wa mwanamke Mungu ameratibu uzazi, mithili ya majira na kwa njia hiyo mume na mke wanaweza kuyatumia majira hayo kwa ajili ya kupata uzao au kwa ajili ya kuahirisha uzao. Ndiyo majira ya kiangazi na majira ya masika. Majira ya kiangazi, mwanamke anakuwa mkavu, mithili ya ardhi kavu, kiasi kwamba ukipanda mbegu, hazitaota. Ndiyo wakati mwafaka kwa wanandoa kukutana katika tendo la ndoa kwa ajili ya kushibisha hamu ya upendo wa kindoa. Na katika majira ya masika, udongo umelowa, yaani una unyevunyevu, na kama mkulima atapanda mbegu, kwa hakika zitaota. Ndio wakati wa masika, wakati wa kilimo, yaani kulima na kupanda. Wanandoa wakitumia kiashiria halisi cha ute wa uzazi wanahakika ya kupata uzao wa mtoto, kwani ndio muda mwafaka. Kipindi cha uzazi kwa mwanamke ndio kipindi cha masika, kipindi cha kukutana katika tendo la ndoa kwa wanandoa wanaotaka kupata mtoto. Kwa njia ya mpango huu wa Mungu wa uzazi, wanandoa wanajitoa kila mmoja kwa mwenzake. Kila mmoja anatoa na kupokea upendo kutoka kwa mwenzake.
Hivyo ndivyo Mungu, kutokana na wema na upendo wake alivyopanga uzazi katika mwili wa mwanamke. Lakini Mungu anatudai pia kuvilinda na kuvitunza viungo vya uzazi dhidi ya uharibifu utokanao na sababu mbalimbali. Mungu anatutaka tujiepushe na zinaa kabla ya ndoa na wakati wa ndoa kwani yaweza kusababisha kupata magonjwa ya zinaa yanayoweza kuharibu viungo vya uzazi na hivyo kumfanya mwanamke kushindwa kupata uja-uzito. Vilevile Mungu anatuonya dhidi ya matumizi ya vidhibiti mimba, kama vile vidonge vya majira, sindano, vipandikizi, vitanzi, kondomu na vinginevyo kwani vinaingilia mfumo wa uzazi, kuuchafua na kuuharibu, kuunajisi na hivyo kumfanya mwanamke ama kushindwa kupata mimba, au kuviharibu viungo hivyo, au kumfanya mwanamke kuishi katika huzuni na mateso makubwa. Mume na mke katika ndoa wanaalikwa kuzingatia mpango wa Mungu wa uzazi, ndio ule unaozingatia maumbile. Mpango huu ni rahisi sana kuufuata na unaleta manufaa mengi kwa wanandoa na familia. Injili ya Uhai inadhihirishwa na familia zile zinazoruhusu mpango wa Mungu kutawala maisha ya ndoa.
Kila mwanafamilia leo ajiulize, amejiweka mbali na Mungu kiasi gani kwa kuukataa mpango wake wa uzazi na kukumbatia mpango haribifu wa uzazi ambao unabomoa maisha mazuri ya wanafamilia. Katika mpango haribifu wa uzazi kila mmoja anaishi kwa nafsi yake. Mke anamwogopa mume wake kiasi kwamba anamwekea tahadhari katika maisha ya kindoa. Wakati wowote wa tendo la ndoa mke anamwambia mume wake, "nitakupa mwili wangu, lakini sitakupa uzazi wangu, nimeuharibu". Anamwambia vilevile, "nitakupa akili yangu, lakini sitakupa moyo na roho yangu".
4. Vitisho dhidi ya uhai katika familia
Ibara ya 7 katika Injili ya Uhai inatupatia maelezo mazuri juu ya asili ya ubaya na kifo.
"Mungu hakufanyiza mauti, wala haimpendezi walio hai wakipotea. Kwa maana aliviumba vitu vyote ili vipate kuwako… Mungu alimwumba mwanadamu ili apate kutokuharibika, kwa mfano wake mwenyewe, ila ulimwengu uliingiwa na mauti kwa husuda yake shetani, nao walio wa upande wake hupata kuionja" (Hek.1:13-14; 2:23-24).
Kihoro cha kifo kinachouvamia ulimwengu na kuchafua maana ya maisha ya mtu ni kinyume cha Injili ya Uhai, iliyotangazwa mwanzoni kabisa mwanadamu alipoumbwa kwa mfano wa Mungu, kwa ajili ya utimilifu na ukamilifu wa uhai (Mwa. 2:7; Hek.9:2-3). Mauti iliingia ulimwenguni kwa husuda ya shetani, (Mwa.3:1, 4-5) na dhambi ya wazazi wetu wa kwanza (Mw.2:17, 3:17-19). Tena mauti iliingia duniani kikatili kwa njia ya Kaini kumwua Abel nduguye, (Mwa.4:8).
Mauaji yaliyotapakaa ulimwenguni leo ni matokeo ya dhambi iliyoletwa kwetu kwa husuda ya Shetani. Vita vinavyopiganwa pande zote za dunia ni kinyume na mpango wa Mungu katika Injili ya Uhai. Mungu alipendezwa na binadamu kuwa na uzima, tena ulio mkamilifu. Katika habari ya Kaini kumwua nduguye Abel, Maandiko Matakatifu yanaonyesha kuwepo kwa hasira na wivu ndani ya mtu tangu mwanzo wa historia ya mwanadamu, matokeo ya dhambi ya asili. Mwanadamu kawa adui wa mwanadamu mwenziwe. Katika vita vya leo duiani, taifa huliinukia taifa jingine, kabila kwa kabila jingine, ndugu kwa ndugu yake, mama kawa mtoto wake. Katika matukio haya ya vita, familia zinaathirika vibaya kwa kutenganishwa wanafamilia, wimbi la wakimbizi na hata vifo ndani ya familia. Hali hii inafuta picha nzuri ya Injili ya Uhai katika familia. Kila mauaji ni uvunjaji wa ujamaa wa "kiroho" unaowaunganisha wanadamu katika familia moja kubwa ambamo wote hushiriki haki moja ya msingi, yaani usawa katika utu. Sauti ya damu iliyomwagwa na watu inaendelea kulia kizazi hata kizazi, daima kwa namna mpya na tofauti. Vitisho vingine vinatokana na uzembe wa kutojali uhai wa wengine; vingine vinatokana na jeuri, chuki na migongano ya kimaisha. Aidha, vitisho dhidi ya uhai wa mwanadamu siku hizi vinaendelea kujitokeza kwa namna nyingi, zilizo wazi na zisizo wazi
Utoaji mimba unaharibu ujamaa wa kimwili, kwani uhusiano baina ya watoto na wazazi huvunjika. Kila tendo la kikatili dhidi ya jirani (hasa jirani aliyemo katika tumbo la uzazi la mama) linakuja kwa kuyakubali "mawazo" ya yule mwovu, yeye, "aliyekuwa mwuaji tangu mwanzo" (Yoh.8:44). Watu sasa hawaelekei tena kuyaangalia maovu ya namna hii kama uhalifu. Tena, ni jambo la kushangaza kwamba maovu haya sasa yanachukua sura ya "haki". Watu wamefikia mahali, wanathubutu kuzitaka serikali zao ziidhinishe vitendo hivi viovu kisheria, kwamba upatikanaji wake eti uwe ni wa kawaida kwa njia ya huduma huria ya wataalamu wa tiba. Ni suala linalohusu mashambulizi dhidi ya uhai katika hali yake dhaifu kabisa, wakati uhai unapokosa kabisa uwezo wa kujitetea. Ni jambo la kusikitisha kwamba mara nyingi hata familia ambayo wito wake wa msingi ni kuwa "hifadhi takatifu ya uhai" inahusika na hujuma hii dhidi ya uhai. Yote haya yanadokeza, walau kwa kiasi fulani, jinsi thamani ya uhai inavyoweza kufifia. Hata hivyo, sauti ya dhamiri inaendelea kutukumbusha juu ya thamani kuu ya uhai kama tunu takatifu.
Lakini Mungu hawezi kuuacha uhalifu utendeke bila kuuadhibu: kutoka ardhini, damu ya yule aliyeuawa inamdai Mungu atoe haki (Mwa.37:26; Isa.26:21; Eze.24:7-8). Kwa kadiri ya tamaduni nyingi, damu ni chemchemi ya uhai, hasa wa mwanadamu, ni mali ya Mungu peke yake: kwa sababu hii yeyote anayeushambulia uhai wa mwanadamu kwa namna fulani anamshambulia Mungu Mwenyewe. Dhambi ya mauaji ya kukusudia inaingia katika "dhambi zinazomlilia Mungu atoe haki". Kwa hiyo yeyote aliyewahi kuua, anayeua na atakayeua kwa kutoa mimba anakabiliwa na dhambi hii na anabeba laana kama vile Mungu alivyombebesha laana Kaini baada ya kumwua nduguye Abel.
Vidhibiti mimba
Ili kueneza utoaji mimba kwa urahisi, kiasi kikubwa cha pesa kinawekezwa katika uzalishaji wa madawa au vidhibiti mimba. Lakini kwa vile lengo la madawa haya ni kuushambulia uhai mchanga katika hatua zake za mwanzo, madawa hayo yanatengenezwa kwa namna kwamba utendaji wake sio ule wa kuzuia/kudhibiti mimba, bali kutoa mimba. Sisi watu wa Utamaduni wa Uhai, tunaviita vidhibiti mimba hivyo "viua uhai". Baadhi ya madawa hayo ni "emergency pill", "RU486", na mengineyo mengi. Tusisahau ukweli kwama vidonge vya majira vya sasa hufanya kazi kama viua-uhai badala ya kuwa vidhibiti mimba, na hiyo ni pamoja na "depo provera" na "norplant". Vilevile tufahamu kuwa, vitanzi mara zote hutoa mimba; kamwe havizuii mimba kutungwa.
Matumizi ya vidhibiti mimba huondoa uwajibikaji wa uzazi unaojali (unaoheshimu) thamani halisi ya tendo la ndoa – hatimaye hustawisha fikra za chuki dhidi ya mtoto anayetungwa tumboni mwa mama yake. Na tufahamu ukweli kuwa tabia ya utoaji mimba imestawi zaidi pale ambapo watu wanatumia sana vidhibiti mimba. Na kwa mtazamo wa kimaadili udhibiti mimba na utoaji mimba ni maovu ya aina mbili tofauti: la kwanza linapingana na maana halisi ya tendo la ndoa kama kielelezo halisi cha upendo wa maisha ya ndoa, wakati la pili linaharibu uhai wa mtu. Aidha la kwanza linapingana na fadhila ya usafi wa moyo wakati la pili linapingana na fadhila ya haki na linakiuka moja kwa moja amri ya Mwenyezi Mungu, "usiue".
Lakini, licha ya kuhitilafiana kwao katika uzito wa ubaya wa kimaadili, hayo yote ni mambo mawili yenye uhusiano wa karibu sana, na kama vile matunda ya mti mmoja. Vidhibiti mimba vinatumika kwa visingizio mbalimbali, "hali ngumu ya maisha”, "kuabudu sana anasa" ambayo inajenga dhana ya uhuru pasipo kuwajibika. Kwa hiyo mimba yoyote itakayopatikana wakati mwanamke anatumia vidhibiti mimba itauawa kwa sababu lengo la tendo la ndoa halikuwa kupokea uhai mpya.
Katika kundi la vidhibiti mimba tunaweza kuongeza uzalishaji wa madawa, vifaa mbalimbali pamoja na chanjo. Vitu hivi vyote ambavyo vinaharibu uhai wa mwanadamu katika hatua zake za awali kabisa vinasambazwa kwa wepesi kabisa kama ilivyo kwa madawa ya kuzuia mimba kwa nguvu ya fedha na utashi wa kisiasa kwa watawala nchi. Tunaweza vilevile kuongeza vitendo vya kufunga kizazi vinavyoendeshwa kwa kampeni kubwa katika nchi zinazoendelea kwa sasa.
Vitisho dhidi ya uhai vinafanyika pia kwa njia za kiteknolojia ambazo kwa juujuu zinaonekana kuhudumia uhai lakini kwa undani wake zinaharibu uhai wa mwanadamu. Njia hizo zinahusu kuzalisha binadamu katika maabara na kuchagua walio na nguvu na afya na kupandikiza katika matumbo ya mama ambao walikuwa na matatizo ya uzazi. Njia hizo sio tu kwamba hazikubaliki kimaadili kwa vile zinatenganisha uzazi na mazingira yake ya tendo la ndoa, lakini pia ni njia zenye uwezekano mkubwa wa kushindwa, siyo tu katika utungaji wa uhai mpya bali pia katika kuukuza na kuundeleza uhai huo. Zaidi ya hayo idadi ya binadamu wanaotengenezwa ni kubwa kuliko idadi ile inayohitajika, na idadi kubwa ya binadamu wanaobakia kama "akiba" huteketezwa au kutumika kwa ajili ya majaribio ya kisayansi kwa kisingizio cha maendeleo ya kisayansi au tiba. Njia hii humdhalilisha binadamu kwa kumfanya afanane na kitu cha kibaolojia tu, anayeweza kutengenezwa, kuuawa au kuhifadhiwa katika majokofu.
Yutanasia. Watu wenye magonjwa sugu na wale wanaokabili vifo nao wanakabiliwa na vitisho vikubwa. Katika mazingira ya kijamii na kitamaduni ambamo watu wanaona vigumu sana kukubaliana na hali halisi ya mateso, kipo kishawishi kikubwa kutaka kuondokana na hili kwa njia za mkato, kwa kuharakisha kifo, au kukatisha uhai. Zipo sababu kadhaa zinazowezesha kufikia hatua ya kuwaua watu wa aina hiyo. Kwa upande wa mgonjwa mwenyewe anaweza kukabiliwa na mahangaiko, kukata tamaa kutokana na mateso ya muda mrefu. Hivyo mtu mwenyewe au hata familia wanaweza kushawishika kufikia hatua ya kukatisha uhai wa mgonjwa huyo. Wale wanaowahudumia wagonjwa wanaweza kusukumwa na huruma potovu na hivyo kushawishika kukatisha uhai wa mgonjwa. Kwa jumla, utamaduni wetu wa leo umeathiriwa na hali fulani ambayo inamfanya mtu kudhani kwamba anaweza kuudhibiti uhai na kifo na kujitwalia mikononi mwake madaraka yote juu yake. Mtazamo huu ndio unaopelekea kuwaua watu kwa kuwahurumia – kifo cha huruma – yutanasia. Watu wanaouawa kwa njia hii ni watu wenye magonjwa sugu, watoto walemavu [tumboni au baada ya kuzaliwa], vikongwe na wengine ambao uwepo wao huhatarisha maisha ya wengine.
Ushoga na umame
Vitisho vingine dhidi ya uhai vinaweza kujificha katika nadharia na matendo kadhaa kiasi cha kushindwa kuviona. Hetu tuangalie nadharia na matendo ya ushoga. Ushoga ni hali ya mvuto wa kimapenzi wa watu wa jinsi moja na ambayo, kwa siku hizi zetu yamepelekea kudai haki ya hao mashoga kuishi pamoja kama mume na mke. Kimaadili ushoga haukubaliki kwa vile unavunja mpango wa Mungu wa uzazi na maagano ya ndoa kati ya mtu mume na mtu mke. Vilevile vitendo vya ngono vya mashoga vinapingana na amri ya Mungu ya "zaeni mkaongezeke na kuijaza nchi". Zaidi ya hayo ushoga umezaliwa katika ukengeushaji wa kiakili, ambapo, kwa silika ya uumbaji, mvutano wa kimapenzi ni haki na halali kati ya mtu mume na mtu mke. Mashoga walianza kama kundi dogo katika kila jamii, lakini katika miaka ya hivi karibu wamepata nafasi ya kusikiwa na kutetewa na serikali kadhaa na mashirika ya kimataifa na hata Umoja wa Mataifa. Mashirika ya kishoga yameanza kuwepo duniani tangu miaka ya 1912 na sasa yameenea duniani kote. Ni hivi juzi tu, Umoja wa Mataifa umeutambua Umoja wa Mashoga Duniani na kuupa hadhi ya uwakilishi katika umoja huo. Umoja huo unaitwa "The International Gay and Lesbian Human Rights Commission" (IGLHRC) Umame ni nadharia iliyozaliwa kutokana na mapinduzi ya viwanda huko Ulaya, ikapata nguvu katika siasa za Kikomunisti za akina Lenin na Karl Marx. Umame ni itikadi iliyozaliwa miongoni mwa wanawake wanaopigania siyo tu haki za wanawake, bali pia usawa kati ya wanaume na wanawake katika nyanja zote za maisha. Katika mtazamo wake wa ndani na katika itikadi yake umame unakataa ndoa, familia, uzao na malezi ya watoto. Wamame wanapigania uwakilishi sawa katika serikali, bunge, mahakama na taasisi zote za kijamii. Katika mtazamo wa umame, uzazi na umama ni vitu vilivyopitwa na wakati na vinaleta mateso kwa wanawake na kuwafanya washindwe kufaidi maendeleo na starehe za dunia. Mwanamke amezaliwa ili afurahie maisha bila adha ya uja-uzito, kunyonyesha na kulea. Umame unadai kuwa dunia imetawaliwa na mfumo dume tangu kuumbwa kwake, na hivyo ni mfumo unaopaswa kubomolewa. Mwanaume anaonekana kuwa ni mkandamizaji, mtesaji, mnyanyasaji wa mwanamke. Hivyo jitihada zifanyike kuvunja mfumo na mateso haya. Uzao wa watoto upatikane kwa njia nyingine za kimaabara. Tangu miaka ya 1914 Wamame katika nchi za Magharibi walianzisha vyama vya kupigania ukombozi wa wanawake, wakilaani ndoa, kuzaa, kulea na majukumu yatokanayo na umama. Hadi hivi karibuni wanawake walikuwa na vyama vinne vilivyowawakilisha katika Umoja wa Mataifa - the United Nations Development Fund for Women (UNIFEM), the International Research and Training Institute for the Advancement of Women (INSTRAW), Division for the Advancement of Women (DAW) and the Office of the Special Advisor on Gender Issues and Advancement of Women (OSAGI).
Lakini majuma machache yaliyopita, Umoja wa Mataifa umeridhia kuundwa na kuwakilishwa chama kimoja cha wanawake chenye nguvu zaidi kiitwacho "Centre for Women's Global Leadership". Haya ni matokeo ya jitihada za umame zenye lengo la kupigania haki na hadhi ya wanawake duniani, wakiendeleza sera za utoaji mimba, vidhibiti mimba, kufunga kizazi, ushoga na matendo yanayozishambulia imani na taasisi za kidini na tamaduni za watu katika nchi mbalimbali.
g) Tukifikiria jinsi vitisho dhidi ya uhai vinavyoenea kwa kasi duniani, huku tukitambua tunachofahamu ni sehemu tu ya hali halisi, na kwa upande mwingine jinsi mambo haya yanavyokubalika na jamii kwa urahisi na kwa kiasi kikubwa, kama vile kuidhinisha sheria za kutoa mimba, kuhusika kwa wanataaluma wa sekta ya afya, wanasheria, na hata wanadini, tunaona wazi kuwa jamii ya wanadamu leo hii wanatutengenezea dunia ya kutisha. Kwa kadiri vitisho hivyo dhidi ya uhai vinavyoenea duniani, ndivyo hivyo Injili ya Uhai katika familia inavyodhohofika kiasi kwamba familia zenyewe zinasambaratika. Kusema kweli tunakabiliwa na hila dhahiri dhidi ya uhai, ambazo zinazishirikisha hata taasisi za kimataifa zinazohimiza na kufanya kampeni mahsusi kuhalalisha utoaji mimba, matumizi ya vidhibiti mimba, kufunga kizazi na hata kutukuza utasa. Maneno mazuri na matamu lakini yenye kubeba hila bayana yanatumika kuwalaghai watu wa ulimwengu huu – maneno kama, afya ya kizazi, afya ya ujinsia, haki za wanawake, uhuru wa wanawake, mikataba ya kimataifa, na kadhalika yanatumika kujenga ukubalifu. Vyombo vya habari vinatumika kikamilifu kueneza dhana na matendo ya utamaduni wa kifo.
5. Kujenga utamaduni mpya wa uhai wa mwanadamu katika familia
Tupo kwa ajili ya huduma ya Injili ya uhai ambayo kiini chake ni Yesu Kristo mwenyewe. Tunatambua, kama familia, kuwa tumeipokea kama zawadi na tumetumwa kuitangaza kwa watu wote, hata kwenye miisho ya dunia (Mate.1:8). Kwa unyenyekevu na shukrani tunajitambua kuwa sisi tu watu hai kwa ajili ya uhai na tunataka kila mtu atuelewe hivyo.
Familia zimetumwa kuuhudumia uhai na huu ni wajibu wetu unaotokana na hali yetu kama watu wa uhai. Katika safari yetu tunatiwa nguvu na kuongozwa na sheria ya upendo, upendo ambao kiini na kielelezo chake ni Mwana wa Mungu aliyetwaa ubinadamu, ambaye "kwa kifo chake ameupatia ulimwengu uhai".
Kila mmoja katika familia anao wajibu wa kutoa mchango wake kwa ajili ya uhai. Na wote kwa pamoja tunalitambua jukumu letu la kuihubiri Injili ya Uhai, kuiadhimisha katika maisha yetu na kuihudumia kwa njia ya programu na mifumo mbalimbali inayosaidia kustawisha uhai.
Familia inao wajibu mahsusi katika maisha yote ya wanafamilia tangu kuzaliwa hadi kufa. Familia ya kweli "hifadhi takatifu ya uhai", ni mahala ambapo uhai unaweza kupata 'karibu ya kweli na kukingwa dhidi ya mashambulizi na hivi kuwezeshwa kukua katika misingi halisi ya kiutu'. Familia ni muhimu hivi kwamba nafasi yake katika kuujenga utamaduni wa uhai haiwezi kuchukuliwa na kitu kingine. Zaidi ya hayo familia inapowalea watoto inatekeleza utume wake wa kuitangaza Injili ya Uhai. Kwa maneno na matendo ya kila siku na mahusiano ya wanafamilia, wazazi wanawaongoza watoto wao kwenye uhuru halisi unaodhihirika katika kujitoa nafsi, na wanakoleza ndani yao tabia ya kuwajali watu wengine pamoja na haki zao, ukarimu, ushirikiano na moyo wa kuhudumia.
Familia inaadhimisha Injili ya Uhai kwa sala za kila siku, sala ya binafsi na za familia. Familia inasali ili kumtukuza na kumshukuru Mungu kwa zawadi azizi ya uhai, pia kuomba mwanga na nguvu yake ili kuwezeshwa kuhimili nyakati za shida na mateso bila kukata tamaa. Kazi ya kuihudumia Injili ya Uhai itafanikishwa na familia katika kushirikiana na familia nyingine, kwa kujiunga na vyama au aina nyingine ya umoja unaoziunganisha familia mbalimbali, kuhakikisha kwamba sheria na taasisi za serikali hazikiuki haki ya mtu kuishi, katika ngazi zote za uhai wa mwanadamu, yaani tangu kutungwa mimba hadi kifo.
Kitaifa tunahitaji kuleta mageuzi ya kitamaduni. Kinachohitajika sasa hivi ni kuhamasisha ujenzi wa urazini sahihi na bora katika dhamiri za watu, na msimamo wa pamoja katika masuala ya kimaadili na kuendesha kampeni kabambe za kuustawisha uhai. Ni lazima tuungane pamoja kuujenga utamaduni mpya wa uhai. Tunahitaji kuanza mageuzi ya utamaduni wa uhai ndani ya jumuiya zetu wenyewe, yaani jumuiya zetu za kikristo. Hatua ya kwanza na ya msingi kuelekea kwenye mageuzi haya ya kiutamadunini ni kujenga dhamiri inayotambua thamani kuu na yenye hadhi kutoingiliwa, ya uhai wa mwanadamu. Sote tufanye hivyo kwa kutambua kuwa mwanadamu ni kiumbe ambaye Mwenyezi Mungu amemwumba na kumjalia uhai kama zawadi na kama wajibu. Ndiyo kusema, maisha ya mwanadamu yanategemezwa na Mungu.
Uundaji wa dhamiri safi ni kazi ya malezi. Lipo hitaji la malezi kuhusu thamni ya uhai hasa katika misingi yake, yaani upendo na jinsia. Malezi haya yaambatane na ustawishaji wa fadhila ya usafi wa moyo, yaani vijana waheshimu na kuijali miili yao kwa manufaa yao na ya wengine. Kazi ya kulea kwa ajili ya kuuhudumia uhai ni pamoja na kuwaelimisha wau wa ndoa kuusu uzazi wenye kuwajibika, yaani kuishi kwa kadiri ya mpango wa Mungu wa uzazi.
Kwa namna ya pekee wanawake wana nafasi muhimu katika kuleta mageuzi yenye kuwezesha kujengwa utamaduni wa uhai, iwe ni kifikra au kiutendaji. Wanawake waelekezwe katika kuona thamani azizi inayobebwa na umama wao, na kutokomeza dharau ya kijinsia, 'U-mama unaunganika kwa namna ya pekee na fumbo la uhai…. Uhusiano anaokuwa nao mama na kiumbe kinachokua katika mwili wake, unamjengea tabia ya kuwa na maelekeo kwa watu, siyo tu kwa watoto wake bali hata kwa watu wengine, na hii ndiyo ishara dhahiri ya utu wa mwananmke'
Mama anamkaribisha na kumchukua ndani mwake kiumbe – mwanadamu mwingine, anamjali kama mtu huku akimpa hifadhi na kumpatia nafasi ya kukua ndani mwake. Mama anaupokea uja-uzito kwa upendo na shukrani kubwa.
Tunafahamu kuwa waliopania kuendeleza "utamaduni wa kifo" wana rasilimali kubwa na nyingi zaidi kuliko wale wanaojenga "utamaduni wa uhai na mapendo". Pamoja na hayo sisi tunamtegemea Mungu katika yote tutendayo. Kutokana na ukweli huu tunaalikwa kusali kwa ajili ya kuuombea uhai. Sala hii isikike na kuenea duniani kote. Tukifanya jitihada kubwa katika sala za kila siku, sauti ya maombi inayosikika kutoka kila jumuiya ya kikristo, vikundi na vyama mbalimbali, familia na kutoka katika mioyo ya waamini, hatimaye imfikie Mwenyezi Mungu aliye Mwumbaji na mpenda uhai.
Imetayarishwa na kuwasilishwa nami
Emil Hagamu
Mkurugenzi, Pro-Life Tanzania
Human Life International Regional Coordinator for Anglophone Africa